RIPOTI SPESHO

7 WAIGOMEA CAMEROON KUCHEZA AFCON 2017 JANUARI HUKO GABON!

CAMEROON-MATIPWACHEZAJI 7 wa Cameroon wamesema hawana nia ya kuichezea Timu ya Taifa ya VCameroon kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Africa, AFCON 2017, zitakazoanza Januari 14 huko Gabon.

Wachezaji hao 7, ambao waliteuliwa kwenye Kikosi cha Awali cha Wachezaji 35 na Kocha Hugo Broos mapema Mwezi huu, sasa wapo hatarini kufungiwa kuzichezea Klabu zao wakati AFCON 2017 ikiendelea.

Saba hao wote ni Maprofeshenali huko Ulaya nao ni Joel Matip (Liverpool), Andre Onana (Ajax Amsterdam), Guy Roland Ndy Assembe (Nancy), Allan Nyom (West Bromwich Albion), Maxime Poundje (Girondins Bordeaux), Andre-Frank Zambo Anguissa (Olympique Marseille) na Ibrahim Amadou (Lille).

Akiongea hapo Jana, Kocha wa Cameroon Broos amelalamika kuwa Wachezaji hao wameweka maslahi yao binafsi mbele kuliko ya Taifa na Shirikisho la Soka la Cameroon, FECAFOOT, lina haki ya kuwaadhibu kwa mujibu wa Kanuni za FIFA.

Matip, ambae ni Mzaliwa wa Germany, amedai yeye hataki kuichezea Cameroon kutokana na uhusiano mbovu na Makocha waliopita na amesusa kuichezea Cameroon tangu Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 kwisha huko Brazil.

Mara mbili Kocha Broos alijaribu kumshawishi Matip lakini Mchezaji huyo aligoma.

Nao Nyom, by Amadou, Ndy Assembe, Onana na Zambo Anguissa wamemwambia Kocha huyo kuwa hawataki kuondoka Klabuni kwao kwa kuhofia kupoteza namba zao.

Nae Poundje, ambae hajawahi kuitwa na Cameroon nah ii ni mara ya kwanza kwake, amesisitiza kuwa nia yake ni kuichezea France.

Cameroon inatarajiwa kutangaza Kikosi chao cha mwisho kwa ajili ya AFCON 2017 mapema Wiki ijayo.

MAHREZ MCHEZAJI BORA AFRIKA 2016, TUZO YA BBC

MAHREZ-BBCMCHEZAJI wa Kimataifa wa Algeria Riyad Mahrez ametwaa Tuzo ya BBC ya Mchezaji Bora Afrika kwa Mwaka 2016.
Mahrez, Mzaliwa wa France mwenye Miaka 25, aliisaidia mno Leicester City kutwaa Ubingwa wa England Mwezi Mei kwa mara ya kwanza katika Historia yao na hilo limempa Tuzo hii maarufu na inayosifika ya BBC, Shirika la Utangazaji la Uingereza.
Mapema Mwaja huu, Mahrez alitunukiwa Tuzo ya PFA ya Mchezaji Bora wa Mwaka kwa England baada ya kuifungia Bao 17 na kutoa Msaada wa Bao 11 kwenye EPL, Ligi Kuu England, na kuwa Mchezaji wa Kwanza kutoka Afrika kuwahi kushinda Tuzo hiyo ya PFA, Professional Footballers Association, ambacho ni Chama cha Kutetea Maslahi ya Wanasoka wa Kulipwa.
Mahrez alishinda Tuzo hii ya BBC kwa kuzoa Kura nyingi za Mashabiki na kuwabwaga Wagombea wengine ambao ni Yaya Toure, Sadio Mane, Pierre-Emerick Aubameyang na Andre Ayew.
Mahrez, ambae alijiunga Leicester Mwaka 2014 akitokea Klabu ya France Le Havre kwa Dau la Pauni 400,000, sasa anaungana na kina Didier Drogba na  Staa wa Liberia George Weah ambao waliwahi kushinda Tuzo hii.

PLANI YA GIANNI INFANTINO FAINALI KOMBE LA DUNIA: MAKUNDI 16 YA TIMU 3, NCHI 48 KUCHEZA!

FIFA-GIANNI-INFANTINORAIS wa FIFA Gianni Infantino ana matumaini kuwa Fainali za Kombe la Dunia huko mbeleni zitakuwa na Makundi 16 ya Timu Tatu Tatu kwenye Mashindano yakatakayokuwa na Jumla ya Timu 48.

Awali Infantino, ambae alitwaa wadhifa wa Rais wa FIFA Mwezi Februari, alizungumzia kuwepo Timu 32 hadi 40.

Kwenye Plani hii ya sasa ya Makundi 16, Timu 2 za juu za kila Kundi ndizo zitasonga na kuunda Makundi mengine ya Timu 32 na kisha baada ya hapo Mashindano kuendelea kwa kufuuatia Raundi za Mtoano hadi Fainali.
Uamuzi huu wa kutumia Mfumo mpya utafanywa Mwezi Januari lakini kutumika kwake kutaanzia Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2026.

Ikiwa Mfumo huo wa Makundi 16 ya Timu Tatu Tatu hautapita yapo mapendekezo kadhaa ya Mifumo tofauti ambayo ni:

-Fainali za Timu 48 lakini awali Timu 32 zitacheza Mtoano wa Mechi 1 tu ili kupata Timu 16 ambazo zitaungana na Timu 16 nyingine ambazo zinapita moja kwa moja bila kucheza Mtoano ili kufanya Jumla ya Timu 32 kama ilivyo Fainali za Kombe la Dunia za sasa.

-Mfumo mwingine ni wa kuwa na Fainali ya Timu 40 ambazo zitakuwa na Makundi 10 ya Timu 4 kila moja au Makundi 8 ya Timu 5 kila moja.

Mara ya mwisho kwa idadi ya Timu zinazocheza Fainali ya Kombe la Dunia kuongezwa ilikuwa ni Fainali za 1998 zilipoongezwa kutoka Timu 24 hadi 32.

AZAM FC KUSAKA VIJANA U-17 MWANZA JUMAMOSI

AZAMFC-VIPAJIVIJANA wa Kanda ya Ziwa mpo tayariii? Hii ni habari njema kwenu kwani Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepanga kuendesha msako wa vipaji kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘U-17’ Jumamosi ijayo Novemba 26, mwaka huu ndani ya Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza.

Mpango huo wa kitaifa wa mabingwa hao uliopita kwenye mikoa mingine mitano nchini, utafanyika kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi 9.00 Alasiri ndani ya jiji hilo lenye historia ya kutoa wachezaji wengi wenye vipaji waliowahi kutamba na wengine wakitamba hivi sasa nchini.

Mara ya mwisho zoezi hilo lilifanyika jijini Mbeya na kuhudhuriwa na vijana 433, ambapo Azam FC ilivuna vijana 10 pekee watakaoingia kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika mwezi ujao kwenye makao makuu ya Azam Complex, Chamazi.

Mpaka sasa kwenye mikoa yote hiyo mitano, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro & Dodoma, Visiwani Zanzibar na Mbeya, Azam FC imechagua jumla ya vijana 60 kati ya vijana 2,999 waliofanyiwa usajili.

Kwa majaribio mengine ya wazi katika maeneo mengine kuzunguka Tanzania yatatangazwa hivi karibuni.

IMETOLEWA NA AZAM FC [By Abducado Emmanuel on November 24, 2016]

MKUU WA MKOA DAR MAKONDA AFANYA ZIARA AZAM FC, AIPONGEZA KWA UWEKEZAJI

MAKONDA-AZAMMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda, leo mchana amefanya ziara kwenye Makao Makuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC akiwa na lengo kuu la kuipongeza kutokana na juhudi kubwa wanazofanya za kuwekeza katika soka la Tanzania.

Mbali na kuipongeza Azam FC inayomilikiwa na familia ya mmoja ya wafanyabiashara maarufu Afrika, Alhaji Said Salim Bakhresa, pia ametoa shukrani zake kutokana na jitihada zinazoonyeshwa na mfanyabiashara huyo mzawa katika maeneo mengine aliyofanya uwekezaji mkubwa kwenye tasnia ya habari (Azam Media) na viwanda.

Kwenye msafara huo, Makonda aliambatana baadhi ya viongozi wengine wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, alikofanya ziara tofauti kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Jackson Lyanivana.

Ugeni huo ulipokelewa na viongozi wa juu wa Azam FC, wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa, Meneja wa timu, Phillip Alando, ambao katika kumalizia ziara hiyo waliweza kumtembeza kwenye maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa uwekezaji ndani ya Azam Complex.

Akitoa neno lake kwenye ziara hiyo, Makonda alisema haina ubishi kuwa Azam FC ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwekeza ipasavyo kwenye soka huku akidai kuwa timu hiyo imeshaanza kwa vitendo kutekeleza suala la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini.

“Leo hii mnatuunga mkono zaidi kwa sababu ni kiwanja kimoja na ni timu moja ambayo kila mtu aliyeko Dar es Salaam anaizungumzia, katika suala zima la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini nyinyi Azam mmeshaanza kutekeleza kwa vitendo na watu wote hatuwezi kuajiriwa serikalini, haiwezekani leo serikali ikaajiri watu wote.

“Inawezekana kabisa kila mtu na kipaji chake anaweza akafanya vizuri na mwisho wa siku akaendesha maisha yake, kwa hiyo tunawashukuru sana sana sana Azam FC,” alisema.

Makonda alichukua fursa hiyo pia kutoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitokeza, na kuiga mfano wa watu wa Azam FC ili kuwa na timu nyingi zenye ushindani na kuondoa migogoro kwenye soka la Tanzania.

“Waige mfano wa Azam, watengeneze timu zao, watengeneze viwanja ili tuwe na watu wengi, tuwe na timu nyingi zenye ushindani na hata hii migogoro migogoro inayotokea Yanga na Simba, wenye hela zao wasihangaike, kama wamegoma kukodishwa waje tu watengeneze timu zao ili na wenyewe waendelee kunufaika kwa sababu mwisho wa siku tunajua tukiwa na timu nyingi kama ilivyo Azam FC, ikapatikana timu nyingine ya watu wenye uwezo kama nyie mnavyowajali vijana wenu ushindani utakuwa mkubwa sana.

“Na hivyo ndivyo tunaweza kuweka vijana wengi wakawa kwenye vipaji vyao tukajenga uchumi wetu kupitia ajira inayotokana na michezo na mwisho wa siku tukapeperusha vema bendera ya Taifa letu katika mataifa mbalimbali katika sekta nzima ya michezo, mimi naamini kwa kazi na mfano mnaoonyesha niwaombe watu wengine waendelee kuiga,” alisema.

Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine Makonda amewaomba Watanzania waendelee kununua bidhaa zinazotengenezwa na wazawa akitolea mfano baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na makampuni ya Bakhresa.

“Mfano kama hivi viwanda vyenu vinatengeneza juisi, mnatengeneza maji, mnatengeneza ngano, walioajiriwa ni Watanzania wenzetu kwa hiyo kadiri mnavyouza bidhaa zenu manake kuna uhakika wa kupanua biashara, mkipanua biashara wadogo zetu, kaka zetu wanapata ajira lakini la pili mkiendelea kuuza mnalipa kodi, ile kodi tunapata barabara, madawa, tunapata shule, tunapata kila kitu tunachokitafuta,” alisema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, alimshukuru Makonda kwa ugeni wake huo ndani ya klabu hiyo, huku akichukua fursa hiyo pia kumwelezea historia fupi ya Azam tokea ianzishwe mwaka 2004 hadi ilipo mpaka sasa.

Mbali na historia, alimweleza timu mbalimbali zilizoko ndani ya Azam Complex, timu ya vijana (U-20) na ile ya wakubwa pamoja na mipango kabambe inayoendelea ya kuunda timu za vijana za chini ya umri wa miaka 15 na 17, mchakato unaoelekea ukingoni ukihusisha mikoa mbalimbali.

“Baada ya michuano ya Copa Coca Cola kutokuwa na mwelekeo, kama klabu tumeamua kuwafuata vijana kule walipo tumefanya majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam, tumekwenda Zanzibar, Tanga, Morogoro na wiki iliyopita tulikuwa mkoani Mbeya tulikopata vijana saba, bado tutaendelea kufanya uwekezaji tutaenda mkoani Tabora, Mwanza, Kigoma na Mtwara,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Kwa hiyo sisi tunaamini ya kuwa hata Mheshimiwa hapa Mkuu wa Mkoa utakuwa ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa wa kutusapoti na karibu sana Azam FC usichoke kuja wakati wowote…Yote tunayoyafanya ni kutokana na kampuni mama ya Azam na wadhamini wetu ambao ni Benki ya NMB lakini haitoshi kwa hiyo tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni mengine ambayo yanaweza kuona nafasi ya wao kuwekeza waje, tuna timu za vijana, njooni mfanye kazi na sisi tuweze kusomba mbele.”

IMETOLEWA NA AZAM FC [Kupitia Abducado Emmanuel November 22, 2016]