FIFA KOMBE LA MABARA: VAR YACHENGUA, YAKERA WADAU!

==INAFAA AU MAUZAUZA TU?
FIFACONFED OFSIDEVAR, Mfumo wa Teknolojia ya Video uliobuniwa kuwasaidia Marefa kutoa maamuzi sahihi, unaipa FIFA wakati mgumu kutokana na matumizi yake kwa Majaribio huko Russia katika Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara yaliyoanza Jumamosi.
Lengo la FIFA ni kuwa VAR, Video Assistant Referee, itumike kikamilifu kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 ambazo pia zitachezwa Nchini Russia.
Lakini Jana Jumapili, katika Mechi 2 za Kombe la Mabara, matumizi ya VAR yalileta mkanganyiko na hasa pale yalipoonekana kuchukua muda mrefu tangu Refa alipoomba msaada wa VAR, kutoka kwa Marefa Wasaidizi waliokuwepo pembezoni mwa Uwanja wakirudia Mikanda ya Video ya tukio husika, hadi Refa huyo kutoa uamuzi baada ya kupata msaada wa VAR.
++++++++++++++
JE WAJUA?
-VARs=Video Assistant Referee:
-Kwenye Mfumo huo wa Video, Refa Msaidizi atakuwepo pembeni mwa Uwanja na atakuwa na Mawasiliano na Refa wa Mechi wakati wote wa Mechi hiyo akipitia Video bila kusitisha Mechi.
-Ikiwa litatokea tukio ambalo Refa Msaidizi ameliona atamtonya Refa wa Mechi ambae ana ruksa ya kuukubali ushauri huo au akaamua mwenyewe kwenda pembeni kulipitia na kutoa uamuzi wake.
-Ama Refa anaweza kumuomba Refa Msaidizi wa VARs kulipitia tukio ili ampe ushauri.
++++++++++++++
Jana Portugal na Chile wote walinyimwa Magoli kwa Ofsaidi zilizoamuliwa kwa msaada wa VAR.VIDAL
Portugal pia walilazimika kusubiri kwa muda baada ya kufunga Bao safi wakisubiri VAR impe uhakika Refa wa uhalali Bao lao.
Maelekezo ya FIFA kwa Marefa ni kuwa waombe msaada wa VAR pale tu kuna matukio tata yanayoweza kuibadili Gemu kamili vile utoaji Penati na maamuzi ya Ofsaidi wakati Goli limefungwa wakati wakiwa hawana uhakika kama waliashiria sawa.
Jana Mechi ya Portugal na Mexico ilikwisha 2-2 na Chile kuitwanga Cameroon 2-0.
Akiongea baada ya Mechi kuhusu VAR, Kocha wa Chile, Juan Antonio Pizzi, alisema: "Hata kama ni sahihi, hili hutibua akili za Wachezaji wakati wa Mechi!"
Kwenye Mechi ya Jana, Staa wa Chile Arturo Vidal alionekana akibishana vikali na Refa Damir Skomina baada ya Bao lao lililofungwa Dakika za Majeruhi za Kipindi cha Kwanza na Eduardo Vargas kukataliwa rasmi Dakika 1 baada ya kufungwa.
Maelekezo ya FIFA ni kuwa tangu Refa aombe msaada wa VAR hadi yeye atakapoamua baada kupokea msaada huo yasizidi Sekunde 6.
Bao la Pili la Chile lililofungwa Dakika za Majeruhi baada Dakika 90 kwisha nalo lilipelekwa VAR na kuchukua Sekunde 30 kuthibitishwa baada ya mwanzoni kutolewa uamuzi tata kuwa Alexia Sanchez alikuwa Ofsaidi kwenye muvu ya kufunga Bao hilo.
Dhidi ya Mexico, Nani wa Portugal alifunga Bao ambalo nalo halikuthibitishwa na Refa licha kutoonyeshwa Kibendera cha Ofsaidi na baada ya muda kufutwa kabisa baada VAR kutoa ushauri.
Utata zaidi ulionekana pale Refa kutoka Argentina, Nestor Pitana, akiomba msaada wa VAR bila sababu ya msingi baada ya Cedric Soares kuifungia Portugal Bao katika Dakika ya 86 na kuongoza 2-1 lakini baada ya ushauri huo uliokula muda Bao hilo likabaki kama lilivyo.
Kocha wa Portugal Fernando Santos ameeleza: "Lazima tuwe waangalifu..Sidhani Watu wanaifahamu hii Sheria Mpya!"
Katika Siku ya Pili tu ya Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara kumezuka utata wa Matukio Manne yaliyohusisha VAR wakati Mwaka Jana Mkuu wa Marefa wa FIFA, Massimo Busacca, alijigamba kuwa VAR itapindua uamuzi mbovu Mmoja tu katika kila Mechi 4 au 5.
Kocha wa Cameroon Hugo Broos ameeleza: "Kama hayo yatatokea mara kadhaa katika Mechi basi si jambo zuri kwa Wachezaji!"
Kwa mpango wa Rais wa FIFA Gianni Infantino anataka Majaribio haya ya VAR yafanikiwe ili Mwezi Machi Mwakani yapitishwe na IFAB ili wao wabariki VAR itumike rasmi kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Russia Mwezi Juni 2018.

Habari MotoMotoZ