ARSENAL YATAFAKARI KUUZA WACHEZAJI ILI KUWABAKISHA SANCHEZ NA OZIL!

HIVI sasa Arsenal inafanya juhudi kubwa ili Alexis Sanchez na Mesut Ozil wasaini Mikataba Mipya ili waendelee kubaki Emirates lakini kufanikisha hilo ni lazima wauze Wachezaji wengine.

WENGER HENRYHiyo inatokana na Kanuni Mpya za EPL, LIGI KUU ENGLAND, inazotaka Klabu kutozidi Kiwango Maalum kwenye Fungu la Mishahara ya Wachezaji wao.

Kanuni hizo zinataka Klabu isizidishe Fungu la Mishahara zaidi ya Pauni Milioni 7 kutoka lile la Msimu uliopita na si zaidi ya Pauni Milioni 19 toka ule wa Msimu wa 2012/13.

Endapo Klabu itavuja hapo basi Fedha za ziada za Mishahara ni lazima zitoke nje kwenye Mapato yatokanayo na kuuza Wachezaji, Tiketi na shughuli nyingine za Biashara na si toka mgao toka Mafungu yanayotokana na EPL.

Ili kuwabakisha Ozil na Sanchez, Arsenal itapaswa kuboresha Mishahara yao na kuwalipa kiasi cha Pauni 280,000 kwa Wiki.

Gharama hiyo itapandisha Fungu la Mishahara na inakadiriwa Mishahara itagota Pauni Milioni 15 bila kuongeza Mchezaji Mpya yeyote.

Hapo ndipo Arsenal lazima wauze baadhi ya Wachezaji wao.

Miongoni mwa wanaolengwa kuuzwa ili kuwabakisha Ozil na Sanchez ni Alex Oxlade-Chamberlain, Olivier Giroud na Jack Wilshere.

++++++++++++

Arsenal - Uhamisho waliofanya kwa kipindi hiki:

Ndani

Sead Kolasinac (Schalke) Uhamisho wa Bure

+++++++++++++

Wengine ambao Arsenal inaweza kuwaweka Sokoni ni Calum Chambers, Wojciech Szczesny, Chuba Akpom, Kieran Gibbs, Lucas Perez na Carl Jenkinson.

Hata hivyo, Wachunguzi wanadai Arsenal ipo imara Kifedha na inaweza kuwabakisha Ozil na Sanchez na pia kununua Wapya wachache huku wakikidhi Kanuni za EPL za Fungu la Mishahara.

FIFA YAISAFISHA MAN UNITED UHAMISHO WA POGBA, KUISHITAKI JUVE! MOURINHO AKANA UKWEPAJI KODI SPAIN!

JANA Meneja wa Manchester United Jose Mourinho alituhumiwa na Waendesha Mashitaka huko Spain kwa Ukwepaji Kulipa Kodi alipokuwa na Klabu ya Real Madrid kati ya Mwaka 2011 na 2012 na sasa kufunguliwa Mashitaka Mahakamani Kosa ambalo sasa amelikana na wakati huo huo, FIFA sasa wameisafisha Klabu ya Manchester United kutokana na Uchunguzi wa Uhamisho wa Paul Pogba kutoka Juventus.

PATA UNDANI WAKE:

PAUL POGBA: MAN UNITED YASAFISHWA, JUVENTUS KUSHITAKIWA!

MANUNITED POGBA RAIOLAManchester United wamesafishwa na FIFA kwa kutoonekana kutokuwa na Kosa lolote kufuatia Uchunguzi wa Uhamisho wa Paul Pogba kutoka Juventus kwenda Man United Agosti Mwaka Jana.

Lakini FIFA imetamka Juventus itashitakiwa kwa kuvunja Kanuni kutokana na Uhamisho huo.

Mwezi uliopita, FIFA ilizitaka Man United na Juventus kutoa maelezo kuhusu Uhamisho huu ulioweka Rekodi ya Dunia kwa Ada kuwa Pauni Milioni 89.3 na kuripotiwa kuwa Wakala Mino Raiola alivuna Pauni Milioni 41 kutokana na Dili hiyo.

Akiongea na ESPN, Msemaji wa FIFA alisema: “Tunathibitisha Man United haitashitakiwa. Tunathibitisha Mashitaka dhidi ya Juventus yamefunguliwa. Hatuna la ziada la kusema.”

Wakati FIFA ikizitaka Klabu hizo mbili kutoa Maelezo, Man United iliwajibu hawana la ziada kwani kila kitu kimo wazi kwenye Mtandao wa FIFA wa Uhamisho wa Wachezaji Kimataifa kupitia Mfumo wao wa International Transfer Matching System (ITMS) ambao huhitaji taarifa zaidi ya 20 zikiwemo aina ya Uhamisho, Mawakala wanaohusika, Ulipwaji wa Ada zote na namna zitakavyolipwa.

Baada kukidhi yaliyokuwemo kwenye ITMS, FIFA wenyewe wakaikabidhi Man United Cheti cha Uhamisho wa Kimataifa, ITC International Transfer Certificate.

Inaaminika Uchunguzi wa FIFA ulitokana na kuchapishwa kwa Kitabu huko Germany Mwezi uliopita, The Football Leaks: The Dirty Business of Football, ambacho, miongoni mwa mengi kililipua mengi nyuma ya pazia kuhusu Soka, pia kiligusia Ada kubwa mno aliyolipwa Wakala wa Pogba, Mino Raiola, kiasi cha kudaiwa kuvunja Kanuni za FIFA za Uhamisho wa Wachezaji.

Hasa FIFA walitaka kubaini ikiwa Pogba hamilikiwa pekee na Juventus na yupo ‘Mtu wa Tatu’ [Third Party Ownership] kitu ambacho ni marufuku kwa FIFA.

MOURINHO TAX

MOURINHO AKANA MADAI UKWEPAJI KODI AKIWA NA REAL MADRID

MENEJA wa Manchester United José Mourinho amesema yeye hana hatia yoyote na Kosa la Ukwepaji Kulipa Kodi alipokuwa na Real Madrid.

Jana, Mourinho aliburuzwa Mahakamani huko Spain akidaiwa kukwepa kulipa Kodi ya thamani ya Pauni Milioni 2.9 [Euro Milioni 3.3] aliyopaswa kulipa katika Miaka ya 2011 na 2012 alipokuwa Meneja wa Real Madrid.

Mwendesha Mashitaka kwenye Mahakama ya Spain amedai Mourinho hakubainisha Mapato yake yatokanayo na Mauzo ya Umiliki wake wa Picha na Matangazo mengine.

Mashitaka ya Mourinho, mwenye miaka 54, ni Mawili ya kukwepa Kodi ya Euro Milioni 1.6 Mwaka 2011 na Euro Milioni 1.7 Mwaka 2012.

Taarifa iliyotolewa na Kampuni ya Wakala wa Mourinho, Gestifute, ambayo ni ya Wakala Jorge Mendes, imedai Mourinho alipewa Cheti cha kutimiza matakwa yote ya ulipaji Kodi katika kipindi hicho anachotuhumiwa na wanashangazwa na Mashitaka haya ambayo yameibuka ghafla bila wao kupewa taarifa.

Pamoja na Taarifa ya Gestifute, pia walitoa Nakala za Vyeti vya Mamlaka ya Kodi ya Spain vikithibitisha Mourinho ametimiza wajibu wake wa kulipa Kodi.

Huko Spain, kwa Miaka ya hivi karibuni kumeibuka wimbi la Mastaa wa Soka kusakamwa kwa madai ya Kukwepa Ulipaji Kodi.

Mastaa wengine wa Soka walioandamwa na Kesi za aina hii ni pamoja na Cristiano Ronaldo ambae Wiki iliyopita alifunguliwa rasmi Mashitaka kiasi cha kumuudhi na sasa ametishia kuihama Spain na kuacha kuichezea Real Madrid.

Wengine waliowahi kushitakiwa na kuhukumiwa ni Fowadi wa Barcelona, Lionel Messi, ambae alipigwa Faini na kuamriwa ende Jela Miezi 21 ingawa Kifungo hiki kinaaminika kitakuwa cha nje, na Javier Mascherano wa Barcelona aliefungwa Kifungo cha nje cha Mwaka Mmoja.

 

 

STAA CHELSEA ATAKA KUJUMUIKA TENA NA MOURINHO!

CHELSEA MATICZIPO ripoti nzito kuwa Staa wa Chelsea Nemanja Matic anataka kujumuika tana na Jose Mourinho huko Manchester United.

Mourinho ndie aliempeleka Matic huko Stamford Bridge alipomnunua Januari 2014 kutoka Benfica wakati yeye akiwa Meneja wa Chelsea ingawa Matic alitua kwa mara ya kwanza Chelsea Mwaka 2009 akitokea Klabu ya Serbia Kosice.

Matic alikaa Chelsea hadi 2011, akicheza Mechi 2 tu, na kisha kupelekwa kwa Mkopo huko Vitesse Arnhem, kati ya 2010 hadi 2011, na kisha kuuzwa kwa Benfica ya Ureno Mwaka 2011.

Licha kuisaidia Chelsea kutwaa Ubingwa Msimu uliopita, Kiungo huyo kutoka Serbia mwenye Miaka 28 anahisi kuwa Meneja Antonio Conte anataka kummwaga hasa baada ya kuibuka habari kuwa Chelsea inamsaka Kiungo wa AS Monaco Tiemoue Bakayoko ambae ni Mchezaji wa Kimataifa wa France.

+++++++++++++

Manchester United – Uhamisho wa Wachezaji katika kipindi hiki:

Ndani

Victor Lindelof (Benfica) Ada Haikutajwa

Nje

Hakuna

+++++++++++++

Nia ya Mourinho kumleta Matic Old Trafford ni kumfungua Paul Pogba awe huru kwenye idara ya Kiungo kwa kwenda mbele zaidi kuleta ubunifu kwenye Mashambulizi huku Matic akibaki Kiungo Mkabaji.

Mourinho pia anamlenga Kiungo Chipukizi wa Tottenham Eric Dier lakini kikwazo kikubwa ni Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy, ambae ni mgumu mno kufanya nae Biashara na tayari ashatundika Dau la Pauni Milioni 50 kumn’goa Dier.

 

RIPOTI – MOHAMED SALAH KUPIMWA LIVERPOOL JUMANNE!

SALAH ROMAZIPO RIPOTI zimeibuka kuwa Winga wa Egypt na Klabu ya Italy AS Roma Mohamed Salah atapimwa Afya yake Klabuni Liverpool hapo Jumanne ili kufanikisha Uhamisho wake.

Kwa Wiki kadhaa sasa, Liverpool na AS Roma zimekuwa zikivutana kuhusu Dau la Uhamisho lakini sasa, kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka Egypt, KingFut, Salah anatarajiwa kuwasili England ili apimwe Afya huko Anfield hapo Jumanne.

KingFut limedai maafikiano sasa yamefikiwa na Liverpool watailipa AS Roma Pauni Milioni 39.4 (€45m) kama Ada ya Uhamisho.

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amevutiwa mno na Salah ambae Msimu uliopita aliifungia AS Roma Bao 19 na kusaidia 15 katika Mechi 41 na kuiwezesha AS Roma ikamate Nafasi ya Pili kwenye Serie A nyuma ya Mabingwa Juventus.

Salah aliwahi kuwa Mchezaji wa Chelsea kati ya 2014 na 2015 na kucheza Mechi 19 tu kisha kupelekwa kwa Mkopo huko Italy kwa Klabu za Fiorentina na AS Roma na Agosti 2016 kuhama moja kwa moja kujiunga na AS Roma.

Staa wa zamani wa Tottenham na Egpyt, Mido, ana wasiwasi kama Mmisri mwenzake huyo atamudu Soka la England lakini amekiri kuwa Staili ya Salah ipo sahihi kwa Liverpool na pia ni ile anayoipenda Klopp.

Salah atakuwa Mchezaji wa Pili kusainiwa na Liverpool katika kipindi hiki baada pia kumsaini Chipukizi wa Chelsea Dominic Solanke alieng’ara kwenye FIFA Kombe la Dunia U-20 na kuiwezesha England kutwaa Ubingwa wa Dunia hivi Juzi.

 

BAYERN WAGUTUKA, SANCHEZ ADAI PAUNI 420,000 KWA WIKI ILI ASAINI!

ARSENAL SANCHEZ HATIMABayern Munich wamestushwa mno na madai ya Alexis Sanchez ya kutaka alipwe Mshahara wa juu kabisa ili asaini kwa Mabingwa hao wa Bundesliga na Maafisa wao wanahisi ni ujanja wake ili achukuliwe na Manchester City.

Inaaminika Bayern Munich na Man City ndizo Timu pekee ambazo zinamwania Straika huyo kutoka Chile ambae yuko na Arsenal na Mkataba wake huko unamalizika Mwakani.

Arsenal wenyewe hawataki Mchezaji huyo auzwe kwa Mpinzani wao yeyote anaecheza EPL, Ligi Kuu England, lakini madai haya ya Sanchez kwa Bayern ni wazi yataifanya Klabu hiyo ya Germany ibwage manyanga kumnunua na kuwaachia City kuwa Wanunuzi pekee.

Imeripotiwa kuwa Sanchez anataka Bayern imlipe Mshahara wa juu mno, £420,000 kwa Wiki, kitu ambacho hakimo kabisa kwenye Mfumo wa Wajerumani hao.

Kizuizi kingine ni Dau wanalotaka Arsenal wakimuuza Sanchez ambalo ni Pauni Milioni 50 ambalo nalo ni kubwa mno kwa Mchezaji aliebakiza Mwaka Mmoja tu kwenye Mkataba wake na hivyo anaweza kuondoka Bure bila kulipwa Senti ikifika Mwakani.

Kwa upande wa Man City, wao wako tayari kumlipa Mshahara wa Pauni 300,000 kwa Wiki endapo Arsenal itaruhusu aende Etihad.

 

 

Habari MotoMotoZ