RIPOTI SPESHO

PEP GUARDIOLA – MASTAA ALIOKOROFISHANA NAO – IBRA, ETO’O, HART NA SASA YAYA!

PEP-YAYAJANA ulibuka mzozo mkubwa baada ya Meneja wa Manchester City Pep Guardiola kumtaka Wakala wa Yaya Toure, Dimitri Seluk, kumuomba radhi la sivyo Mchezaji huyo hatachezea tena Timu hiyo.

Seluk alijibu mara moja kuwa hataomba radhi na sasa ni wazi Yaya Toure atatoswa tu.

Mbali ya kupata mafanikio makubwa kama Kocha katika Miaka 8 iliyopita, Guardiola pia ana sifa kubwa ya kugombana na kuwatimua Mastaa wakubwa kwenye Timu zake.

Baadhi ya hao ni Zlatan Ibrahimovic, Samuel Eto'o, Joe Hart na sasa Yaya Toure ambae alimtema alipokuwa nae huko Barcelona na kumuuza kwa Man City.

Mara baada Guardiola kukabidhiwa mikoba huko Barca Mwaka 2008 aliwatangaza Mastaa wakubwa wa Timu hiyo, Ronaldinho, Deco na Eto'o, kwamba wataondoka.

Eto'o aliweza kubakia kwa vile tu walishindwa kumpata Fowadi mbadala kwa wakati.

Baada ya Msimu mmoja aliofunga Bao 36 na kuipa ushindi Barca kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI, Eto’o akaondoka kwenda Inter Milan ya Italy.

Eto’o aliwahi kuongea Mwaka 2014: “Guardiola hakuwa na ubavu wa kuongea vitu mbele yangu. Hatukusaliamiana!”

Kuondoka kwa Eto’o kulimleta Zlatan Ibrahimovic Barca akitokea Inter Milan na kuiwezesha Barca kutetea Ubingwa wa La Liga na kutwaa Kombe la Dunia kwa Klabu lakini wakatupwa nje ya Copa del Rey na pia Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI na Inter Milan.

Ibrahimovic nae akaingia matatani na Guardiola na Straika huyo wa Man United hivi sasa ameeleza: “Sikuwa na tatizo na Mtu yeyote. Miezi ya mwanzo ilienda vizuri na kisha kikatokea kitu nisichokijua hadi Leo. ‘Mwanafalsafa’ huyo [Akimaanisha Guardiola], aliacha kuongea na mimi!”

Ibrahimovic pia alidai Wachezaji wenzake huko Barca walikuwa kama Watoto wa Shule wakikaa kimya tu mbele ya Guardiola.

Ameeleza: “Chumba chetu cha Kubadili Jezi kilikuwa kimya. Messi, Xavi na Iniesta Siku zote walitii bila kusema lolote. Mie siko hivyo!”

Wakati utawala wake ukiendelea huko Nou camp, zipo ripoti kuwa Guardiola alikodi Wapelelezi kuchunguza maisha binafsi ya Wachezaji wake na mmoja wao alikuwa Gerard Pique ambae Guardiola alitaka kujua kama alikuwa akila laifu kwa Mapati ya Usiku na Mpenzi wake Staa Muimbaji Shakira.

Kutoboka kwa hili la Wapelelezi pia likafichua kuwa Guardiola aliwahi mtindo huo huo na kuwachunguza kina Ronaldinho, Deco na Eto'o maisha yao binafsi.

Akielekea kuondoka Nou Camp, ziliibuka taarifa kuwa Guardiola pia aliwahi kukwaruzana na Messi na Cesc Fabregas.

Hata alipotua huko Germany akiwa na Bayern Munich, Wachezaji walishikishwa adabu na kunyamazishwa lakini zipo ripoti wa ugomvi na Mfaransa Frank Ribery.

Alipoondoka Guardiola huko Bayern na nafasi yake kuchukuliwa na Kocha wa Italy, Carlo Ancelotti, Ribery alifunguka na kumkandya Guardiola kimafumbo: “Ancelotti anajua kuishi na Wachezaji. Ancelotti ni zawadi kwa Bayern na kwa yeye najiamini. Nahitaji Makocha kama yeye, Jupp Heynckes na Ottmar Hitzfeld!”

Akiwa Bayern, Guardiola alimtosa pia Lejendari wao Bastian Schweinsteiger na alipotua Man City tu shoka likatua kwa Kipa wa England Joe Hart na kumnyemelea Yaya Toure.

Toure na Guardiola wana historia ya uhasama iliyoanzia wote wakiwa huko Barcelona.

Baada ya Toure kuihama Barca na kumuacha Guardiola huko na yeye kutua City, Toure alieleza: “Kila nilipokuwa nikimuuliza kitu, Pep hunijibu vitu vya ajabu. Siku zote alinidharau hadi ilipokuja Ofa ya City. Hapo nikaamua kuondoka. Sikuongea na Guardiola Mwaka mzima. Kama angekuwa anaongea na mimi nisingeondoka. Mie nilitaka nimalizie Soka langu Barca. Lakini yeye hakuwa na Imani na mimi!”

Jana ndipo likaibuka hili sakata jipya la Toure na Guardiola pale Yaya Toure alipoambiwa na Meneja Pep Guardiola kwamba hatachezea tena Manchester City mpaka Wakala wake atakapoomba radhi kwa matamshi yake kwenye Vyombo vya Habari.

Mara baada ya kauli hiyo, Wakala wa Toure, Dimitri Seluk, akajibu mapigo na kumtaka Guardiola ndie aombe radhi kwa Manuel Pellegrini na Kipa Joe Hart.

Kauli ya Seluk kwa Vyombo vya Habari iliyoleta tafrani hiyo ni pale alipodai Guardiola amemfedhehesha Toure kwa kumuacha kwenye Kikosi cha Man City cha UCL, UEFA CHAMPIONZ LIGI Msimu huu.

Tangu Guardiola atue City mwanzoni mwa Msimu huu, Toure amecheza Mechi 1 tu kati ya 8 City walizocheza hadi sasa.

Guardiola ameeleza kuwa ilikuwa ngumu kwake kumuacha Toure kwenye Kikosi cha UCL.

Guardiola akaongeza: “Lakini Siku Wakala wake alipoongea, hapo hapo Yaya alikuwa nje. Nitakubali tu arejee ikiwa Dimitri Seluk ataongea kwa Rafiki zake wa Vyombo vya Habari na aiombe radhi Man City, na Wachezaji wenzake na Kocha, na hilo likitokea Yaya atakurudi Kundini na atakuwa na nafasi kucheza Mechi zote kama wengine.”

Wachambuzi wengi wanaamini Guardiola hampendi Toure kwani ni yeye aliemuuza Mchezaji huyo wa Ivory Coast kwa Man City walipokuwa wote huko Spain Klabuni FC Barcelona.

Hiyo Jana Wakala Seluk alitoboa: “Pep hataki Wachezaji Mastaa wenye haiba kubwa. Yeye anataka Wachezaji wanaomuogopa tu na kufanya kila analosema. Ndio maana alipotua City akaibua bifu na Yaya na Joe Hart, Wachezaji wakubwa hapo City!”

KASEJA GUMZO IVORY COAST, SERENGETI BOYS KAMBINI MAJUU!

KASEJA AACHA GUMZO IVORY COAST

Ivory Coast imeiondoa Tanzania katika mchezo wa mpira wa miguu wa ufukweni baada ya kushinda kwa mabao 6-4, lakini wamebaki na jina la Kipa Na. 1 wa timu ya Tanzania, Juma Kaseja wakisema: “Angekuwa tangu mwanzo, wangekuwa na wakati mgumu.”

Kaseja alikuwa kikwazo kwa Ivory Coast katika mchezo uliofanyika Jumamosi iliyopita huko jijini Abdijan ambako wenyeji walitamba kwamba wangeshinda mabao mengi, lakini kikwazo kilikuwa Kaseja na wakahoji wenyeji wa Tanzania: “Anacheza timu gani Tanzania, au mmemtoa nje ya nchi?”

“Kaseja alicheza kwa umahiri na kuzuia michomo mingi kutoka kwa washambuliaji wa Ivory Coast, na mabao aliyofungwa yalikuwa ni kwa bahati mbaya,” amesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu mara baada ya kurejea kutua jijini Dar es Salaam leo alfajiri.

Tanzania imeondolewa kwa jumla ya mabao 13-7 baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika hapa nyumbani kupoteza kwa mabao 7-3. Michezo hiyo ni ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni ambako fainali zake zitafanyika jijini Lagos, Nigeria Desemba, mwaka huu.

TFF imepanga kuhakikisha kwamba inaboresha soka la ufukweni baada ya kutengeneza uwanja maalumu wa mchezo huo ulioko kando ya Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

SERENGETI BOYS KUPIGA KAMBI NJE TENA

serengetiBaada ya kuifunga Congo-Brazzaville mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika, timu ya taifa Serengeti inatarajiwa kuondoka Alhamisi wiki hii kwenda kupiga kambi nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, taratibu zinapangwa kuhakikisha kwamba timu hiyo inakwenda kupiga kambi kwenye nchi tulivu inayolingana hali ya hewa na Congo Brazzaville kadhalika chakula pamoja na mazingira. Tanzania na Congo Brazzavile, zinatarajiwa kurudiana Oktoba 2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itakayopata ushindi wa jumla katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.

Katika mchezo uliofanyika jana Septemba 18, 2016 timu hiyo ya Tanzania maarufu kwa jina la Serengeti Boys ilipata mabao yake kupitia Yohana Mkomola na Abdi Makamba wakati yale ya Congo yalifungwa na Langa-Lesse Percy na Makouana Beni ambao mashabiki wa soka walikuwa wakiwalalamikia kuwa ni “wakubwa.”

Ili ifuzu kwa fainali zitakazofanyika mwakani huko Antananarivo, Madagascar katika fainali zitakazoanzia Aprili, 2017, Serengeti Boys inatakiwa ibaki na matokeo yake ya sasa na ihakikishe inapata ushindi na kama sare basi wapate bao kufuta faida ya bao la ugenini ambalo Congo Brazzaville walikuwa wanasheherekea  baada ya mchezo.

IMETOLEWA NA TFF

CAF U-17: SERENGETI BOYS YAICHAPA CONGO-BRAZZAVILLE 3-2!

>>WAKILINDA USHINDI HUO OKT 2 HUKO BRAZZAVILLE KUTINGA FAINALI MADAGASCAR!

serengetiTIMU ya Taifa ya Vijana ya Tanzania wa chini ya Miaka 17, Serengeti Boys, Leo huko Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wameifunga Congo-Brazzaville Bao 3-2 katika Mechi ya Kwanza ya Raundi ya Mwisho ya Mashindano ya CAF ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana U-17.

Bao za Serengeti zilifungwa na Yohana Oscar Nkomola, Bao 2, na Issa Abdi Makamba.

Congo walipata Bao zao kwa Penati ya Langa-Lesse Percy na Bopoumela Chardon Serengeti Boys inatarajiwa kurudiana na Congo huko Mjini Brazzaville hapo Oktoba 2 na Mshindi kutinga Fainali.

Fainali za Mashindano haya zitachezwa huko Nchini Madagascar kati ya Aprili 2 na 16 Mwakani 2017 na Timu ambazo zitafika Nusu Fainali za Mashindano hayo watakwenda kucheza Fainali za FIFA Kombe la Dunia U-17 huko India Mwakani 2017.

SERENGETI BOYS -Kikosi cha Leo:

Ally Msengi [Kevin Kayego. 73’], Ramadhan Kambwili, Nickson Kibabage, Enrick Nkosi, Israel Mwenda, Shaaban Zubeiry, Asad Ali, Kevin Naftali, Ibrahim Ali [Muhsin Makame, 48’], Yohana Nkomola [Issa Makamba, 65’], Mohamed Rashid Abdallah

TOKA TFF: OFA YA WAZIRI NAPE KUIONA SERENGETI LEO, WACHEZAJI WAJAZWA MINOTI!

serengetiKUONA SERENGETI NA CONGO –BRAZZAVILLE BURE, VIJANA WAJAZWA NOTI
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye ametoa ofa kwa wananchi kujumuika pamoja leo Septemba 18, 2016 katika mchezo wa mpira wa miguu utakaozikutanisha timu za vijana taifa za Tanzania na Congo-Brazzaville kwenye Uwanja wa Taifa, ulioko Chang’ombe, jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zitakutana kweye mchezo wa kwanza kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka. Zinatarajiwa kurudiana Oktoba 2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itafayopata ushindi wa jumla katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.
Nape alitoa ofa hiyo tangu jana Septemba 17, 2016 na leo asubuhi Septemba alipata kifungua kinywa na wachezaji wa Serengeti Boys ambako alitoa Sh 200,000 kwa kila mchezaji zilizotokana na kundi linalosapoti Serengeti Boys ambao walichangia Sh 2,600,000 wakati nyingine zilitoka kwa wadau wengine.
Nape ameahidi pia kununua bao moja kwa Sh 500,000 na atalipa fedha hizo kadiri ya idadi ya mabao hata kama yatafika 10 hivyo gharama yake itakuwa Sh 5,000,000. “Kuna wabunge na viongozi wengine wameahidi kutoa fedha zaidi, kwa hiyo Serengeti Boys kazi kwenu kutafuta ushindi leo mbele ya Watanzania watakaoingia uwanjani bure.”
Kuingia bure kesho ni ofa iliyotolewa na Nape ambako Rais Jamal Malinzi amemshukuru Nnauye ambaye ni Mbunge wa Mtama kwa ofa hiyo ambayo imelenga kutoa hamasa kwa Watanzania kwenda kushangilia timu yao.
Katika mchezo huo ambao Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, amesema kwamba amemaliza kila kitu na kwamba anasubiri Watanzania kuja uwanjani leo kuishangilia timu yao, utachezwa na waamuzi kutoka Shelisheli ambako mpiga kipenga atakuwa Nelson Fred akisaidiwa na Hensley Petrousse na Stive Marie wakati mwamuzi wa akiba akiwa Allister Barra. Kamishna wa mchezo atakuwa Gladmore Muzambi kutoka  Zimbawe.
IMETOLEWA NA TFF

DELE ALLI: JEZI YAKE MGONGONI SASA NI DELE BADALA ALLI BAADA KUFUTA UHUSIANO NA BABA YAKE!

DELE-ALLI-JINAKiungo wa England na Tottenham Hotspur Dele Alli sasa atavaa Jezi yake ikiwa na Jina la Dele badala ya Alli alilokuwa akitumia nyuma.

Akielezea uamuzi huo, Dele amesema: “Nilitaka Jina kwenye Jezi yangu ambalo litawakilisha mimi ni nani na sasa sina uhusiano na Jina la Alli. Huu si uamuzi niliochukua bila kufikiria. Nimefikiri sana na kuongea na Familia iliyo karibu yangu!”

Alli ni Jina la Baba yake Mzazi Dele mwenye asili ya Nigeria anaeishi huko USA na ambae aliachana na Mama yake Dele, Denise, Mwaka 1996 mara baada ya Ndoa yao.

Denise, ambae alikumbwa na ulevi wa kupindukia, ‘alimgawa’ Mwanawe Dele akiwa na Miaka 13 ili alelewe na Rafiki zake wa karibu Alan na Sally Hickford.

Hivi sasa Dele anawachukulia Mume na Mke, Alan na Sally Hickford, kama ndio Wazazi wake wa kufikia na yuko karibu nao mno.

Hivi karibuni, Mama Mzazi wa Dele, Denise, ambae bado ana urafiki na Mumewe wa zamani Kelly Alli, amefafanua: “Nilijua ‘kumgawa’ Dele kutampa nafasi pekee ya kutimiza ndoto yake ya kuwa Mchezaji wa Kulipwa. Ni ngumu kumtupa mwanao lakini huo ndio ulikuwa ukombozi wake. Nashukuru sana mafanikio yaliyotokea kwake!”

Nayo Klabu ya Tottenham imethibitisha kuwa Dele Alli atabaki na Jezi Namba 20 lakini Jina litabadiliwa kutoka ‘ALLI’ na kuwa ‘DELE’.

Stori hii inafana na ile ya Mchezaji wa Manchester United Memphis Depay ambae aliacha kutumia Jina la ‘DEPAY’ Mgongoni mwa Jezi yake na kubandika ‘MEMPHIS’ ili kutambua kutokuwa na uhusiano na Baba yake Mzazi alieiasi Familia yao yeye akiwa na Miaka minne tu.