KEPTENI WA ‘WATAKATIFU’ AIPA KLABU OMBI LA KUHAMA!

>MAN UNITED, EVERTON ZATAJWA ‘KUMTAKA’!

SOUTHAMPTON-FONTENAHODHA wa Southampton, José Fonte, amepeleka maombi yake aruhusiwe kuihama Klabu hiyo maarufu kama ‘Watakatifu’.

Habari za ombi hilo zimethibitishwa na Mkurugenzi wa Soka wa Watakatifu, Les Reed.

Fonte, ambae aliisaidia Portugal kutwaa EURO 2016, amekuwa akihuzunishwa na hali yake huko Southampton na hasa baada ya Meneja Claude Puel kutompa namba kucheza Mechi zao 6 za UEFA EUROPA LIGI.

Mreno huyo ana Mkataba na Southampton hadi 2018 lakini Reed amesema Fonte amegoma kusaini Mkataba mpya wenye maslahi bora kwake na badala yake kuomba kuruhusiwa kuhama.

Fonte, ambae alijiunga na Southampton Januari 2010 kutoka Crystal Palace, ameichezea Klabu yake Mechi 288 zikiwemo 19 Msimu huu za EPL, Ligi Kuu England, na EFL CUP.

Reed amethibitisha kuwa Klabu yao haijapokea Ofa yeyote ya kumnunua Fonte licha ya Mchezaji huyo kuhusishwa na Manchester United pamoja na Everton ambayo Meneja wao Ronald Koeman ndie alimpa Fonte, akiwakilishwa na Supa Wakala Jorge Mendes, Mkataba mpya Mwaka 2015 Koeman alipokuwa Southampton.