RIPOTI SPESHO

MAPINDUZI YA SOKA: MECHI ZA DAKIKA 30 KILA KIPINDI, KUBADILI MUUNDO WA FRIKIKI MBIONI!

>IFAB YAJA NA KABRASHA 'CHEZA KWA HAKI'!

IFAB, Chombo pekee chenye uwezo wa kubadili Sheria za Soka, kimekuja na mapendekezo kadhaa ya kubadili sura ya Gemu ya Soka ili kuleta haki na mvuto zaidi.

FIFA-VARS2Kubwa ni kufanya kila Kipindi cha Mechi kiwe Dakika 30 za Mchezo halisi na si Dakika 45 za sasa na pia kuruhusu Mpiga Frikiki na Kona kuucheza Mpira mwenyewe badala ya kwanza kumpasia mwingine.

Mapendekezo haya sasa yamo kwenye majadiliano na Mwezi Machi Mwakani, kwenye Kikao cha IFAB, yanaweza kupitishwa ili yaanze Majaribio.

Hivi sasa IFAB, International Football Association Board, imetoa Kijitabu kiitwacho, ‘Cheza kwa Haki!’ ['Play Fair!'] ambacho nia yake ni kuboresha Kanuni za FIFA za Mchezo wa Haki.

Mapendekezo yaliyomo kwenye Kijitabu hicho yana nia ya kuleta heshima zaidi kwa Waamuzi na Sheria za Soka lakini pia kuongeza Muda wa Kuchezwa Soka Uwanjani na kuleta mvuto zaidi.

Mapendekezo hayo yanalenga kuongeza muda halisi wa uchezaji Soka na kupunguza upotezaji muda kwani utafiti umebaini kuwa ingawa Mechi hupaswa kuchezwa Dakika 90 lakini ukweli ni kuwa Mchezo halisi, yaani wakati ule Wachezaji wanaucheza na kuugusa Mpira, hauzidi Dakika 60 katika kila Mechi kwani mara nyingi huwepo upotezaji muda, mwingine wa makusudi.

Sasa IFAB itajadili kupunguza Vipindi vya Mechi kuwa Dakika 30 kila Kipindi huku Saa ikisimama wakati Mpira ukiwa umetoka nje ya Uwanja au pale Gemu ikiwa imesimamishwa ili kulinda Dakika 30 za Mchezo halisi zibaki hizo hizo 30.

Pia, watajadili kumruhusu Mpiga Frikiki kuucheza Mpira mwenyewe baada ya yeye kupiga Frikiki badala ilivyo sasa kwamba lazima ampasie Mtu ili auguse tena yeye.

Hilo limeonekana litafanya Gemu iende haraka bila kusimama sana kwani Mchezaji akifanyiwa Faulo yeye mwenyewe anaweza kuanzisha Gemu kwa moja kwa moja kuicheza ile Frikiki na kusonga akipiga Chenga.

Mengine yaliyo kwenye mjadala huu ni ufafanuzi wa Sheria ya Kuunawa Mpira na kupiga Filimbi za Haftaimu na Kumaliza Mpira pale tu Mpira ukiwa umetoka nje ya Uwanja na si wakati Gemu ikiendelea.

Jingine ni kuhusu Penati ambapo mabadiliko ni kuwa ikipigwa basi iwe Goli au ikiokolewa au kugonga Posti basi hapo hapo huamriwa kuwa Golikiki na si kuruhusu Mpira uendelee.

Hilo la kusimamisha na kutoa Golikiki baada ya Mkwaju wa Penati kukoswa linalenga kufuta ule utata wa Wachezaji kuingia ndani ya Penati Boksi kabla Penati haijapigwa kwa lengo la kuokoa ikiwa Kipa atacheza au Mpira kupiga Posti.

++++++++++++++++++++++

CHEZA KWA HAKI - Baadhi ya Mapendekezo:

REFA ATASIMAMISHA SAA YAKE,ambayo inaungana na Saa kubwa Uwanjani itakayoonwa na Watazamaji wote, [ILI KULINDA DAKIKA ZA MCHEZO HALISI ZIBAKI 30] pale:

-Anapotoa Penati hadi ipigwe.

-Anapokubali kuwa ni Goli hadi Mpira utakapoanza tena.

-Anaposimamisha Mpira baada ya Mchezaji kuumia hadi Mpira utakapoanza tena.

-Akimwonyesha Kadi Mchezaji hadi Mpira utakapoanza tena.

-Mechi inaposimama ili Timu kubadili Mchezaji hadi Mpira uanze tena

-Anaposimamisha Gemu kwa ajili ya Frikiki hadi inapopigwa.

MAPENDEKEZO MENGINE NI:

-Kujipasia na kucheza mwenyewe kutoka Frikiki, Kona na Golikiki.

-Saa kubwa Uwanjani iliyoungana na ya Refa inayosimama Refa akisimamisha Saa yake.

-Kuruhusu Golikiki kuchezwa hata kama Mpira haujasimama tuli, yaani ukiwa unazunguka.

-Tafsiri safi ya Kuunawa Mpira

-Mchezaji anaefunga Goli au kuzuia Goli kufungwa kwa Mkono apewe Kadi Nyekundu.

-Kipa anaedaka Mpira aliorudishiwa nyuma na Beki wake au kudaka Mpira wa Kurushwa, ipigwe Penati.

-Refa ataamuru ni Goli ikiwa Mchezaji atazuia Mpira kutinga Wavuni kwa Mkono akiwa Golini.

++++++++++++++++++++++

Wakati mengi ya Mapendekezo hayo ya IFAB inabidi kwanza yajadiliwe, yapo yale ambayo hayahitaji mjadala na yanaweza kujaribiwa kuanzia sasa.

Hayo ni pamoja na Mabeki kuruhusiwa kupokea Pasi kutoka Golikiki hata kama wako ndani ya Penati Boksi yao ili kurahisisha kuucheza Mpira kutoka nyuma na jingine ni Mfumo wa Upigaji Mikwaju ya Penati.

Mfumo huo wa upigwaji Penati mpya, unaoitwa ‘ABBA’, ni ule wa Timu A kupiga Penati ya Kwanza, kisha Timu B kupiga Penati 2 mfululizo na kufuatia Timu A kupiga 2 zinazofuatia na kuendelea kwa kupokezana.

Yaani mpangilio wa upigaji ni A, B, B, A…ABBA…mpaka Penati Tano Tano zinamalizika.

Mbali ya Mfumo huo wa Upigaji Penati ambao sasa uko Majaribioni, pia kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara yaliyoanza Jana huko Russia, kunajaribiwa amri ya kuruhusu Manahodha wa Timu pekee kuruhusiwa kumfuata na kuongea na Refa ili kufuta ile tabia ya Wachezaji wa Timu nzima kumzonga Refa.

Ili Mapendekezo yaliyomo kwenye ‘Cheza kwa Haki!’ yapite inabidi yabarikiwe kwa Kura za IFAB ambao Memba wake ni FIFA, Asilimia 50, na Wawakilishi kutoka Vyama vya Soka vya England, Wales, Scotland na Northern Island, Vyama ambavyo ndio vinatambulika kuwa ndio Waanzilishi wa Gemu ya Soka na hivyo wao pekee, pamoja na FIFA, ndio pekee wenye Mamlaka ya Kubadili Sheria za Soka.

Mabadiliko yeyote ya Sheria za Soka yatapitishwa tu ikiwa zitapatikana Kura Robo Tatu za Memba Halali wa IFAB na hii inamaanisha FIFA pekee haiwezi Kubadili Sheria bila Sapoti ya Vyama vya Soka vya Waanzilishi.

 

Habari MotoMotoZ