RIPOTI SPESHO

NINGEKUWA JOSEPH OMOG…

NA MWANDISHI WETU
received 1116885805076862KWA siku hizi mbili yaani jana na leo, wamiliki wa boti zinazopiga ruti zao kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea visiwani Zanzibar, wamekuwa na furaha kutokana na biashara ya usafirishaji kufanya vizuri kutokana na abiria kumiminika kwa wingi.
Idadi hiyo ya abiria kuwa wengi inatokana na mpambano wa kukata na shoka wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Yanga, itakayopigwa leo usiku kwenye Uwanja wa Amaan.
Ni mpambano ambao utawafanya baadhi ya mashabiki kutoa machozi baada ya dakika 90 kumalizika na wengine kubaki wakicheka kwani lazima mshindi apatikane hata kwa kurusha shilingi.
Kama Simba wataibuka na ushindi mashabiki wao watauona mwaka huu ni wa neema kwao na wale wa Yanga watajiona wenye mkosi.
Na iwapo Wanajangwani hao watapata ushindi itakuwa ni furaha isiyo na kifani huku mitaa ya Msimbazi ikitawaliwa na vilio.
Kila shabiki anatamani timu yake iibuke na ushindi lakini yote kwa yote, matokeo yatakayopatikana ndani ya dakika 90 ndiyo yatakayoamua nani wa kununa na nani wa kuangua kicheko cha furaha. Ngoja tusubiri kwani kila timu inaonekana kujiandaa vilivyo.
Yanga wataingia katika mchezo huo wakitaka kuwatuliza mashabiki wao baada ya kukung’utwa mabao 4-0 na Azam FC huku Simba wao wakitaka kuendelea kuwafurahisha mashabiki wao kwani hawajapoteza mchezo wowote kwenye michuano hiyo.
Ni ukweli ulio wazi kuwa timu hizi zinapokutana ni ngumu kutabiri matokeo ya haraka kwani timu inayoonekana mbovu inaweza ikafanya jambo la kushangaza na hilo limezoeleka.
Ni kweli kwamba Simba msimu huu wanaonekana kujiimarisha zaidi na kusaka makombe lakini jambo la kufurahisha kwa Yanga ni kwamba hawajafanya usajili mkubwa msimu huu. Wachezaji wamezoeana vilivyo na hiyo inaweza ikaufanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi.
Binafsi kama ningekuwa kocha wa Simba, Joseph Omog, kuna baadhi ya mambo ambayo ningeyafanya katika mchezo huo ili kuhakikisha ninawazidi ujanja Yanga na kupeleka furaha kwa mashabiki wangu ikizingatiwa kuwa matokeo ya sare hayataamua mchezo.
Katika michezo miwili iliyopita Omog amemtumia kipa Manyika Peter na kijana huyo amerudisha fadhila kwa kuonesha kiwango cha kuridhisha.
Lakini kwenye mchezo wa Yanga, iwapo ningekuwa Omog ningemrudisha golini Daniel Agyei. Unajua kwanini? Ni kwa sababu ya uzoefu wake wa kimataifa utakaompa nguvu ya kushughulika na presha ya mchezo wa Simba na Yanga.
Ni kweli kwamba mpambano wa Simba na Yanga una siasa zake lakini Agyei anaweza kucheza vizuri zaidi ya Manyika na faida kubwa atakayoileta kipa huyo ni kwamba, anaweza kuzungumza vizuri na mabeki wake.
Kwa upande wa mabeki, kama mimi ndiye Omog nisingefanya mabadiliko yoyote kwani hao waliopo wameshaanza kuzoeana vizuri na katika eneo la kiungo wa kati wala nisingethubutu kumwanzisha James Kotei na badala yake Jonas Mkude na Mzamiru Yassin wangekuwa na nafasi kubwa na baadaye nitamtumia Said Ndemla kama silaha mbadala iwapo nitaihitaji.
Unadhani ni kipi ambacho kinanishawishi nifanye hivyo? Ni hiki, kiungo cha Yanga kinabebwa na watu wawili, Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima.
Viungo wajanja, waliozoeana hivyo wanatakiwa kukutana na wajanja wenzao vinginevyo mambo yanaweza kuharibika kwani ukimpa nafasi mtu kama Niyonzima bila shaka akina Donald Ngoma watakuwa na kazi rahisi ya kufunga kutokana na pasi zake maridhawa na uwezo wa kupangua ngome za ulinzi.
Kuhusu mawinga, nafasi ya Shiza Kichuya itakuwepo kwenye mchezo huo na ningemwongeza Jamal Mnyate ambaye katika michuano hii amekuwa akitokea benchi na anapoingia unaona wazi kasi ikiongezeka na kuwafanya mabeki wa timu pinzani kuwa na presha kubwa.
Washambuliaji wa mwisho hakuna shaka ningewaanzisha Juma Luizio na mwenzake Laudit Mavugo ambaye kwa sasa anaonekana kuanza kurudi kwenye kiwango chake tofauti na awali na hii inaweza ikawapa presha kubwa akina Kelvin Yondani.
Lingine kubwa ambalo ningewashauri wachezaji wangu, kwanza kabisa ni kutoingiwa na presha yoyote na pia kuendelea na soka la kwenye kitabu, pasi fupifupi na za uhakika huku nikiendelea kutumia mfumo wa 4-4-2 ambao unaonekana kuwakubali zaidi Simba.

Habari MotoMotoZ