UHAMISHO LINDELOF KWENDA MAN UNITED: BENFICA WAWANIA KUZIPIGA DILI MAN UNITED NA VASTERAS!

VICTOR-LINDELOFMBALI ya kuwepo taarifa za Manchester United kukamilisha makubaliano ya kumsaini Beki wa Sweden Victor Lindelof kutoka Benfica, upo uvumi mzito kuwa Klabu hiyo ya Ureno inataka Mchezaji huyo asaini Mkataba mpya ili kupandisha Dau lake.

Kwenye Mkataba wa sasa wa Mchezaji huyo mwenye Miaka 22 kipo Kipengele cha Benfica kulipwa Pauni Milioni 30 ikiwa atahama ndani ya Mkataba huo.

Jarida la huko Ureno, O Jogo, limeripoti kuwa Benfica wanataka asaini Mkataba Mpya ili Dau la Kuhama liwe Pauni Milioni 50 na pia kuidhibiti Klabu ya kwanza ya Lindelof, Vasteras ya Sweden, ambayo inaidai Benfica Malipo ya kumtumia Mchezaji huyo kwenye Ligi na UEFA CHAMPIONZ LIGI baada ya kufikisha Mechi kadhaa kama Mkataba wa Uhamisho kutoka Vasteras kwenda Benfica unavyotamka ambapo pia Benfica wanapaswa kulipa Asilimia 10 ya Mauzo ya Mchezaji huyo kwa Klabu nyingine.

Inaaminika baada ya Benfica kupanchi kukidhi matakwa ya Mkataba huo mvutano kati ya Vasteras na Benfica sasa umetua FIFA.

Mbali ya utata huu, imedaiwa Meneja wa Man United, Jose Mourinho, ana nia thabiti ya kumsaini Lindelof ambae mwenyewe amefurahia Dili hii ambayo itamtoa kwenye Mshahara wa Pauni 3, 000 kwa Wiki anaopata Benfica hadi Pauni zaidi ya 58, 000 kwa Wiki huko Old Trafford.