WENGER ‘AMRUDIA’ LACAZETTE, MAN UNITED YAAMBIWA ‘WEKA £50M MCHUKUE DIER!

UHAMISHO ULIOBAMBA ENGLAND:

WENGER ‘AMRUDIA’

Arsenal wamerudi tena kumwinda Straika wa Lyon Alexandre Lacazette ambae sasa anatingwa na kukosa kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI kama akitua Emirates.

Arsene Wenger yupo tayari kupandisha dau kwa Lacazette Mchezaji ambae alitaka pia kumnunua mwanzoni mwa Msimu uliopita.

LACAZETTE-DIERKwa Lacazette, mipango ilikuwa tayari ajiunge na Atletico Madrid na kutocheza Miezi 6 kwa vile Atletico wako kwenye Kifungo cha FIFA cha kutosaini Mchezaji Mpya hadi Januari 2018.

Lakini hilo lilitegemea kwa Atletico kumuuza Antoine Griezmann kwa Man United kitu ambacho pia kimekwamishwa kwa hiyo Adhabu ya FIFA baada ya Rufaa yao kutupwa.

Msimu uliopita Wenger alijaribu kumsaini Lacazette lakini Ofa yao ya Pauni Milioni 30 ikakataliwa na sasa Ada ya kumnunua ni Pauni milioni 50.

Hata hivyo, licha ya Lyon kuwa tayari kumuuza, inadaiwa kikwazo kingine hivi sasa ni Mchezaji huyo mwenyewe kusita kwenda kuchezea Klabu ambayo haimo UEFA CHAMPIONZ LIGI Msimu ujao.

Kwa kumaliza Nafasi ya 5 kwenye EPL, LIGI KUU ENGLAND, Arsenal italazimika kucheza UEFA EUROPA LIGI.

Hata hivyo, Arsenal wanadaiwa pia kukubali kuwapa Lyon Straika wao Olivier Giroud ili wampate Lacazette.

Katika Misimu Mitatu iliyopita, Lacazette alipiga Bao 91.

MAN UNITED YAAMBIWA ‘WEKA £50M MCHUKUE DIER!

Manchester United wamepewa Dau la Pauni Milioni 50 ikiwa watataka kumnunua Kiungo wa Tottenham Hotspur Eric Dier.

Inadaiwa Dier yumo kwenye Listi ya Meneja Jose Mourinho ambayo amemkabidhi Makamu Mwenyekiti wa Man United Ed Woodward ya Wachezaji anaotaka waletwe Old Trafford kwa ajili ya Msimu unaokuja.

Tayari Mourinho na Woodward washamnasa Mchezaji Mmoja katika Listi hiyo baada ya Juzi kumnunua Beki Victor Lindelof kutoka Benfica ya Ureno.

Mourinho anamwona Dier, mwenye Miaka 23, kama ndie mrithi anaestahiki wa Michael Carrick ambae nae alinunuliwa kutoka Spurs Miaka 11 iliyopita na ambae hivi sasa ameongezewa Mkataba wa Mwaka mmoja hadi Juni 2018.

Dier ashaonywa na Meneja wa Spurs Mauricio Pochettino kwamba ni Spurs iliyomkuza hadi akafikia hapo na kuweza pia kuichezea Timu ya Taifa ya England.

Lakini tatizo kubwa kwa Dier na kumfanya avutiwe kwenda Man United ni Mshahara.

Mwezi Septemba Mwaka Jana, Dier alipewa Mkataba Mpya na Spurs na Mshahara wake kuwa Pauni 70,000 kwa Wiki lakini akitua tu Man United Kiungo huyo atazoa Mshahara usiopungua Pauni 150,000 kwa Wiki.

Lakini tatizo kubwa kwa Man United kufanya biashara na Spurs ni ‘ulalamishi’ wa Mwenyekiti wao Daniel Levy katika kukamilisha Dili.

Tangu wamnunue Dimitar Berbatov kutoka Spurs Mwaka 2008, Man United hawajarudi tena kumtaka Mchezaji mwingine licha ya kupenda sana kuwanunua Luka Modric na Gareth Bale walipokuwepo Spurs.

Habari MotoMotoZ