UHAKIKA WENGER KUNG’OKA MWISHONI MWA MSIMU WAJENGEKA!

WENGER-BAIBAIKwa mujibu wa mmoja wa Wachezaji Magwiji wa Arsenal walioipa Klabu hiyo Taji lao la mwisho la Ubingwa wa England Msimu wa 2003/04, Meneja wa Timu hiyo Arsene Wenger hakika atang’oka wakishindwa kutwaa Taji Msimu huu.

Ray Parlour, Kiungo mahiri wa Arsenal enzi za ‘Timu isiyofungika’, ameongea mara baada ya Jana Usiku Arsenal kuchapwa 2-1 Nyumbani kwao Emirates na Watford na kuachwa wakiwa Pointi 9 nyuma ya Vinara Chelsea kwenye EPL, Ligi Kuu England.

Mbali ya Parlour, pia Washabiki wengi wa Klabu hiyo wanajumuika zaidi na kuongezeka zaidi Siku hadi Siku kwenye kampeni ya kumtaka Mfaransa Wenger aliedumu Arsenal kwa Miaka 20 aondoke.

Akihojiwa, Ray Parlour amenena: “Atajua kama hakufanya kazi nzuri Msimu huu na nadhani ataondoka!”  

Parlour pia ametabiri kuwa ikifika wakati wa Wenger kung’oka basi hatakuwa na uhusiano tena na Klabu hiyo tofauti na Klabu kama Manchester United wakati Meneja wao wa Miaka 26, Sir Alex Ferguson, alipostaafu akapewa Ukurugenzi kwenye Klabu hiyo.

Parlour ameeleza: “Sidhani kama atabaki Klabuni. Yeye si Mtu wa aina hiyo!’