FIORENTINA KUMBURUZA WINGA WA CHELSEA KWA PILATO!

FIORENTINA-LOGOKlabu ya Italy Fiorentina inatafakari kumchukulia hatua za kisheria Winga wa Chelsea Mohamed Salah ambae amegoma kurudi kwenye Klabu hiyo kwa ajili ya Kipindi cha pili cha Mkopo wake.
Salah, Mchezaji kutoka Egypt mwenye Miaka 23, alihamia kwa Mkopo Fiorentina Januari Mwaka huu huku akitoboa wakati huo kuwa Mkopo huo unaweza kurefushwa na kuongezwa Msimu wa pili.
Lakini Fiorentina sasa imedai Salah anataka kujiunga na Klabu nyingine baada ya kuukataa Mkataba mpya ulioboreshwa na pia kugomea kurudi mazoezini kwa ajili ya Msimu mpya.
Fiorentina imesema suala hilo sasa liko kwa Wanasheria wao.
Akiwa na Fiorentina kwa Mkopo, Salah alicheza Mechi 26 na kufunga Bao 9 na alijiunga na Chelsea Mwaka uliopita kutoka FC Basel ya Uswisi kwa Dau la Pauni Milioni 11 lakini alicheza Mechi 19 tu na kuanza Mechi 6 za Ligi Kuu England ndipo akatolewa kwa Mkopo.
Uhamisho wa Mkopo wa Salah kwenda Fiorentina Mwezi Januari ulihusisha Uhamisho wa kudumu wa Winga kutoka Colombia Juan Cuadrado kwenda Chelsea kwa Dau la Pauni Milioni 23.3.
Wakitoa Taarifa kwa Wanahabari, Fiorentina walieleza: "Makubaliano ya Mkopo yanaisha Tarehe 30 Juni 2015 lakini kipo Kipengele cha kuongezwa hadi mwisho wa Msimu 2015/16 na pia kuufanya Uhamisho uwe wa kudumu. "
 

NI RASMI 'EL APACHE' ARUDI KWAO BOCA JUNIORS, TEVEZ AIHAMA JUVE!

Tevez-Fuerte-Apache-Juventus-PP-1024x576Straika wa Argentina Carlos Tevez amekamilisha Uhamisho wake kwenda Boca Juniors kutoka kwa Mabingwa wa Italy Juventus.
Tevez, mwenye Miaka 31, alianzia Soka lake huko kwao na Klabu ya Boca ambayo aliihama Mwaka 2004 kwenda Brazil kuchezea Corinthians na kisha kukaa Miaka 9 akichezea Klabu za Ulaya.
Huko Ulaya alizichezea Klabu za England, West Ham, Mwaka 2006-2007, Manchester United, 2007-2009, na Manchester City, 2009-2013, na kisha kwenda Italy kuichezea Juventus ambako msimu uliopita aliisaidia tena kutetea Taji lao la Ubingwa kwa kupiga Bao 20.
Majuzi Juventus walimbadili Tevez kwa kumsaini Straika wa Atletico Madrid ya Spain, Mario Mandzukic ambae anatoka Croatia.
Alfajiri hii, Tevez alitoa mchango mkubwa kwa Nchi yake Argentina pale alipofunga Penati ya mwisho katika Mechi ya Robo Fainali ya Copa America na kuifikisha Argentina Nusu Fainali baada ya kuibwaga Colombia kwa Penati 5-4 baada ya Sare ya 0-0 katika Dakika 90.
Akithibitisha Uhamisho huu, Rais wa Boca Juniors Daniel Angelici alisema: "Ni Siku ya furaha sana na ya kuridhisha. Kurudi kwa Tevez akiwa kwenye kilele cha mafanikio ni habari njema kwa Washirika na Mashabiki wote wa Boca na Soka la Argentina!"
Tevez, ambae alitwaa Ubingwa mara 3 huko England na mara 2 huko Italy, alifunga Bao 38 katika Mechi 110 alizochezea Boca alipokuwepo huko mara ya kwanza ambako pia alitwaa Ubingwa Mwaka 2003 na kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Marekani ya Kusini kwa mara 3 mfululizo.
Tevez alizaliwa akijulikana kama Carlos Alberto Martínez huko Ciudadela Jimbo la Buenos Aires lakini Wazazi wake wakabadili Jina lake na kumpa ubini wa Mama yake kutokana na mfarakano kati ya Klabu yake ya Utotoni All Boys na Boca Juniors.
Tevez alikulia huko Jimbo la Buenos Aires kwenye Kitongoji cha Ejército de Los Andes, maarufu kama "Fuerte Apache". 
Na ndio maana Carlos Tevez hujulikana sana huku kwao kama "El Apache".
 

KLABU MAARUFU ITALY MUFLISI, YADONDOKA TOKA SERIE A HADI D!

4096Klabu maarufu huko Italy, Parma, ambayo Msimu huu ilishuka Daraja toka Serie A na kwenda Serie B baada ya kushika mkia sasa itabidi ianze Serie D baada ya Leo kutangazwa rasmi kuwa ni muflisi.
Klabu hiyo ilikuwa kwenye harakati kubwa za kumsaka mnunuzi ili aweze kulipa zigo la madeni yao lakini Leo wamesalimu amri na kutangaza wameshindwa kumpata huyo mnunuzi na hivyo ni rasmi wamefilisika.
Habari hizi za kufilisika kwa Parma zilitangazwa rasmi na Wasimamizi wa Klabu hiyo waliokuwa wakiiendesha baada ya kudhihirika ni muflisi, Dr Angelo Anedda na Dr Alberto Guion.
Wasimamizi hao wamesema watakutana na Jaji anaesimamia kufilisika kwa Parma ili mambo yakamilike kisheria.
Parma ilitangazwa imefilisika Mwezi Machi na Mahakama huko Italy lakini wakapewa muda kutafuta mnunuzi ili kuwanusuru na kwa vile hili limeshindikana basi hawatawezi tena kucheza Serie B na badala yake itabidi waanze upya kwenye Serie D ambako Timu za Ridhaa hucheza.
Katika historia yao, Parma hawajawahi kutwaa Ubingwa wa Serie A lakini katika Miaka ya 1990 walibeba UEFA CUP mara 2 na mara 1 kutwaa Kombe la Washindi Ulaya na pia Mwaka 1997 kumaliza Nafasi ya Pili Serie A nyuma ya Juventus.
 

MARADONA AMKARIBISHA CARLOS TEVEZ LA BOMBONERA!

 83746779 tevezLenjendari wa Boca Juniors Diego Maradona amemkaribisha Carlos Tevez Klabuni hapo huku kukiwa na uvumi mkubwa kuwa Straika huyo wa Juventus yuko mbioni kurejea Klabu yake ya zamani maarufu kwa jina la La Bombonera.
Msimu uliopita, Tevez, mwenye Miaka 31 na ambae huitwa Apache huko kwao, alipiga Bao 20 kwenye Ligi Serie A Msimu huu uliokwisha Majuzi na kuisaidia Juventus kutwaa tena Ubingwa wa Italy.
Lakini Staa huyo wa Argentina hivi sasa anahusishwa kuihama Juve na Klabu za Liverpool, Atletico Madrid na Paris St-Germain pia zinatajwa kumlenga ingawa yeye mwenyewe ameshakaririwa mara kadhaa akisisitiza mapenzi yake ya kurudi kule alikoanzia, La Bombonera, ambako alichezea Timu ya Kwanza kuanzia 2001 hadi 2004.
Hivi sasa Tevez yuko Nchini Chile akiwa na Kikosi cha Argentina kinachoshiriki Copa America.
Maradona, ambae aliichezea Boca Juniors na kisha kuwa Makamu wa Rais wake na pia Kocha wa Argentina kati ya 2008 na 2010 huku Tevez akiwemo kwenye Kikosi hicho, ametumia ukurasa wake wa Mtandao wa Facebook kumkaribisha tena Carlos Tevez Klabuni Boca Juniors.
Akiwa na Boca Juniors, Tevez alicheza Mechi 110 na kufunga Bao 38 na pia kutwaa Ubingwa Mwaka 2003 na vile vile kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Marekani ya Kusini kwa Misimu Mitatu mfululizo.
Kabla Msimu wa 2005 kuanza, Tevez akahamia Klabu ya Brazil Corinthians na Mwaka uliofuatia kujiunga na West Ham huko England kisha kwenda Manchester United na Manchester City.
 

MANDZUKIC KUMBADILI TEVEZ JUVE!

TEVEZ-JUVE-SHANGILIACarlos Tevez Siku zote amekuwa akisisitiza kuwa anataka kumalizia Soka lake kule alikoanzia Utotoni kwenye Klabu ya Nchini kwao Argentina Boca Juniors na ndoto hii sasa iko mbioni kukamilika.mariomandzukic-cropped 1ukx2ifdly4bv1ppedo8lvn5st
Meneja Mkuu wa Juventus, Giuseppe Marotta,  ametoboa kuwa wao washamtambua Straika kutoka Croatia, Mario Mandzukic, ndie atakaembadili Tevez hapo Juve.
Nayo Klabu ya Mandzukic, Atletico Madrid, kupitia Kocha wao Diego Simeone, imedokeza kuwa Straika huyo anaweza kuondoka licha ya wao kumtegemea sana.
Marotta, akiongea na Tuttosport, amesema kuwa wao wanaitambua ndoto ya Tevez ya kurudi kwao Argentina na wanaiheshimu.
Pia Meneja Mkuu huyo amesema: "Tunatambua mchango mkubwa wa Tevez kwetu lakini sasa tunangoja majibu na tutajua katika Siku mbili tatu."
Tevez alijiunga na Juve Mwaka 2013 akitokea Manchester City na kuifungia Bao 39 katika Mechi 66.