FAINALI KOMBE LA DUNIA - RUSSIA 2018: DROO KUFANYIKA DESEMBA 1 HUKO KREMLIN!

WC-RUSSIA2018-LOGOFIFA imethibitisha kuwa Droo za kupanga Makundi na Mechi za Fainali za Kombe la Dunia la Mwaka 2018 huko Russia itafanyika Ijumaa Desemba 1 huko Kremlin Jijini Moscow.
Wakati Tarehe ya Droo ilikuwa ishajulikana, mahali pa kuifanyia palikuwa bado hapajatangazwa.
Kwa kuichagua Kremlin, Russia imeonyesha jinsi inavyoipa kipaumbele Fainali hizo.
Kremlin ni Ngome kubwa ya Urusi ambayo inatambuliwa na UNESCO kama moja ya Sehemu za Urithi wa Dunia (UNESCO World Heritage Site).
Kremlin ni eneo ambalo lina Makanisa ya Kiasili na Majumba ya Kifalme na mojawapo ni yale Makazi Rasmi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Huko Kremlin Droo yenyewe itafanyika kwenye Jengo la Kifalme liliokuwa likitumika kwa ajili ya Mikutano ya Chama cha Kikomunisti cha Soviet Union na baadae kugeuzwa kuwa Ukumbi wa Burudani.
Ukumbi huo una uwezo wa kuchukua Watazamaji 6,000.
Russia walishinda Kura za kuwa Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 zilizofanyika Desemba 2010 kwa kuwabwaga Wagombea wengine ambao ni Belgium/Netherlands (Waliotaka kuwa Wenyeji wenza), England na Portugal/Spain (Waliotaka kuwa Wenyeji wenza).
Kuanzia Juni 17 na Julai 2 Mwaka huu, Russia watakuwa Wenyeji wa Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara, FIFA CONFEDERATION CUP, ambalo washindani wake ni Russia, kama Mwenyeji, Mabingwa wa Dunia Germany na Mabingwa wa Mabara 6 Duniani amvao ni Australia, Chile, Mexico, New Zealand, Portugal na Bingwa wa AFCON 2017, Kombe la Mataifa ya Afrika ambazo Fainali zake zinaendelea hivi sasa huko Gabon.
Ni desturi kwa Mashindano hayo kufanyika kwa Nchi Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia Mwaka mmoja kabla Fainali zenyewe ili kupima uwezo wao kuandaa Mashindano makubwa.