JUVE, CHELSEA DILI YA STAA MBRAZIL!

CHELSEA imeripotiwa kufikia makubaliano na Juventus ili wamnunue Fulbeki Staa kutoka Brazil.

Alex Sandro, nwenye Miaka 26, amekuwa akihusishwa sana kuhamia Stamford Bridge hasa baada ya Meneja wao Antonio Conte kutaka Mtu wa kumpa changamoto Fulbeki wao wa Kushoto Marcos Alonso.

SANDROWiki iliyopita Mkuu wa Juve Giuseppe Marotta alitoboa wameikataa Ofa nzuri ya Chelsea wakitaka kumnunua Staa huyo alieichezea Timu ya Taifa ya Brazil mara 12.

Lakini sasa duru za Kisoka zimebaini Chelsea watamwaga Pauni Milioni 60 kumchota Sandro.

Tayari Mchezaji huyo ashakubaliana na Chelsea Maslahi yake binafsi na Mshahara wake wa Pauni 75,000 kwa Wiki huko Juve kuongezeka maradufu huko Jijini London.

Ripoti hizi za Sandro zimepata uzito Mkuu baada ya Giuseppe Marotta Jana kukiri Juve imepata Ofa kubwa mno kuhusu Sandro ambae walimsaini kutoka FC Porto ya Ureno kwa Pauni Milioni 23 Miaka Miwili iliyopita.

Marotta ameeleza: "Ofa kubwa imekuja Wiki hii. Hatuna nia kuuza Mchezaji lakini Mchezaji akiamua kuondoka, kama ilivyotokea Miaka ya nyuma, mwisho wa Siku lazima aondoke tu. Hatulazimishi Mtu kubaki!"

Mbali ya Sandro, Chelsea pia ipo mbioni kuwezesha Dili ya kumsaini Kiungo wa AS Monaco Tiemoue Bakayoko, mwenye Miaka 22, kwa Dau la Pauni Milioni 35.

Kutua kwa Mchezaji huyo wa Kimataifa wa France huko Stamford Bridge kutafungua njia kwa Kiungo Nemanja Matic kujiunga na Manchester United kama anavyowania Meneja wa Man United Jose Mourinho.

Mourinho, alipokuwa Chelsea, ndie aliemrudisha tena Matic Klabuni hapo kutoka Benfica ya Ureno.

ARSENAL YAANUA JEZI MPYA, NAMBA 7 YA SANCHEZ ANAYO WELBECK, MASHABIKI WAHOFU ‘KAUZWA’!

ARSENAL JEZI MPYALEO Arsenal wametangaza Jezi zao mpya kwa ajili ya Msimu Mpya wa 2017/18 na Danny Welbeck akaonekana ndie mwenye Namba 7 aliyokuwa akivaa Alexis Sanchez Msimu uliopita.

Matangazo yalikuwa ya kuwapa nafasi Mashabiki wa Arsenal kuona Jezi hizo Mpya na kuweka Oda ya Kununua Jezi hizo ambazo zitaanza kuwa Sokoni Julai 3.

Mashabiki walipoingia kwenye Tovuti hiyo kuchagua Jezi na wale waliochagua Jina la Danny Welbeck walishtushwa walipoona Mgongoni ipo Namba 7 iliyokuwa ya Alexis Sanchez.

Hivi sasa upo uvumi mkubwa kuwa Sanchez anataka kuhama na hili linazidi kushika kasi kwa vile hataki kusaini Mkataba Mpya wakati huu wa sasa ukiwa unaisha Mwakani.

Zipo taarifa Man City, Bayern Munich na Klabu kadhaa huko Italy zinamnyemelea huku Arsenal wakiwa wamejiwekea thamani yake kuwa ni zaidi ya Pauni milioni 50.

Mara baada ya Mashabiki kuhoji kulikoni kuhusu Jezi Mpya na Namba 7 kupewa Welbeck, haraka haraka Tovuti ya Arsenal ikamrejesha Welbeck kwenye Namba yake ya kawaida 23.

MOURINHO NAE ABURUZWA KWA PILATO KWA MADAI YA UKWEPAJI KODI!

MANUNITED MOU BLACKMENEJA wa Manchester United Jose Mourinho nae ameungana na mlolongo wa Mastaa Wachezaji Soka walioburuzwa Mahakamani huko Nchini Spain kwa tuhuma za Ukwepaji Kulipa Kodi.

Imedaiwa Mourinho amekwepa kulipa Kodi ya kiasi cha Pauni Milioni 2.9, Euro Milioni 3.3, aliyopaswa kulipa kati ya Miaka 2011 na 2012.

Mwendesha Mashitaka kwenye Mahakama ya Spain amedai Mourinho hakubainisha Mapato yake yatokanayo na Mauzo ya Umiliki wake wa Picha na Matangazo mengine.

Mashitaka ya Mourinho, mwenye miaka 54, ni Mawili ya kukwepa Kodi ya Euro Milioni 1.6 Mwaka 2011 na Euro Milioni 1.7 Mwaka 2012.

Mourinho mwenyewe hajatamka lolote kuhusu tuhuma hizi.

Mastaa wengine wa Soka walioandamwa na Kesi za aina hii ni pamoja na Cristiano Ronaldo anmbae Wiki iliyopita alifunguliwa rasmi Mashitaka kiasi cha kumuudhi na sasa ametishia kuihama Spain na kuacha kuichezea Real Madrid.

Wengine waliowahi kushitakiwa na kuhukumiwa ni Fowadi wa Barcelona, Lionel Messi, ambae alipigwa Faini na kuamriwa ende Jela Miezi 21 ingawa Kifungo hiki kinaaminika kitakuwa cha nje, na Javier Mascherano wa Barcelona aliefungwa Kifungo cha nje cha Mwaka Mmoja.

 

 

 

FIFA KOMBE LA MABARA: VAR YACHENGUA, YAKERA WADAU!

==INAFAA AU MAUZAUZA TU?
FIFACONFED OFSIDEVAR, Mfumo wa Teknolojia ya Video uliobuniwa kuwasaidia Marefa kutoa maamuzi sahihi, unaipa FIFA wakati mgumu kutokana na matumizi yake kwa Majaribio huko Russia katika Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara yaliyoanza Jumamosi.
Lengo la FIFA ni kuwa VAR, Video Assistant Referee, itumike kikamilifu kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 ambazo pia zitachezwa Nchini Russia.
Lakini Jana Jumapili, katika Mechi 2 za Kombe la Mabara, matumizi ya VAR yalileta mkanganyiko na hasa pale yalipoonekana kuchukua muda mrefu tangu Refa alipoomba msaada wa VAR, kutoka kwa Marefa Wasaidizi waliokuwepo pembezoni mwa Uwanja wakirudia Mikanda ya Video ya tukio husika, hadi Refa huyo kutoa uamuzi baada ya kupata msaada wa VAR.
++++++++++++++
JE WAJUA?
-VARs=Video Assistant Referee:
-Kwenye Mfumo huo wa Video, Refa Msaidizi atakuwepo pembeni mwa Uwanja na atakuwa na Mawasiliano na Refa wa Mechi wakati wote wa Mechi hiyo akipitia Video bila kusitisha Mechi.
-Ikiwa litatokea tukio ambalo Refa Msaidizi ameliona atamtonya Refa wa Mechi ambae ana ruksa ya kuukubali ushauri huo au akaamua mwenyewe kwenda pembeni kulipitia na kutoa uamuzi wake.
-Ama Refa anaweza kumuomba Refa Msaidizi wa VARs kulipitia tukio ili ampe ushauri.
++++++++++++++
Jana Portugal na Chile wote walinyimwa Magoli kwa Ofsaidi zilizoamuliwa kwa msaada wa VAR.VIDAL
Portugal pia walilazimika kusubiri kwa muda baada ya kufunga Bao safi wakisubiri VAR impe uhakika Refa wa uhalali Bao lao.
Maelekezo ya FIFA kwa Marefa ni kuwa waombe msaada wa VAR pale tu kuna matukio tata yanayoweza kuibadili Gemu kamili vile utoaji Penati na maamuzi ya Ofsaidi wakati Goli limefungwa wakati wakiwa hawana uhakika kama waliashiria sawa.
Jana Mechi ya Portugal na Mexico ilikwisha 2-2 na Chile kuitwanga Cameroon 2-0.
Akiongea baada ya Mechi kuhusu VAR, Kocha wa Chile, Juan Antonio Pizzi, alisema: "Hata kama ni sahihi, hili hutibua akili za Wachezaji wakati wa Mechi!"
Kwenye Mechi ya Jana, Staa wa Chile Arturo Vidal alionekana akibishana vikali na Refa Damir Skomina baada ya Bao lao lililofungwa Dakika za Majeruhi za Kipindi cha Kwanza na Eduardo Vargas kukataliwa rasmi Dakika 1 baada ya kufungwa.
Maelekezo ya FIFA ni kuwa tangu Refa aombe msaada wa VAR hadi yeye atakapoamua baada kupokea msaada huo yasizidi Sekunde 6.
Bao la Pili la Chile lililofungwa Dakika za Majeruhi baada Dakika 90 kwisha nalo lilipelekwa VAR na kuchukua Sekunde 30 kuthibitishwa baada ya mwanzoni kutolewa uamuzi tata kuwa Alexia Sanchez alikuwa Ofsaidi kwenye muvu ya kufunga Bao hilo.
Dhidi ya Mexico, Nani wa Portugal alifunga Bao ambalo nalo halikuthibitishwa na Refa licha kutoonyeshwa Kibendera cha Ofsaidi na baada ya muda kufutwa kabisa baada VAR kutoa ushauri.
Utata zaidi ulionekana pale Refa kutoka Argentina, Nestor Pitana, akiomba msaada wa VAR bila sababu ya msingi baada ya Cedric Soares kuifungia Portugal Bao katika Dakika ya 86 na kuongoza 2-1 lakini baada ya ushauri huo uliokula muda Bao hilo likabaki kama lilivyo.
Kocha wa Portugal Fernando Santos ameeleza: "Lazima tuwe waangalifu..Sidhani Watu wanaifahamu hii Sheria Mpya!"
Katika Siku ya Pili tu ya Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara kumezuka utata wa Matukio Manne yaliyohusisha VAR wakati Mwaka Jana Mkuu wa Marefa wa FIFA, Massimo Busacca, alijigamba kuwa VAR itapindua uamuzi mbovu Mmoja tu katika kila Mechi 4 au 5.
Kocha wa Cameroon Hugo Broos ameeleza: "Kama hayo yatatokea mara kadhaa katika Mechi basi si jambo zuri kwa Wachezaji!"
Kwa mpango wa Rais wa FIFA Gianni Infantino anataka Majaribio haya ya VAR yafanikiwe ili Mwezi Machi Mwakani yapitishwe na IFAB ili wao wabariki VAR itumike rasmi kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Russia Mwezi Juni 2018.

RONALDO ASISITIZA KUONDOKA REAL, ATAENDA WAPI?

>MAN UNITED AU PSG?

WAKATI Dunia ikishangazwa kwa kuibuka habari kuwa Mchezaji Bora Duniani Cristiano Ronaldo sasa ameamua kuondoka Real Madrid ili aihame Spain iliyomburuza Mahakamani kwa tuhuma za Ukwepaji Kulipa Kodi, imedaiwa yeye mwenyewe ameng’ang’ania msimamo huo kwa kuwaambia Wachezaji wenzake wa Timu ya Taifa ya Ureno.

Akiongea na wenzake hao ambao wako wote huko Russia kwa ajili ya Michuano ya FIFA Kombe la Mabara inayoanza Leo, inasemekana Ronaldo alisema: “Naondoka Real Madrid. Nishafanya uamuzi. Hakuna kurudi nyuma!”

RONALDO-MAUNITEDJe, Ronaldo akiondoka Real atakwenda wapi?

Gazeti la A Bola la huko Nchini kwa Ronaldo, Portugal, limedai tayari ipo Ofa ya Euro Milioni 180 ya kumnunua Supasta huyo huku Manchester United na Paris Saint-Germain zikitajwa.

Lakini Wadadisi wanadai, kwa uhalisia, Uhamisho wowote wa Ronaldo utagharimu kiasi kinachoweza kufikia Euro Milioni 400 ukijumuisha Ada ya Uhamisho na Mshahara wake kwa Kipindi cha Mkataba.

Je Man United wataafiki Ronaldo arejee?

Ukweli ni kuwa Manchester United na Mashabiki wao wote watapenda sana Ronaldo arejee Old Trafford.

Akiwa na Man United, Ronaldo alicheza Mechi 292 na kufunga Bao 118.

++++++++++++++

JE WAJUA?

-Ronaldo ni mmoja wa Wachezaji Wanne wa Man United waliotwaa Ballon d'Or katika Historia ya Klabu hiyo.

-Wengine ni George Best, Dennis Law na Bobby Charlton ambao nje ya Uwanja wa Old Trafford imesimikwa Sanamu ya Watatu hao.

++++++++++++++

Ni Wayne Rooney aliecheza na kufunga Bao mara 2 zaidi ya Ronaldo lakini moyoni mwa Mashabiki wa Man United Ronaldo ndie alieshika hatamu.

Mashabiki wa Klabu hiyo kubwa Duniani bado wanamwimba Ronaldo Majukwaani Viwanjani wakati wa Mechi na hii Leo, kwenye Majukwaa ya Mitandao ya Kijamii, Mashabiki wanambembeleza Mtendaji kuu Ed Woodward amrejeshe Cristiano Ronaldo.

Ukweli ni kuwa, nyuma ya pazia, Ed Woodward na Maafisa wa Man United watakuwa wakifuatilia kwa karibu sana sakata hili la sasa la Ronaldo.

Habari MotoMotoZ