RIPOTI SPESHO

VPL: TOTO, NA HIMAYA MPYA YA NGASSA, YAINYUKA KAGERA HUKO BUKOBA, MBEYA CITY, STAND UNITED NGOMA NGUMU!

VPL: LIGI KUU VODACOM

Ijumaa Oktoba 7

Matokeo:

Mbeya City 0 Stand United 0

Kagera Sugar 0 Toto African 2

++++++++++++++++++++++++

VPL-2016-17-LOGO-1TOTO AFRICANS ya Mwanza Leo hii imeibuka kidedea huko Kaitaba, Bukoba kwa kuifunga Kagera Sugar 2-0 kwenye Mechi ya VPL, Ligi Kuu Vodacom.

Wakicheza Mechi yao ya kwanza chini ya Kocha wao wa zamani Khalfan Ngassa, Toto walipata ushindi wao kwa Bao za Dakika za 47 na 80 zilizofungwa na Jamal Sudi na Mohammed Soud.

Ngassa amekamata wadhifa huu baada ya kuondoka kwa Kocha Rogasian Kaijage.

Ushindi huu umewaweka Toto Nafasi ya 11 wakiwa na Pointi 8.

Huko Sokoine Mjini Mbeya, Mechi nyingine ya VPL kati ya Mbeya City na Stand United ilimalizika kwa Sare ya 0-0.

VPL: LIGI KUU VODACOM

Jumamosi Oktoba 8

Ratiba:

Majimaji FC v Mbao FC

African Lyon v Ndanda FC

JKT Ruvu v Mtibwa Sugar

LIGI KUU VODACOM DIMBANI IJUMAA

TFF-HQ-1-1Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inatarajiwa kuendelea kesho Oktoba 7, 2016 kwa michezo miwili ambako Kagera Sugar itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja Kaitaba mkoani Kagera wakati Stand United itakuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Mbali ya mechi hizo za kesho, Jumamosi Oktoba 8, 2016 pia kutakuwa na michezo mitatu ambako Majimaji ya Songea itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati African Lyon itaikaribisha Ndanda FC jijini Dar es Salaam huku JKT Ruvu ikiialika Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi ulioko mkoani Pwani.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, kundi A Jumamosi Oktoba 8, kutakuwa na mchezo kati ya Pamba ya Mwanza na Polisi Dar kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam es Salaam wakati African Sports itakuwa mwenyeji wa Kiluvya United kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ligi hiyo ya Daraja la Kwanza itaendelea Jumapili Oktoba 9, 2016 kwa mchezo utakaozikutanisha Ashanti United na Friends Rangers; zote za Dar es Salaam. Kadhalika Jumatatu, kutakuwa na mchezo kati ya Mshikamano ya Dar es Salaam na Lipuli ya Iringa. Mchezo huo, pia utafanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kundi B; Jumamosi Oktoba 8, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Kurugenzi ya Iringa na Coastal Union ya Tanga ufakaofanyika huko Mufindi ukifuatiwa na michezo mitatu siku ya Jumapili Oktoba 9 ambayo Mlale itacheza na Majimaji ya Songea huko Uwanja wa Majimaji Njombe Mji itaikaribisha Kemondo wakati KMC itacheza na Mbeya Warriors kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Kundi C; Jumamosi Oktoba 8, mwaka huu Mvuvumwa ya Kigoma itacheza na Stand United ya Singida wakati Panamo itapambana na Alliance huku Polisi Dodoma itacheza na Polisi Mara wakati Jumapili Rhino ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Mgambo JKT ya Tanga.
IMETOLEWA NA TFF

SIMBA YAADHIBIWA KWA KUVUNJA VITI TAIFA!

 ==HAFLA KUIPONGEZA SERENGETI BOYZ!
HAFLA YA KUWAPONGEZA SERENGETI BOYS
TFF-HQ-1-1Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu,
Bunge na Vijana, Dk. Abdallah Possi amesema kwamba Serikali itaendelea
kusapoti michezo kwa sababu ya umuhimu wake, lakini akataka kutafutwa
mbinu za kuhakikisha wadhamini wanasapoti timu za taifa na klabu
mbalimbali zinazoshiriki ligi zinazosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Dk. Possi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwapongeza vijana wa
Timu ya Taifa ya Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti
Boys’, alisema kwamba fursa ipo ya kufanya vema katika michezo na
ndiyo maana Serikali inasapoti michezo kwa sababu ya kuleta faraja,
kuunganisha au kuleta umoja katika nchi yoyote kadhalika ni ajira.
Dk. Possi aliyesifu juhudi za TFF na timu hiyo, aliwapoza vijana hao akiwaeleza kuwa “Juhudi zilifanyika na mnaona kiwango kilichotumika kuandaa timu yenu. Matokeo mliyopata ndiyo mchezo. Kushindwa haina maana tumeishia hapa,” alisema Dk. Possi alipokuwa akiwapongeza vijana hao katika hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Ili kuepuka gharama kubwa za kuendesha timu hizo ambako Serengeti Boys imetumika karibu bilioni moja, Dk. Possi amesema kwamba kunahitajika kutengenezwa mfumo wa kupata wadhamini ili baadaye bidhaa za TFF zigombaniwe na hata kampuni zinazofanya biashara inayofanana zinaweza kuingia kudhamini katika ligi moja au klabu kwa sababu zitavuna maslahi.
Akiwageukia wachezaji, Dk. Possi alisema wachezaji hawana budi kuwa na nidhamu ya hali ya juu si katika kuonyesha kusabahi tu, bali kutunza mwili. “Mtafika mbali kama mkiwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja. Mna walimu, mna viongozi, ni vema mkawa mnawasikiliza wengine,” alisema Dk. Possi huku akitaja majina ya nyota waliofanikiwa kwa kuwa na nidhamu na wengine ambao walioanguka kwa kuwa na nidhamu mbovu.
Kabla ya kumkaribisha Dk. Possi, Rais wa TFF Jamal Malinzi alianza na kutoa taarifa ya matokeo huko Congo Brazzaville, akisema: “Ilikuwa siku mbaya sana kwangu. Watoto walikwenda kufia nchi. Lakini jahazi halijafika mwisho, kuvunjika kwa mpini, sio mwisho wa uhunzi. Userengeti Boys unakwisha na sasa unakuja Ungorongoro Heroes timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.”
Malinzi aliyetumia nafasi hiyo kumpa nafasi tena Kocha Mkuu wa vijana hao, Bakari Nyundo Shime alisema kikosi hicho kinapambana kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2019 na ili kujindaa timu hiyo inatarajiwa kwenda Korea Kusini kwenye mashindano maalumu itawasaidia kuongeza uwezo wenu, kutembea na kutafuta soko la kimataifa la soka.
Alisema kwamba mara baada ya timu hiyo kurejea, itakuwa inakusanhyika kila baada ya miezi mitatu ili kufanya mazoezi ya pamoja na kupata mchezo angalau mmoja wa kirafiki huku akitangaza kuwa vijana wa Mwanza, wanaosoma katika shule ya Alliance wanatarajiwa kuunda kikosi kipya cha timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
“Timu ile ya Mwanza ambayo kwa sasa ina vijana wa chini ya miaka 15, ndio watakaounda kikosi cha fainali za vijana ambazo zitafanyika hapa nchini mwaka 2018. Desemba watoto wale watacheza mechi ya kwanza ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, ambako watapigiwa wimbo wa taifa,” alisema Malinzi na kuongeza kuwa vijana walioibuliwa kutoka michuano ya Airtel Rising Stars nao watajumuishwa.
“Ligi ya wanawake inayokuja. Ndiyo nayo itazaa timu bora ya wanawake ambayoi itashiriki fainali za Kombe la Dunia hapo mwaka 2019. Ili tuweze kufanya yote haya, tunahitaji fedha na tayari tumeanzisha mfuko maalumu wa kuchangia timu hizi unaitwa TFF Fund ambao utakuwa na mtendaji wake na ofisi yake,” alisema na kuongeza, “Yote haya yanalenga Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2016.”
Timu hiyo iliyofanyiwa hafla, ilikuwa ikipambana kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini ikaondolewa na Congo Brazzaville kwa kufungwa bao 1-0 dakika za majeruhi hivyo kuondolewa kwa sheria za bao la ugenini. Mchezo wa kwanza Tanzania ilishinda 3-2 na katika mchezo wa marudiano, ilipoteza.
UAMUZI WA KAMATI YA BODI YA UENDESHAJI LIGI
Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga
faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) klabu ya Simba, kuiagiza ilipe
gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi
ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Oktoba
Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4,
2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya
aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza
mechi bila washabiki. Adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa
Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.
Vilevile kwa kuzingatia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu, Kamati imefuta adhabu ya kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi wa mechi hiyo kwa Jonas Mkude wa timu ya Simba baada ya kuthibitika bila mashaka kuwa nahodha huyo hakustahili kadi hiyo.
Mbali ya ripoti ya Kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo iliyoonyeshwa 'live', Kamati inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya, na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake.
Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuingia uwanjani baada ya mechi hiyo wakati yeye hakuwa miongoni mwa maofisa wa mechi waliotakiwa kuwepo katika eneo hilo.
Adhabu dhidi ya Manara ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(10). Eneo husika ni kwa ajili ya wachezaji, mabenchi ya ufundi, waamuzi, madaktari, huduma ya kwanza, wapiga picha na maofisa wengine wa mechi.
Klabu ya Azam imepigwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu kwenye mkono mmoja tu badala ya miwili ambapo ni kinyume na Kanuni ya 13(1), na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 13(6).
JKT Ruvu imepewa onyo na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya Msimamizi wa Kituo, na Ofisa wa Bodi ya Ligi kushambuliwa na mshabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Mshabiki huyo amefungiwa miezi 12, na iwapo vitendo hicho vitaendelea Uwanja huo utafungiwa kwa mechi za Ligi Kuu.
Mwamuzi Ahmed Seif amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kumudu mechi kati ya African Lyon na Mbao FC ikiwemo kutoa adhabu ya penalti ambayo haikuwa sahihi. Pia Mwamuzi huyo alipata alama za chini ambazo hazimruhusu kuendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
Pia Makamisha David Lugenge na Godbless Kimaro wamepewa onyo kwa kuwasilisha taarifa zenye upungufu katika mechi walizosimamia za raundi ya tano na saba.
Katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Mbeya Warriors imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kupitia mlango usio sahihi ikiwemo kuvunja kufuli kwenye mechi kati yao na Kimondo FC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Uwanja Vwawa mkoani Songwe. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Kwanza.
IMETOLEWA NA TFF
 

RAIS FIFA GIANNI INFANTINO ATAKA FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA ZIWE TIMU 48!

FIFA-GIANNI-INFANTINORAIS wa FIFA Gianni Infantino amependekeza Fainali za Kombe la Dunia ziwe na Nchi 48 badala ya 32 za sasa.
Infantino, Raia wa Italy mwenye Miaka 46 aliteuliwa Februari Mwaka huu kumrithi Sepp Blatter, amesema Timu 16 kati ya hizo 48 zitatolewa nje ya Fainali hizo baada ya kuchezwa Raundi ya Awali ya Mtoano huko huko kwa Mwenyeji wa Mashindano na baada ya Raundi hiyo mfumo utakuwa kama wa sasa wa Makundi 8 ya Timu 4 kila moja ambapo Timu 2 za juu za kila Kundi zitasonga Raundi ya Mtoano.
Kwenye Nchi 48 zitakazoingia Fainali 16 zenye Ubora wa juu kwenye Listi ya FIFA ya Ubora Duniani hazitacheza hiyo Raundi ya Awali ya Mtoano na kuacha 32 zikiingizwa kwenye Droo kupanga Mechi zao za Mtoano ili kutinga Makundi.
 Infantino amesema hivi sasa yapo majadiliano kuhusu mapendekezo hayo na uamuzi wa mwisho utafanywa Januari Mwakani.
Wakati wa Uchaguzi wa Rais wa FIFA mapema Mwaka huu, Infantino alisema ataongeza Nchi kwenye Fainali za Kombe la Dunia kuwa 40 kutoka 32 za sasa na kuipa Afrika nafasi nyingi zaidi badala ya 5 za sasa.

CAF U-17: BAO LA DAKIKA YA 90 LAIKATILI SERENGETI KUTINGA FAINALI!

serengetiBAO la Dakika ya 90 la Mountou limewapa Vijana wa chini ya Miaka 17 wa Congo Brazzaville ushindi wa 1-0 walipocheza na wenzao wa Tanzania, Serengeti Boys, na kuwaingiza Fainali za CAF huko Madagascar.
Ushindi huo umeifanya Congo ifungane 3-3 na Serengeti Boys kwa vile 3-2 Jijini Dar es Salaam lakini wamesonga kwa Magoli ya Ugenini.
Congo ni miongoni mwa Nchi nyingine 7 wakiwemo Wenyeji Madagascar kucheza Fainali zitakazopigwa Mwakani kati ya Aprili 2 na 16.
Timu zitakazotinga Nusu Fainali ya Fainali hizo zitapelekwa India Mwakani kucheza Mashindano ya FIFA ya Kombe la Dunia kwa U-17.
CAF U-17: NCHI ZILIZOTINGA FAINALI:
Angola
Cameroon
Congo
Ghana
Guinea
Madagascar (hosts)
Mali
Niger
CAF U-17
Jumapili Oktoba 2
Matokeo:
**Kwenye Mabano Jumla ya Mabao kwa Mechi 2
Congo 1 Tanzania 0 (3-3)
Cameroon 5 Sudan 1 (7-5)
Ethiopia 1 Mali 2 (1-4)
Jumamosi Oktoba 1
Ivory Coast 0 Ghana 0 (1-3)
Gabon 3 Niger 3 (3-4)
Comoros 0 Angola 2 (0-7)