RIPOTI SPESHO

NINGEKUWA JOSEPH OMOG…

NA MWANDISHI WETU
received 1116885805076862KWA siku hizi mbili yaani jana na leo, wamiliki wa boti zinazopiga ruti zao kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea visiwani Zanzibar, wamekuwa na furaha kutokana na biashara ya usafirishaji kufanya vizuri kutokana na abiria kumiminika kwa wingi.
Idadi hiyo ya abiria kuwa wengi inatokana na mpambano wa kukata na shoka wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Yanga, itakayopigwa leo usiku kwenye Uwanja wa Amaan.
Ni mpambano ambao utawafanya baadhi ya mashabiki kutoa machozi baada ya dakika 90 kumalizika na wengine kubaki wakicheka kwani lazima mshindi apatikane hata kwa kurusha shilingi.
Kama Simba wataibuka na ushindi mashabiki wao watauona mwaka huu ni wa neema kwao na wale wa Yanga watajiona wenye mkosi.
Na iwapo Wanajangwani hao watapata ushindi itakuwa ni furaha isiyo na kifani huku mitaa ya Msimbazi ikitawaliwa na vilio.
Kila shabiki anatamani timu yake iibuke na ushindi lakini yote kwa yote, matokeo yatakayopatikana ndani ya dakika 90 ndiyo yatakayoamua nani wa kununa na nani wa kuangua kicheko cha furaha. Ngoja tusubiri kwani kila timu inaonekana kujiandaa vilivyo.
Yanga wataingia katika mchezo huo wakitaka kuwatuliza mashabiki wao baada ya kukung’utwa mabao 4-0 na Azam FC huku Simba wao wakitaka kuendelea kuwafurahisha mashabiki wao kwani hawajapoteza mchezo wowote kwenye michuano hiyo.
Ni ukweli ulio wazi kuwa timu hizi zinapokutana ni ngumu kutabiri matokeo ya haraka kwani timu inayoonekana mbovu inaweza ikafanya jambo la kushangaza na hilo limezoeleka.
Ni kweli kwamba Simba msimu huu wanaonekana kujiimarisha zaidi na kusaka makombe lakini jambo la kufurahisha kwa Yanga ni kwamba hawajafanya usajili mkubwa msimu huu. Wachezaji wamezoeana vilivyo na hiyo inaweza ikaufanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi.
Binafsi kama ningekuwa kocha wa Simba, Joseph Omog, kuna baadhi ya mambo ambayo ningeyafanya katika mchezo huo ili kuhakikisha ninawazidi ujanja Yanga na kupeleka furaha kwa mashabiki wangu ikizingatiwa kuwa matokeo ya sare hayataamua mchezo.
Katika michezo miwili iliyopita Omog amemtumia kipa Manyika Peter na kijana huyo amerudisha fadhila kwa kuonesha kiwango cha kuridhisha.
Lakini kwenye mchezo wa Yanga, iwapo ningekuwa Omog ningemrudisha golini Daniel Agyei. Unajua kwanini? Ni kwa sababu ya uzoefu wake wa kimataifa utakaompa nguvu ya kushughulika na presha ya mchezo wa Simba na Yanga.
Ni kweli kwamba mpambano wa Simba na Yanga una siasa zake lakini Agyei anaweza kucheza vizuri zaidi ya Manyika na faida kubwa atakayoileta kipa huyo ni kwamba, anaweza kuzungumza vizuri na mabeki wake.
Kwa upande wa mabeki, kama mimi ndiye Omog nisingefanya mabadiliko yoyote kwani hao waliopo wameshaanza kuzoeana vizuri na katika eneo la kiungo wa kati wala nisingethubutu kumwanzisha James Kotei na badala yake Jonas Mkude na Mzamiru Yassin wangekuwa na nafasi kubwa na baadaye nitamtumia Said Ndemla kama silaha mbadala iwapo nitaihitaji.
Unadhani ni kipi ambacho kinanishawishi nifanye hivyo? Ni hiki, kiungo cha Yanga kinabebwa na watu wawili, Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima.
Viungo wajanja, waliozoeana hivyo wanatakiwa kukutana na wajanja wenzao vinginevyo mambo yanaweza kuharibika kwani ukimpa nafasi mtu kama Niyonzima bila shaka akina Donald Ngoma watakuwa na kazi rahisi ya kufunga kutokana na pasi zake maridhawa na uwezo wa kupangua ngome za ulinzi.
Kuhusu mawinga, nafasi ya Shiza Kichuya itakuwepo kwenye mchezo huo na ningemwongeza Jamal Mnyate ambaye katika michuano hii amekuwa akitokea benchi na anapoingia unaona wazi kasi ikiongezeka na kuwafanya mabeki wa timu pinzani kuwa na presha kubwa.
Washambuliaji wa mwisho hakuna shaka ningewaanzisha Juma Luizio na mwenzake Laudit Mavugo ambaye kwa sasa anaonekana kuanza kurudi kwenye kiwango chake tofauti na awali na hii inaweza ikawapa presha kubwa akina Kelvin Yondani.
Lingine kubwa ambalo ningewashauri wachezaji wangu, kwanza kabisa ni kutoingiwa na presha yoyote na pia kuendelea na soka la kwenye kitabu, pasi fupifupi na za uhakika huku nikiendelea kutumia mfumo wa 4-4-2 ambao unaonekana kuwakubali zaidi Simba.

TUZO ZA CAF 2016: MAHREZ, ONYANGO NDIO BORA AFRIKA!

>>DIAMOND PLATINUMZ ATUMBUIZA KWENYE HAFLA!

MAHREZ-CAF-BORAKWENYE HAFLA iliyofanyika Jana ndani ya International Conference Centre huko Abuja, Nigeria Winga kutoka Algeria anaewachezea Mabingwa wa England Leicester City, Riyad Mahrez, ameteuliwa kuwa ndie Mchezaji Bora Afrika kwa Mwaka 2016 huku Kipa wa Uganda Denis Onyango akitwaa Tuzo kama hiyo kwa Wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika.

Mahrez, mwenye Miaka 25, amekuwa Mualgeria wa kwanza kushinda Tuzo hiyo kwa kuzoa Kura 361 akiwashinda Mshindi wa 2015 Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon na Borussia Dortmund aliepata Kura 313 na Sadio Mane wa Senegal na Liverpool aliepata Kura 186.

Kura kwa Washindi zilipigwa na Makocha Wakuu wa Timu za Taifa Wanachama wa CAF, Wajumbe wa Kamati ya Habari ya CAF na Kamati Ufundi na Maendeleo ya CAF na Jopo la Mabingwa 20.

Onyango, mwenye Miaka 31, ambae pia ni Kipa wa Mabingwa wa Afrika kwa Klabu, Mamelodi Sundowns, ameweka Historia kuwa Kipa wa Kwanza kutwaa Tuzo hii.

Tuzo nyingine zilizotolewa Jana ni:

-Mchezaji Bora kwa Wanawake: Asisat Oshoala [Nigeria]

-Kipaji che Matumaini: Kelechi Iheanacho [Nigeria]

-Mchezaji Bora Kijana: Alex Iwobi [Nigeria]

-Klabu Bora: Mamelodi Sundowns

-Kocha Bora: Pitso Mosimane [Mamelodi Sundowns]

-Timu ya Taifa Bora: Uganda

-Refa Bora: Bakary Papa Gassama [Gambia]

-Kiongozi Bora: Manuel Lopes Nascimento [Guinea Bissau]

-Malejendari: Laurent Pokou [Ivory Coast] & Emilienne Mbango [Cameroon].

Kwenye Hafla hii ya Tuzo za Ubora Afrika Wanamuziki waliotumbuiza walikuwa ni Femi Kuti, Flavour, Yemi Alade na Omawumi, wote kutoka Nigeria, Kundi la Afrika Kusini, Muffinz, na Diamond Platinumz wa Tanzania.

CAF-XI

KARIBU KARIAKOO, EMMANUEL MARTIN

Na Ally Kamwe

YANGA-MARTINSKaribu Kariakoo, Emmanuel Martin.

Karibu Dar es salaam kwa Mheshimiwa Paul Makonda, karibu sana katika jiji la maajabu.

Ni ardhi hii aliyozikwa Steven Kanumba na filamu zake, ni sehemu hii hii anapoteketea Chid Benz na umwamba wake, nini zaidi unahitaji kujuzwa kuhusu Dar es salaam?

Kila mtu ana sura yake na moyo wake hapa, usidanganyike na vicheko vyao. Wabaya na wazuri wanaishi hapa!

Unataka starehe? Zipo hapa, mpaka zile zisizompendeza shetani. Hii ndio Dar es salaam tamu iliyomkimbiza Mr Nice na kumfedhehesha 20 Percent akiwa na utamu wake.

Hili ndilo jiji pekee duniani wanakopatikana watu aina ya Shilole, Snura, Amber Lulu na Giggy Money kwa wakati mmoja.

Wako wazuri hapa wa kila rangi na utakutana nao kama alivyokutana nao mahotelini Andrey Coutinho kipindi kile, uamuzi ni wako kijana mwenzangu.

Karibu sana Emmanuel.

Kama umekuja na akili zako kama alivyokuja nazo Farid Mussa kipindi kile, bila shaka una pepo yako ndogo ya kuishi pale Kariakoo.

Ila kama umekuja na mabegi tu kama alivyokuja nayo Malimi Busungu, jiandae kuishangaa Kariakoo kama anavyoishangaa Mahadhi Juma hivi sasa, jiji limekosa adabu hili.

Nilivyokutazama na niliyoyasikia baada ya ule mchezo wa Yanga dhidi ya Ndanda, hakika nafsi yangu ilijiridhisha kuwa ‘Dar es salaam imepata mtu wao’

Lile jiji la maajabu sasa limepata mtu wake wa maajabu!

Wakati huu huruma yangu iko Deus Kaseke, najua yuko kwenye vita kubwa na nafsi yake.

Uwezo wa Emmanuel unatishia moja kwa moja nafasi yake katika kikosi cha kwanza.

Kaseke anatakiwa kupambana sana kama ambavyo Geofrey Mwashiuya anavyotakiwa kuamka usingizini, asipokubali kuamka kwa hiari yake, ule mguu wa kushoto wa Emmanuel utamlaza milele.

Bahati nzuri Emmanuel amekuja Yanga na amekutana na George Lwandamina.

Kocha anayemaini uwezo kabla ya jina, kocha anayetengeneza mfumo utakaofatwa na wachezaji na si kuwa na mfumo utakaofata wachezaji.

Sikushangaa na sitashangaa kama Said Makapu ataendelea kumburuza benchi Justice Zulu ‘Mkata umeme’, sitashangaa hata kidogo.

Macho yakishamdanganya Lwandamina, hana muda tena wa kuliamini sikio.

Emmanuel hakwenda Yanga kwa nguvu ya viongozi kama wanavyokwenda wengine, hayuko pale kwa bahati mbaya, uwezo wake ulionekana na kocha ndiye aliyependekeza asajiliwe.

Mara ngapi unaona hili likitokea kwenye usajili wa Bongo uliotawaliwa na tabia za watu wa ‘bongo movie’?

Emmanuel ana muda mwingi sana wa kucheza Yanga, ana muda mwingi wa kukuza kiwango chake na kuzihamisha ndoto zake kuwa kweli.

Yanga ni mahala sahihi sana kwake kwa wakati huu, kwanini? Sababu ni mbili tu. Moja, Atacheza mechi nyingi kubwa, hivyo atapata uzoefu na mbili, yuko kwenye barabara ya kwenda Ughaibuni.

Ndio, michuano ya Ligi ya mabingwa ni ndoto za wachezaji wengi wa Kiafrika, Yanga wataanza kucheza Februari mwaka huu, ni fursa kwa Emmanuel kuonyesha thamani yake kwa faida ya klabu na maendeleo yake binafsi.

Akili yake inatakiwa kutulia mara mbili zaidi anavyotulia akiwa na mpira mguuni, ni wakati wake wa kufungua macho na kuchagua njia anayotaka kupita.

Anataka sifa na makelele ya Kariakoo? Kipo kiti cha Mrisho Ngassa ambacho hakijapata mtu wa kukikalia mpaka leo hii, ziko laki na viroba vya mchele vinamsubiri kama akiamua kuwa ‘mfalme wa Kariakoo’.

Ila kama nafsi yake ina wivu wa kufika alipofika Mbwana Samatta au anapokwenda Farid Mussa, nafasi na wakati ni huu.

Magazeti hayataacha kuandika habari zake, akifanya vyema yatasifia, akiboronga atashughulikiwa vilevile, asiyaweke sana akilini japo ni changamoto anayotakiwa kuizoea kuanzia sasa.

Binafsi nimeona nuru kubwa ikiangaza ndani yake, nimemuona mchezaji mkubwa wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu baadae kama nilivyowahi kumtazama Shiza Kichuya.

Wao ndio mashujaa wa maisha yao na wataamua kilicho sahihi kwao. Kitu pekee anachotakiwa kukumbuka kwa sasa, yuko Kariakoo iliyo ndani ya jiji la Dar es salaam, mengi yasiowezekana kwingine, hufanyika kirahisi sana hapa.

MAPINDUZI CUP: YAANZA, TAIFA JANG’OMBE YAWATUNGUA ‘WAPWA’ ZAO JANG’OMBE BOYS!

AMAAN-STADIUM-17MASHINDANO ya Kombe la Mapinduzi ya kuenzi Mapinduzi tukufu ya Visiwa vya Zanzibar na Pemba yameanza Usiku huu huko Amaan Stadium, Zanzibar kswa Timu pinzani kucheza na Taifa Jang’ombe kuifunga Jang’ombe Boys 1-0 kati Mechi ya Kundi A.

Bao la ushindi la Taifa Jang’ombe lilifungwa Dakika ya 83.

Michuano yapo na Makundi Mawili na Kundi A lina timu za Simba ya Dar es Salaam, Taifa ya Jang’ombe, Jang’ombe Boys, KVZ na Mabingwa Watetezi, URA ya Uganda.

Kundi B lina Timu za Yanga, Azam FC, Jamhuri na Zimamoto.

+++++++++++++++++

MAKUNDI:

KUNDI A

-Simba

-Taifa Jang;ombe

-Jang’ombe Boys

-KVZ

-URA [Mabingwa Watetezi, Toka Uganda]

KUNDI B

-Yanga

-Azam FC

-Jamhuri

-Zimamoto

+++++++++++++++++

Baada ya Mechi hii ya Leo, Januari 1 Mabingwa Watetezi, URA watacheza na KVZ kuanzia Saa 10 Jioni na baadae Simba kumenyana na Taifa ya Jang'ombe Saa 2 na Nusu Usiku.

Mechi za Kundi B zitaanza Januari 2, kwa Azam FC kucheza na Zimamoto kuanzia Saa 10 Jioni na Yanga kuivaa Jamhuri Saa 2 na Nusu Usiku.

KOMBE LA MAPINDUZI

Ratiba/Matokeo:

Desemba 30, 2016

Taifa Jang'ombe 1 Jang'ombe Boys 0

Januari 1, 2017

KVZ VS URA (Saa 10:00 jioni)

Simba vs Taifa Jang'ombe (Saa 2:30 usiku)

Januari 2, 2017

Azam vs Zimamoto (Saa 10:00 jioni

Yanga vs Jamhuri (Saa 2:30 usiku)

Januari 3, 2017

Jang'ombe Boys vs URA (Saa 10:00 jioni)

KVZ vs Simba (Saa 2:30 usiku)

Januari 4, 2017

Zimamoto vs Yanga (Saa 10:00 jioni)

Jamhuri vs Azam saa 2:30 usiku.

Januari 5, 2017

KVZ vs Jang'ombe Boys (Saa 10:00 jioni)

Simba vs URA (Saa 2:30 usiku)

Januari 6, 2017

Taifa Jang'ombe vs KVZ (Saa 2:30 usiku)

Januari 7, 2017

Jamhuri vs Zimamoto (Saa 10:00 jioni)

Yanga vs Azam (Saa 2:30 usiku)

Januari 8, 2017

Simba vs Jang'ombe Boys (Saa 10:00 jioni)

Taifa Jang'ombe vs URA (Saa 2:30 usiku).

Januari 10, 2017

Nusu Fainali

Nusu Fainali ya kwanza (Saa 10: 00 jioni)

Nusu Fainali ya Pili (Saa 2:30 usiku)

Januari 13, 2017

FAINALI

Saa 2: 30 usiku.

BAADA KUZOA TUZO NYINGINE, RONALDO: '2016 NI MWAKA BORA KWANGU!'

>’WANAONITILIA SHAKA, HUU NDIO USHAHIDI!’

GLOBAL-SOCCER1STAA wa Real Madrid na Portugal Cristiano Ronaldo ametoboa kuwa Mwaka 2016 ndio Mwaka Bora kwake hadi sasa baada ya kutwaa Tuzo nyingine, safari hii ikiwa ni ile ya Globe Soccer Award.

Mwaka huu, Ronaldo aliiwezesha Real Madrid kutwaa UEFA CHAMPIONZ LIGI na pia Nchi yake Portugal kubeba EURO 2016 huku Majuzi tu Real Madrid ikitwaa FIFA Kombe la Dunia kwa Klabu.

Mapema Mwezi huu, Ronaldo alitwaa Tuzo iliyotukuka ya Ballon d'Or ya Mchezaji Bora Duniani kwa Mwaka 2016.

Jana, huko Dubai, Ronaldo alitajwa kuwa ndio Mshindi wa Tuzo nyingine kubwa iitwayo Globe Soccer Award.

Akiongea kuhusu Tuzo hii mpya, Ronaldo alisema: “Kwa ujumla na binafsi, pengine huu ndio Mwaka Bora mno kwangu!”

Aliongeza: “Tumeshinda UEFA CHAMPIONZ LIGI na Real Madrid, tulitwaa Taji kubwa na Portugal, nilishinda Ballon d'Or, Kombe la Dunia kwa Klabu. Siwezi kuomba zaidi!”

Alimaliza: “Kwa Watu wanaonitilia shaka me, Real Madrid na Timu ya Taifa, sasa wana ushahidi. Tumeshinda kila kitu!”

Ronaldo aliwashukuru Wachezaji wenzake wote.

Nae Kocha wa Timu ya Taifa ya Portugal, Fernando Santos, ametajwa kuwa ndio Kocha wa Mwaka katika Sherehe hizohizo za Tuzo za Globe Soccer Award.

Real Madrid ndio iliyopewa Tuzo ya Timu Bora ya Mwaka, Jorge Mendes akichaguliwa kuwa Wakala Bora wa Mwaka huku Refa Bora wa Mwaka ni Mwingereza Mark Clattenburg.

Tuzo hizo zilikabdhiwa na Rais wa FIFA Gianni Infantino.

GLOBAL-SOCCER2

Habari MotoMotoZ