SUPERCOPPA ITALIANA 2016: KUPIGWA DOHA, QATAR IJUMAA JUVENTUS v AC MILAN

SUPERCOPPA-QA2Klabu za Italy, Juventus na AC Milan, zitapambana huko Doha, Qatar kugombea Supercoppa Italiana.

Kawaida Mashindano haya huchezwa kama Mechi ya Ufunguzi wa Msimu Mpya huko Italy lakini safari hii yamesogezwa hadi Desemba na kwa mara nyingine tena kuchezwa nje ya Italy.

Kombe hili lishawahi kuchezwa huko USA katika Miaka ya 1993 na 2003, Tripoli, Libya Mwaka 2002 na Fainali zake 3 kati ya 5 zilizopita kuchezwa huko China.

Supercoppa, ambayo hushindaniwa na Bingwa wa Serie A na Mshindi wa Coppa Italia.

Kwa vile Juve ndio walizoa Ubingwa wote, AC Milan, ambao walifungwa na Juve kwenye Fainali ya Coppa Italia, ndio watacheza na Juve kugombea Supercoppa Italiana.

Bingwa Mtetezi wa Supercoppa Italiana ni Juve ambae Mwaka Jana waliwafunga Napoli 2-0 huko Shanghai Stadium, Shanghai, China.

Safari hii Supercoppa itachezwa Jassim Bin Hamad Stadium, Doha, Qatar.

Kawaida Mechi kati ya Juve na AC Milan ni ngumu kutabirika na Mechi 4 zilizopita Mshindi kupatikana kwa tofauti ya Bao 1 tu.

Kwenye Fainali ya Coppa Italia Mwezi Mei, Juve waliwatungua AC Milan 1-0 kwa Bao la Alvaro Morata lakini Mwezi Oktoba AC Milan waliifunga Juve 1-0 kwenye Mechi ya Serie A.

Kwenye Serie A hivi sasa, Juve ndio Vinara wakiwa Pointi 7 mbele ya Timu ya Pili AS Roma wakati AC Milan wako Nafasi ya 5 wakiwa Pointi 9 nyuma ya Juve.