RIPOTI SPESHO

TOKA TFF: LIGI VIJANA UZINDUZI BUKOBA NOV 15, STARS YARUKA KWENDA HARARE

LIGI YA VIJANA U20, UZINDUZI BUKOBA NOV. 15

TFF-HQ-1-1-1Ligi ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 za klabu zote za Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuanza Novemba 15, 2016 kwa mchezo maalumu wa ufunguzi utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu kuwa zina taarifa kuhusu kuwako kwa ligi hiyo ya U20 na kwamba mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni Novemba 3, mwaka huu katika barua maalumu kwa kila klabu yenye Kumb. Na. TPLB/CEO/2016/036.

Tayari klabu hizo zimepewa shilingi milioni 10 (Sh 10,000,000) kutokana na udhamini wa Benki ya DTB kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo. Pia  kila klabu itapewa shilingi milioni 10 (Sh 10,000,000) nyingine kutokana na udhamini wa matangazo ya ligi ya U20 wa Azam Tv.

Kwa udhamini huo kila klabu itajigharimia usafiri wa kwenda na kurudi kituoni, malazi, na chakula kwa kipindi chote cha mashindano. Vituo vilivyopangwa ni Dar es Salaan ambako kuna timu za JKT Ruvu, Simba, Ruvu Shooting, Ndanda, Majimaji ya Songea, Mtibwa, Mbeya City na Tanzania Prisons.

Kituo kingine ni Bukoba mkoani Kagera ambako kuna timu za Azam, African Lyon, Mbao FC, Toto Africans, Mwadui ya Shinyanga kama ilivyo Stand United, Kagera Sugar na Young Africans ambazo zitafungua dimba hiyo Novemba 15 kwa mchezo pekee.

Tunazikumbusha klabu kuzingatia Kanuni ya 42 (27) ya Ligi Kuu ya Vodacom inayosema: “Klabu ambayo haikupeleka uwanjani timu ya U20, mechi ya kwanza itapigwa faini ya Sh 2,000,000 na kunyang’anywa na kupoteza mchezo, mechi ya pili itapigwa faini ya Sh 2,000,000 na kunyang’anywa pointi tatu katika Ligi ya Wakubwa (Ligi Kuu) na Ligi ya Wadogo (u20).

Pia tunazikumbusha klabu kuwa kwa mujibu wa Kanuni, wachezaji saba (7) kutoka U17 wanaruhusiwa kuchezea timu ya U20. Ruhusa hiyo ni kwa wachezaji wa U17 waliosajiliwa, kwa maana kuwa katika ligi zote wachezaji  wanatambuliwa kwa kutumia leseni.

TAIFA STARS YAONDOKA MCHANA HUU NOVEMBA 11, 2016

+++Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro kutoka Kampuni ya Bia Tanzania inatarajiwa kuondoka leo Ijumaa saa 7.15 mchana Novemba 11, mwaka huu kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili ya kucheza na wenyeji kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Novemba 13, mwaka huu.

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika jijini Harare, umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. Kikosi cha Taifa Stars chini ya Kocha Charles Boniface Mkwasa ni: Makipa  Deogratius Munishi na Aishi Manula,Mabeki ni Erasto Nyoni Michael Aidan, Mwinyi Haji, Mohamed Hussein na Vicent Andrew.

Viungo wa Kati ni Himid Mao, Mohammed Ibrahim, Jonas Mkude na Muzamiru Yassin na wale wa pembeni ni ni Shiza Kichuya, Simon Msuva na Jamal Mnyate na washambuluaji ni Ibrahim Ajib, John Bocco, Mbwana Samatta, Elius Maguli, Thomas Ulimwengu na Omar Mponda     .

Mchezo huu utakuwa na faida zaidi kwa Tanzania kama ikiwafunga Wazimbabwe kwa kuwa itaongeza alama za nyongeza kwa kushinda ugenini.

Matokeo ya mchezo huo, ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 144 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Zimbambwe yenyewe inashika nafasi ya 110.

Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Chile, Colombia na Ujerumani.

Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 31 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Senegal (32), Algeria (35), Tunisia (38) na Ghana (45).

RAIS MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA HAFIDHI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Dimani Fumba, Zanzibar, Mheshimiwa Hafidh Tahir Ali aliyefariki dunia kwenye Hospitali Kuu ya Dodoma usiku wa kuamkia leo Novemba 11, 2016.

TFF ilijulishwa kifo cha Mheshimiwa Hafidh na Mbunge wa Jimbo jipya la Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, John Kadutu ambaye alisema leo walikuwa na programu ya kusafiri kwenda Tabora kushiriki mazishi ya Mbunge wa zamani wa Urambo, Samwel Sitta lakini kabla ya kwenda mazoezi alfajiri, waliarifiwa kuhusu kifo hicho. “Inasikitisha, lakini ni ya Mungu yote,” alisema Kadutu.

Kifo hicho kimemsikitisha Rais Malinzi ambaye alituma salamu za pole na rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akisema taifa limepata msiba mwingine mzito kwa Mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa mpira wa miguu aliyekuwa anatambuliwa/kuwa na beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Hakika alikuwa kiongozi wa karibu na watu hasa kutokana na michezo ambayo siku zote alikuwa akiota ndoto za kuifikisha mbali hasa ukirejea kuwa ni jana tu Novemba 10, mwaka huu alichaguliwa na wanachama wenzake wa Young Africans  - tawi la Bunge kuwa Katibu wa tawi hilo chini ya Mwenyekiti Venance Mwamoto – Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa.

Ukaribu huo na watu ndio uliompaisha wakati fulani kuwa mmoja watangazaji mahiri wa redio alipoganya kazi hiyo na manguli wengine kama David Wakati kabla ya kuwa Msemaji wa Serikali ya Awamu ya Tano ya SMZ kabla ya kuwa Mbunge wa RahaLeo.

“Wiki hii imekuwa ngumu kwangu, tumepoteza viongozi wa mfano na wanamichezo mahiri katika kucheza michezo hususani mpira wa miguu na kuuongoza hata kama ni kwa mawazo yao chanya tu. Mheshimiwa Hafidhi ni sehemu ya wanamichezo hao mahiri, ni pigo kubwa hasa kwenye tasnia ya mpira wa miguu. Dua zetu ni Mwenyezi Mungu amghufie na kumrehemu marehemu,” alisema Malinzi.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Malinzi pia alitoa pole kwa familia ya marehemu Hafidh Tahir Ali, ndugu, jamaa, majirani, na marafiki hususani wapiga kura wa Jimbo la Dimani Fumba kwa kumpoteza kiongozi wao hivyo kuwataka kuwa watulivu wakati huu mugumu kwao.

Pia Rais Malinzi amesema vifo cha Sheikh Said Mlohammed, Mzee Mheshimiwa Sitta na Mheshimiwa Tahir, vibaki kuwa sehemu ya funzo kwetu katika kujiandaa na maisha ya baadaye kwa sababu zote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.   

Inna lillah wainn ilayh  Rajiuun.

TWIGA STARS KUJIULIZA TENA KWA CAMEROON JUMAPILI

Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Wanawake ‘Twiga Stars’ jana Novemba 10, 2016 ilipoteza kwa taabu mchezo wake wa kwanza wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya wenyeji Cameroon ambayo ilipata mtihani mzito kwa Watanzania kwa dakika zote kabla ya kuibuka kwa ushindi wa mabao 2-0.

Cameroon ambayo ilijipanga kushinda mabao mengi, ilitolewa jasho na hivyo kuomba mchezo mwingine ambao sasa utafanyika Jumapili Novemba 13, mwaka huu jijini Yaounde na Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Sebastian Nkoma amesema: “Nimeona upungufu katika mchezo wa jana, nafanyia kazi.”

Bao la kwanza katika mchezo wa jana lilifungwa na Mshambuliaji Ngoya Ajara wa Klabu ya Sundsvalls ya Sweden ambaye pia ndiye Mchezaji Bora wa mwaka 2016 nchini Cameroon wakati bao la pili lilifungwa na Kiungo wa Klabu ya Aurillac ya Ufaransa Ngono Mani Michelle katika dakika ya 71.

Twiga Stars wao wamealikwa na Waandaaji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake 2016 – Cameroon ambao wameamua kuipa heshima Tanzania na kuona kuwa timu hiyo ina ubora wa na kwamba inafaa kuipimana ubavu kabla ya kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.

Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Queens ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika Mashariki na kati lakini zaidi ni mabingwa wapya wa ukanda huo – ubingwa uliopatikana Septemba, mwaka huu huko Uganda.

Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon (FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa wiki hii. Tayari Twiga Stars imeanza maandalizi ya kutosha chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi wake Edna Lema na El Uterry Mohrery.

Kikosi cha Twiga Stars wamo makipa, Fatma Omari na Najiat Abbas; mabeki ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna Hamisi, Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa ilhali washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi Omari.

Wakati huo huo, taarifa kutoka zinasema timu ya taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imefungwa bao 1-0 na Seongnam katika mchezo wa kwanza wa kuwania Kombe la Korea Kusini katika michuano iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Korea Kusini. Mchezo huo ulifanyika jijini Seoul, Korea Kusini na goli moja lililofungwa kipindi cha kwanza, vijana wetu wameonesha uwezo mkubwa sana.

Kikosi kilicho anza ni Ramadhani Kabwili (1), Kibwana Ally (12), Nickson Kibabage (3), Ally Msengi (14), Dickson Job (5), Ally Ng'azi (2), Shaban Zubeir (13), Asad Juma (10), Mohamed Rshid (11), Nashon Kelvin (7), na Muhsin Makame (19). Kipindi cha pili benchi la Ufundi lilifanya mabadiliko aliingia Cyprian Mtesi (8) Kuchukua nafasi ya Muhsin Mkame (2) na Errick Nkosi (4) kuchukua nafasi ya Ally Ng'anzi (2).

IMETOLEWA NA TFF