SUPERCLASICO: ARGENTINA YAITUNGUA BRAZIL KWA MARA YA KWANZA BAADA MIAKA 5!

MECHI YA KIRAFIKI kati ya Miamba ya Marekani ya Kusini, Brazil na Argentina, iliyochezwa huko Melbourne Cricket Ground Mjini Melbourne, Australia na kuhudhuriwa na Washabiki 95,569 iliisha kwa Argentina kushinda 1-0.

Hiki kimekuwa kipigo cha kwanza kwa Kocha wa Brazil, Tite, alieiongoza Brazil katika ushindi wa Mechi 9 wakifunga Bao 25 na kufungwa 2 tu.

BRA-ARGKwa Jorge Sampaoli, hii ilikuwa Gemu yake ya kwanza tu tangu ateuliwa Kocha wa Argentina na kuamua kuutumia mtindo mpya wa 3-4-3 ambao waliubadili kidogo na kuwa 3-4-2-1.

Kwa Argentina huu ni ushindi mtamu unaowapa morali ya kufanya vyema kwenye Mechi zao 4 zilizobakia za Kanda ya Nchi za Marekani ya Kusini za kufuzu Kombe la Dunia 2018 ambako wao wako Nafasi ya 5 wakati ni 4 tu za juu ndizo hufuzu moja kwa moja.

Brazil wao ndio wanaongoza Kanda hiyo na tayari wameshatinga Fainali hizo za Kombe la Dunia huku wakiwa na Mechi 4 mkononi.

Wakati Argentina walishusha Kikosi ‘fulu nondo’, Brazil haikuwachukua Wachezaji wao wa kawaida ambao wamepumzishwa ambao ni Staa wao mkubwa Neymar, Fowadi wa Liverpool Roberto Firmino, na Mabeki Dani Alves, Marcelo na Marquinhos.

Katika Dakika ya 31, Beki wa Argentina Jonathan Ramón Maidana alipewa Kadi ya Njano kwa kumtimba kwa makusudi Gabriel Jesus.

Dakika ya 44, Kona ya Angel Di Maria ilichezwa kwa Kichwa na Nicolas Otamendi na kupiga Posti na kumkuta Gabriel Mercado, alieonekana kuwa Ofsaidi, na kufunga kilaini.

Hadi Mapumziko Argentina 1 Brazil 0.

+++++++++++++++++

ARGENTINA v BRAZIL

-Matokeo ya hivi karibuni:

Brazil 3-0 Argentina - 10 November 2016

Argentina 1-1 Brazil - 14 November 2015

Argentina 0-2 Brazil - 11 October 2014

Argentina 2-1 Brazil - 21 November 2012

Brazil 2-1 Argentina - 20 September 2012

+++++++++++++++++

Kipindi cha Pili kilianza kwa Brazil kuja juu na kutawala na kukosa Bao kadhaa hasa Dakika ya 62 wakati Gabriel Jesus akiwa nafasi nzuri ya kufunga alipiga Posti na Mpira kumrudi Willian ambae alifumua Shuti na kugonga Posti na kuokolewa.

Baada ya hapo Brazil walifurukuta lakini wakaikuta ngome ya Argentina ikiwa na Kipa wa Man United Sergio Romero ngumu kupenyeka na ambao pia hawakufanya mashambulizi yeyote ya maana huku Staa wao Lionel Messi kuonekana kupooza Mechi nzima.

Dakika za mwishoni, Otamendi alimpiga kipepsi Mchezaji mwenzake wa Man City Gabriel Jesus wakigombea Mpira wa juu na Jesus kulazimika kutolewa kwa Machela na nafasi yake kuchukuliwa na Taison.

VIKOSI:

Argentina (Mfumo 3-4-2-1):

Sergio Romero;

Gabriel Mercado [Emmanuel Mammana, 74], Jonathan Maidana, Nicolas Otamendi;

Jose Luis Gomez [Nicolás Tagliafico, 51], Lucas Biglia, Ever Banega [Manuel Lanzini, 80], Angel Di Maria;

Lionel Messi, Paulo Dybala [Guido Rodriguez, 68];

Gonzalo Higuain [Carlos Joaquín Correa, 46]

Brazil (Mfumo 4-3-3):

Weverton;

Fagner [Rafinha, 72], Gil, Thiago Silva, Filipe Luis;

Paulinho [Giuliano, 80], Fernandinho, Renato Augusto [Douglas Costa, 65];

Willian, Gabriel Jesus [Taison, 90], Philippe Coutinho.

REFA: Chris Beath [Australia]

Habari MotoMotoZ