LALLANA – UKOSEFU UZOEFU USHINDI ‘UNALAANI’ KUZOA UBINGWA!

LIVER-LALLANAKIUNGO wa Liverpool Adam Lallana ameungama kuwa kukosa kwao uzoefu wa ushindi wakati wakiwa hawapo vyema ndio ‘kunalaani’ azma yao ya kutwaa Ubingwa wa England.

Juzi Liverpool walichapwa na Hull City na kutupwa Nafasi ya 5 kwenye EPL, Ligi Kuu England, wakiwa Pointi 13 nyuma ya Vinara Chelsea.

Liverpool, chini ya Meneja Mjerumani Jürgen Klopp, hawajashinda hata Mechi 1 ya EPL Mwaka huu 2017 na kutupwa nje ya 4 Bora kwa mara ya kwanza tangu Septemba 24.

Kabla ya Mechi na Hull, Liverpool, wakiwa kwao Anfield, walitoka Sare na Vinara Chelsea na hilo lilitegemewa kuwafanya wageuke na kuanza kupata ushindi lakini hadithi ikawa nyingine.

Kipigo toka kwa Hull kimeendeleza mwenendo wao wa kufungwa na Timu ‘dhaifu’ kama vile walivyofanywa Msimu huu na Timu zilizo Nafasi za 9 za mwisho ambazo ni Burnley, Bournemouth, Swansea City na hiyo Hull.

Lallana amekiri kuwa kukosa uzoefu kunawaathiri.

Ametamka: “Unaona uzoefu wa Chelsea, wanajua kushinda hata kama hawachezi vyema. Kwetu James Milner pekee ana uzoefu wa kutwaa Ubingwa alipokuwa Man City. Inabidi tujifunze toka kwake.”

Hata hivyo, Lallana amejipa moyo: “Sidhani Chelsea washatokomea na Ubingwa lakini Liverpool inabidi iwe bora zaidi. Mbio za Ubingwa zinaanza Machi!”