INFANTINO WIKI HII KUKUTANA NA VIONGOZI WA SOKA AFRIKA HUKO JO’BURG na HARARE!

>>NI MPANGO KUMNG’OA ISSA HAYATOU CAF?

FIFA-CAF-BIFURAIS wa FIFA, Gianni Infantino, Wiki hii inayokuja anatarajiwa kukutana na Marais wa Vyama vya Soka Afrika zaidi ya 50 huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Viongozi wote wa juu wa Nchi 54 Wanachama wa FIFA kutoka Afrika wamealikwa kwenye Mkutano huo wa Siku moja ulioitwisha na Infantino ambao utajadili mambo kadhaa ikiwemo hatua ya FIFA kuzipanua Fainali za Kombe la Dunia kuwa na Timu 48 na pia mabadilko kuhusu Mipango ya Maendeleo.

Mikutano hiyo itakuwa Miwili na Siku ya Kwanza Viongozo 25 wa Afrika watakutana na Infantino na Kundi jingine kukutana nae Siku ya Pili.

Hatua hii ya Infantino ni kinyume na desturi kwani kawaida FIFA hukutana na Viongozi wa Afrika kupitia Rais wa CAF, Issa Hayatou, na Kamati ya Utendaji yake.

Mikutano hiyo ya Johannesburg itafuatiwa na tripu ya Infantino huko Harare, Zimbabwe ambako atakutana na Rais wa Chama cha Soka cha Zimbabwe, Philip Chiyangwa, pamoja na Kundi la Viongozi wengine wa Soka Afrika waliolikwa mahsusi kwa kile kilichodaiwa kuhudhuria Bethdei Pati ya Mzimbabwe huyo.

Lakini Philip Chiyangwa ni Mpinzani mkubwa wa Issa Hayatou na anamuunga mkono Mgombea kutoka Madagascar, Ahmad, ambae atachuana na Hayatou kwenye Uchaguzi wa Rais wa CAF utakaofanyika huko Addis Ababa, Ethiopia hapo Machi 16.

Hayatou, mwenye Miaka 70, anasaka tena Urais ili abakie madarakani kwa Miaka 30 sasa tangu alipoanza Mwaka 1988.

Wiki iliyopita ilidaiwa Hayatou ametishia kumchukulia hatua Chiyangwa ikiwa ataendelea na Mkutano huo wa Harare ambao Mzimbabwe huyo amesisitiza ni Bethdei Pati na si kingenecho.

Lakini Wachambuzi wa Soka wanahisi kuwepo kwa Infantino huko Harare ni kumkubali Mpinzani wa Hayatou kwenye Uchaguzi wa CAF.

Mwaka Jana, Hayatou na CAF, ilimuunga mkono rasmi mpinzani wa Infantino kwenye Uchaguzi wa Rais wa FIFA, Sheikh Salman bin Ebrahim al Khalifa wa Baharin, ambae, hata hivyo, alibwagwa na Infantino.

REFA CLATTENBURG AIMWAGA LIGI KUU ENGLAND KWENDA SAUDIA!

REFA-MARK-CLATTENBURG-SITMark Clattenburg ameacha kuwa Refa wa EPL, Ligi Kuu England, baada ya kupata wadhifa mwingine huko Nchini Saudi Arabia.

PGMOL, Professional Game Match Officials Limited, Taasisi ya Marefa huko England imetamka Refa huyo mwenye Miaka 41 amepata kazi huko Shirikisho la Soka la Saudi Arabia.

Clattenburg, ambae ndie aliendesha Fainali za UCL, UEFA CHAMPIONZ LIGI, FA CUP na EURO 2016, Msimu uliopita, aliwasilisha ombi lake la kung’atuka toka PGMOL tangu Desemba.

Clattenburg aliwekwa kwenye Listi spesheli ya Marefa wa PGMOL wanaochezesha EPL tu tangu 2004 na kutumikia kwa Miaka 12 kwenye Ligi hiyo.

Lakini, Mwaka 2008 na 2009, aliwahi kufungiwa Miezi 8 baada ya PGMOL kugundua kuna hitilafu kuhusu kazi zake nje ya Urefa.

Mwaka 2012, Chelsea iliwahi kumshitaki kwa kuwa Mbaguzi dhidi ya Mchezaji wao kutoka Nigeria Jon Obi Mikel wakati wa Mechi na Manchester United lakini alisafishwa tuhuma hizo.

Mwaka 2014, Clattenburg alipewa onyo na Mkuu wa PGMOL Mike Riley kwa kukiuka Maadili ya Kirefa kwa kuongea kwa Simu na Meneja wa Crystal Palace mara baada ya Mechi kati ya Palace na West Brom na pia kuondoka Uwanjani kutoka kwenye Mechi hiyo bila kuambatana na Marefa wenzake kinyume na taratibu za Marefa chini ya PGMOL.

UJIO WA JESUS: GUARDIOLA ‘AMWONYESHA MLANGO’ AGUERO!

AGUERO-JESUSPEPPep Guardiola amesema anataka Sergio Aguero abakie Manchester City mwishoni mwa Msimu huu lakini hana hakika kama Straika huyo kutoka Argentina atabikia.

Katika Wiki za hivi karibuni, Aguero amekosa namba katika Kikosi cha City hasa baada ya kuanza kucheza kwa Straika wa Brazil Gabriel Jesus.

Licha ya kupasua kuwa Aguero ni Mchezaji mzuri na muhimu kwa City, lakini Guardiola ameshindwa kutamka kwa uhakika kama Straika huyo mwenye Miaka 28 atabakia City mwishoni mwa Msimu.

Akiongea na Wanahabari, Guardiola alitamka: “Mwishoni mwa Msimu sijui. Najua ni ngumu kupata Wafungaji wa kiwango cha juu na napenda abakie lakini sijui itakuwaje!”

Aguero, ambae ana Mkataba na City hadi 2020, ameifungia Klabu hiyo Mabao 154 tangu ajiunge nao 2011.

Wiki ilyopita, Aguero mwenyewe alibainisha hakuna uhakika kuhusu hatima yake na kutupa Mpira kwa Klabu na kusema ndiyo itakayoamua.

Nae Guardiola alikoleza kutokuwa na uhakika huo kwa kutamka: “Sababu za kutocheza Mechi 2 zilizopita ni kuwa Leroy Sane, Jesus na Raheem Sterling sasa wanacheza vizuri mno. Hiyo ndiyo sababu pekee Aguero hachezi!”

Leo City wako Ugenini huko Fitness Firt Stadium kuivaa Bournemouth katika Mechi ya EPL, Ligi Kuu England na ushindi kwao utawaweka Nafasi ya Pili wakiwa Pointi 8 nyuma ya Vinara Chelsea.

LALLANA – UKOSEFU UZOEFU USHINDI ‘UNALAANI’ KUZOA UBINGWA!

LIVER-LALLANAKIUNGO wa Liverpool Adam Lallana ameungama kuwa kukosa kwao uzoefu wa ushindi wakati wakiwa hawapo vyema ndio ‘kunalaani’ azma yao ya kutwaa Ubingwa wa England.

Juzi Liverpool walichapwa na Hull City na kutupwa Nafasi ya 5 kwenye EPL, Ligi Kuu England, wakiwa Pointi 13 nyuma ya Vinara Chelsea.

Liverpool, chini ya Meneja Mjerumani Jürgen Klopp, hawajashinda hata Mechi 1 ya EPL Mwaka huu 2017 na kutupwa nje ya 4 Bora kwa mara ya kwanza tangu Septemba 24.

Kabla ya Mechi na Hull, Liverpool, wakiwa kwao Anfield, walitoka Sare na Vinara Chelsea na hilo lilitegemewa kuwafanya wageuke na kuanza kupata ushindi lakini hadithi ikawa nyingine.

Kipigo toka kwa Hull kimeendeleza mwenendo wao wa kufungwa na Timu ‘dhaifu’ kama vile walivyofanywa Msimu huu na Timu zilizo Nafasi za 9 za mwisho ambazo ni Burnley, Bournemouth, Swansea City na hiyo Hull.

Lallana amekiri kuwa kukosa uzoefu kunawaathiri.

Ametamka: “Unaona uzoefu wa Chelsea, wanajua kushinda hata kama hawachezi vyema. Kwetu James Milner pekee ana uzoefu wa kutwaa Ubingwa alipokuwa Man City. Inabidi tujifunze toka kwake.”

Hata hivyo, Lallana amejipa moyo: “Sidhani Chelsea washatokomea na Ubingwa lakini Liverpool inabidi iwe bora zaidi. Mbio za Ubingwa zinaanza Machi!”

 

TOKA TFF: KEMONDO SUPER YASHUSHWA MADARAJA MAWILI, ASFC RAUNDI YA 6, KOCHA MOROCCO ‘JELA’ MECHI 3!

PRESS RELEASE NO. 250                                     FEBRUARY 06, 2017

KUSHUSHWA DARAJA KEMONDO SUPER FC

TFF-HQ-1Timu ya Kimondo Super SC imeshushwa madaraja mawili (hadi Ligi ya Mkoa), na matokeo ya mechi zake zote ilizocheza katika kundi la B yamefutwa kwa kushindwa kufika uwanjani kucheza mechi dhidi ya JKT Mlale bila sababu za msingi.

Mechi hiyo namba 47 (JKT Mlale vs Kimondo Super SC), ilitakiwa kuchezwa Januari 28, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, lakini Kimondo Super SC haikutokea uwanjani wala kutoa taarifa yoyote hadi Februari 1, 2017 ilipotuma taarifa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), na kutoa sababu ambazo hazikukubaliwa na Kamati.

Pia Kimondo Super SC imetozwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambapo kati ya hizo sh. 1,000,000 (milioni moja) itachukuliwa na TPLB, na sh. 1,000,000 (milioni moja) italipwa JKT Mlale. Adhabu dhidi ya Kimondo Super SC ni utekelezaji wa Kanuni ya 28(1) na (2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

RAUNDI YA SITA AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017

Raundi ya Sita ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup – 2016/17, itaanza Februari 24, 2017 kwa michezo minne kuchezwa kwa siku hiyo kuanzia saa 10.00 jioni kasoro mchezo mmoja tu utakaopigwa saa 1.00 jioni.

Michezo hiyo kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT Ruvu ya Pwani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilihali Azam na Mtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala – mchezo utakaofanyika saa 1.00 usiku.

Jumapili Februari 26, mwaka huu timu ya Mbao FC itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Jumatano Machi 1, 2017 Simba SC itacheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam wakati Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

KOCHA MOROCCO AFUNGIWA MECHI TATU

Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72), imemfungia Kocha wa Stand United, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kushiriki michezo mitatu uwanjani na faini ya Sh 500,000 (laki tano).

Katika mechi Na. 160 ya Ligi Kuu ya Vodacom uliozikutanisha timu za JKT Ruvu na Stand United iliyochezwa Januari 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Morocco aliondolewa kwenye benchi (Ordered off) kwa kosa la kupiga maamuzi ya mwamuzi na kutoa lugha chafu.

Kamati hiyo ya Saa 72 imechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 40 (11) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Makocha. Morocco hata kama atakuwa amemaliza mechi tatu nje ya benchi, hataruhusiwa kukaa kwenye benchi hadi awe amelipa faini hiyo.

Adhabu hiyo ya Morocco itaendelea kumhusu hata kama utakuwa umehamia kwenye timu nyingine na katika msimu mwingine wowote.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)