CITY YAKIRI KOSA LA KUKIUKA SHERIA ZA MADAWA HARAMU, NAE PAPY DJILOBODJI ‘JELA’ MECHI 4!

ETIHAD-SITWAKATI Klabu ya Manchester City wakikiri kukiuka Sheria za Kuzuia Matumizi ya Madawa Haramu, Mchezaji wa Sunderland Papy Djilobodji amefungiwa Mechi 4 kwa kosa la kucheza kwa fujo.

CITY NA MADAWA

Manchester City walifunguliwa Mashitaka na FA, Chama cha Soka England, hapo Januari 12 kwa Kosa la kukiuka Sheria za Kuzuia Matumizi ya Madawa Haramu na hii Leo wameamua kukubali kosa lao.

Waliposhitakiwa, ilidaiwa City walishindwa kuwapa Taarifa sahihi Maafisa wanaopima Wachezaji Matumizi ya Madawa Haramu.

Kila Klabu hupaswa kujulisha Wachezaji wao watakuwa wapi kwa ajili ya kupimwa lakini City walishindwa kutoa Taarifa za Ratiba ya Mazoezi na wapi Wachezaji hao watapatikana baada ya Mazoezi ili Maafisa wanaohusika wajue wakati wote wapi watawapata wakitakiwa kupimwa.

Imedaiwa City ilishindwa mara 3 kupeleka Taarifa za waliko Wachezaji wao na ndio maana FA ikawashitaki.

Kawaida kosa kama hilo huadhibiwa kwa Faini.

PAPY DJILOBODJI ‘JELA’ MECHI 4!

Beki wa Sunderland Papy Djilobodji amefungiwa Mechi 4 baada ya kukutwa na hatia ya kucheza kwa fujo.

Beki huyo mwenye Miaka 28 alipinga Kosa lake ilipodaiwa alimpiga Usoni kwa Mkono Mchezaji wa West Bromwich Albion Darren Fletcher wakati Timu yake ikichapwa 2-0 Jumamosi iliyopita kwenye Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.

Tukio hilo halikuonwa na Waamuzi wa Mechi hiyo na kupitiwa na Jopo Huru ambalo sasa limeridhika ni Kosa lililostahili Kadi Nyekundu.

Papy Djilobodji, Mchezaji kutoka Senegal, atafungiwa Mechi 4 badala ya 3 kwa vile Novemba 19 pia alitolewa nje kwa Kadi Nyekundu kwenye Mechi ya Sunderland na Hull City.

Mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea sasa atazikosa Mechi za Sunderland dhidi ya Tottenham hapo Januari 31 ikichezwa Nyumbani, na nyingine ni na Crystal Palace, Ugenini, Southampton, Nyumbani, na Everton, Ugenini.

Kukosekana huku kwa Papy Djilobodji ni pigo kwa Sunderland ambao wako mkiani mwa EPL.