RIPOTI SPESHO

KARIBU KARIAKOO, EMMANUEL MARTIN

Na Ally Kamwe

YANGA-MARTINSKaribu Kariakoo, Emmanuel Martin.

Karibu Dar es salaam kwa Mheshimiwa Paul Makonda, karibu sana katika jiji la maajabu.

Ni ardhi hii aliyozikwa Steven Kanumba na filamu zake, ni sehemu hii hii anapoteketea Chid Benz na umwamba wake, nini zaidi unahitaji kujuzwa kuhusu Dar es salaam?

Kila mtu ana sura yake na moyo wake hapa, usidanganyike na vicheko vyao. Wabaya na wazuri wanaishi hapa!

Unataka starehe? Zipo hapa, mpaka zile zisizompendeza shetani. Hii ndio Dar es salaam tamu iliyomkimbiza Mr Nice na kumfedhehesha 20 Percent akiwa na utamu wake.

Hili ndilo jiji pekee duniani wanakopatikana watu aina ya Shilole, Snura, Amber Lulu na Giggy Money kwa wakati mmoja.

Wako wazuri hapa wa kila rangi na utakutana nao kama alivyokutana nao mahotelini Andrey Coutinho kipindi kile, uamuzi ni wako kijana mwenzangu.

Karibu sana Emmanuel.

Kama umekuja na akili zako kama alivyokuja nazo Farid Mussa kipindi kile, bila shaka una pepo yako ndogo ya kuishi pale Kariakoo.

Ila kama umekuja na mabegi tu kama alivyokuja nayo Malimi Busungu, jiandae kuishangaa Kariakoo kama anavyoishangaa Mahadhi Juma hivi sasa, jiji limekosa adabu hili.

Nilivyokutazama na niliyoyasikia baada ya ule mchezo wa Yanga dhidi ya Ndanda, hakika nafsi yangu ilijiridhisha kuwa ‘Dar es salaam imepata mtu wao’

Lile jiji la maajabu sasa limepata mtu wake wa maajabu!

Wakati huu huruma yangu iko Deus Kaseke, najua yuko kwenye vita kubwa na nafsi yake.

Uwezo wa Emmanuel unatishia moja kwa moja nafasi yake katika kikosi cha kwanza.

Kaseke anatakiwa kupambana sana kama ambavyo Geofrey Mwashiuya anavyotakiwa kuamka usingizini, asipokubali kuamka kwa hiari yake, ule mguu wa kushoto wa Emmanuel utamlaza milele.

Bahati nzuri Emmanuel amekuja Yanga na amekutana na George Lwandamina.

Kocha anayemaini uwezo kabla ya jina, kocha anayetengeneza mfumo utakaofatwa na wachezaji na si kuwa na mfumo utakaofata wachezaji.

Sikushangaa na sitashangaa kama Said Makapu ataendelea kumburuza benchi Justice Zulu ‘Mkata umeme’, sitashangaa hata kidogo.

Macho yakishamdanganya Lwandamina, hana muda tena wa kuliamini sikio.

Emmanuel hakwenda Yanga kwa nguvu ya viongozi kama wanavyokwenda wengine, hayuko pale kwa bahati mbaya, uwezo wake ulionekana na kocha ndiye aliyependekeza asajiliwe.

Mara ngapi unaona hili likitokea kwenye usajili wa Bongo uliotawaliwa na tabia za watu wa ‘bongo movie’?

Emmanuel ana muda mwingi sana wa kucheza Yanga, ana muda mwingi wa kukuza kiwango chake na kuzihamisha ndoto zake kuwa kweli.

Yanga ni mahala sahihi sana kwake kwa wakati huu, kwanini? Sababu ni mbili tu. Moja, Atacheza mechi nyingi kubwa, hivyo atapata uzoefu na mbili, yuko kwenye barabara ya kwenda Ughaibuni.

Ndio, michuano ya Ligi ya mabingwa ni ndoto za wachezaji wengi wa Kiafrika, Yanga wataanza kucheza Februari mwaka huu, ni fursa kwa Emmanuel kuonyesha thamani yake kwa faida ya klabu na maendeleo yake binafsi.

Akili yake inatakiwa kutulia mara mbili zaidi anavyotulia akiwa na mpira mguuni, ni wakati wake wa kufungua macho na kuchagua njia anayotaka kupita.

Anataka sifa na makelele ya Kariakoo? Kipo kiti cha Mrisho Ngassa ambacho hakijapata mtu wa kukikalia mpaka leo hii, ziko laki na viroba vya mchele vinamsubiri kama akiamua kuwa ‘mfalme wa Kariakoo’.

Ila kama nafsi yake ina wivu wa kufika alipofika Mbwana Samatta au anapokwenda Farid Mussa, nafasi na wakati ni huu.

Magazeti hayataacha kuandika habari zake, akifanya vyema yatasifia, akiboronga atashughulikiwa vilevile, asiyaweke sana akilini japo ni changamoto anayotakiwa kuizoea kuanzia sasa.

Binafsi nimeona nuru kubwa ikiangaza ndani yake, nimemuona mchezaji mkubwa wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu baadae kama nilivyowahi kumtazama Shiza Kichuya.

Wao ndio mashujaa wa maisha yao na wataamua kilicho sahihi kwao. Kitu pekee anachotakiwa kukumbuka kwa sasa, yuko Kariakoo iliyo ndani ya jiji la Dar es salaam, mengi yasiowezekana kwingine, hufanyika kirahisi sana hapa.

Habari MotoMotoZ