RONALDO-KESI UKWEPAJI KODI: WAKILI WAKE ADAI 'KESI SI YA HAKI'!!

Antonio Lobo Xavier, mmoja wa Mawakili wa Cristiano Ronaldo, amejibu tuhuma za Waendesha Mashitaka wa Mahakama za Spain wanazodai Staa huyo alikwepa kulipa Kodi yenye thamani ya Euro Milioni 14.7 kati ya Miaka ya 2011 na 2014.
REAL-RONALDO-BAOJana Ronaldo, Mchezaji Bora Duniani anaechezea Klabu ya Spain Real Madrid na Timu ya Taifa ya Portugal, alifunguliwa Kesi rasmi Mahakamani ya Ukwepaji Kulipa Kodi.
Wakili huyo amedai Kesi hiyo si haki na kuwa Mchezaji huyo Mwaka 2014 aliwasilisha Mapato yake yote yatokanayo na Mauzo ya Picha na Matangazo yake kama ipasavyo na kulipa Kodi zote stahiki.
Wakili Xavier amedai: "Hili la Kesi ni kitu cha kushtukiza na Ronaldo anahisi hatendewi haki!"
Aliongeza: "Si kwamba hakuwasilisha Mapato yake yote. Alipeleka kila kitu kwenye Mamlaka ya Kodi lakini inaelekea Wahusika hawakupendelea hilo. Hamna kwenye Sheria popote panaposema alivunja Sheria!"
Pia Wakili Xavier alidai Kesi hii ya Ronaldo na ile ya Lionel Messi ambayo alipigwa Faini na kuhukumiwa Kifungo cha Miezi 21 zina tofauti kwani Ronaldo alifuata ushauri wa kulipa Kodi.
Wakili huyo ameeleza: "Kesi ya Messi na wengine kuhusu Kodi ipo tofauti na ya Ronaldo kwani hao hawakusilisha Mapato yao wakati Ronaldo amepeleka kila kitu!"
Vile vile Lobo Xavier ametoboa kuwa Kesi hii ya Ronaldo imekimbizwa Mahakamani kwa sababu tu ya kukwepa kupoteza haki ya kumshitaki kutokana na muda kihalali wa kufanya hivyo unakaribia kwisha.
Lobo Xavier pia ametoboa kuwa kwa jinsi Ronaldo alivyowasilisha Mapato yake Mwaka 2014 na kulipa kwa Mkupuo Kodi husika upo uwezekano mkubwa alilipa Kodi zaidi kupita kama angelipa Kodi kila Mwaka kwa Miaka kati ya 2011 hadi 2014.
Alipohojiwa kuhusu uchunguzi dhidi yake na Redio ya Nchini kwao Ureno kuhusu tuhuma za Ukwepaji Kodi, Ronaldo alijibu:"Quien no debe no teme", ambayo tafsiri yake inamaanisha "Yule ambae hana cha kuficha, haogopi kitu!"
Kwa mujibu wa Magwiji wa Habari za Fedha, Forbes, Ronaldo ndie Mwanamichezo alievuna Pesa nyingi Duniani kwa Miaka Miwili mfululizo akizoa Dola Milioni 93 kutokana na Mshahara, Bonasi na Matangazo kwa Mwaka Jana

Habari MotoMotoZ