Bocco: Tutakaa nafasi nzuri raundi ya pili

IMG 0166IKIWA ni siku ya pili tu tokea Azam FC ianze mazoezi, nahodha wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, John Bocco ‘Adebayor’, anaamini ya kuwa kikosi hicho kitakuwa vizuri na kukaa nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua koo na kuchangamsha mwili, pamoja na Benki bora kabisa nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, tayari kimeanza mazoezi tokea jana asubuhi ili kujiweka fiti zaidi kwa ajili ya kuanza mzunguko wa pili wa ligi.
Bocco ameunambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo ya asubuhi kuwa morali waliyokuwa nayo wachezaji pamoja na nguvu za nyota wapya walioongezwa kikosini kwenye usajili huu wa dirisha dogo, utaweza kuwasaidia kufanya vizuri.
“Tunamshukuru Mungu tumeweza kufika na kufanya mazoezi salama kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili, mazoezi tumeanza vizuri, wachezaji wote wanamorali, wamerudi wameonekana hawakwenda nyumbani tu kupumzika bali walikuwa wakifanya baadhi ya mazoezi, kwa hiyo naamini raundi ya pili itakuwa ni nzuri sana kwetu,” alisema.
Nahodha huyo aliongeza kuwa: “Ukizingatia hata katika usajili kuna nguvu tumeweza kuiongeza, kwa hiyo ninaimani wachezaji tutaweza kujituma na Mungu atatusaidia tutaweza kufanya vizuri raundi ya pili.”
Benchi la Ufundi la Azam FC kwa kushirikiana na uongozi wa timu hiyo, katika usajili huu wa dirisha dogo unaoendelea uwemeza kuongeza nguvu mpya kwa kuwasajili washambuliaji nyota wawili kutoka Ghana, Yahaya Mohamed anayetokea Aduana Stars na staa wa Sekondi Hasaacas, Samuel Afful.
Pia imeweza kuwarudisha kundini wachezaji wake wawili waliokuwa kwa mkopo, beki wa kati kinda Abdallah Kheri aliyekuwa Ndanda na winga wa kushoto Enock Atta Agyei (Medeama).
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, wanaojiandaa pia na michuano ya Mapinduzi Cup, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirikisho Afrika (CC), hadi inamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejikusanyia 35 na Yanga ikiwa nazo 33.
IMETOLEWA NA AZAM FC (By Abducado Emmanuel on December 06, 2016)

RIPHAT HAMISI MCHEZAJI BORA VPL NOVEMBA, TFF U-20 YAENDELEA!

RIPHAT HAMISI MCHEZAJI BORA WA VPL MWEZI NOVEMBA, 2016

TFF-HQ-1-1-1Mchezaji Riphat Hamisi wa timu ya Ndanda FC amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom wa mwezi Novemba kwa msimu wa 2016/2017.

Riphat ambaye ni mshambulaji aliwashinda wachezaji Shaban Idd wa Azam FC na Mbaraka Abeid wa Kagera Sugar. 

Katika mechi mbili ambazo timu ya Ndanda FC ilicheza kwa mwezi huo, Riphat aliisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo yote na kukusanya jumla ya pointi 6 zilizoifanya kushika nafasi ya kumi katika msimamo wa Ligi hiyo ambayo iko mapumzikoni kupisha dirisha dogo la usajili.

Pia aliifungia timu yake mabao mawili katika michezo miwili ambayo timu yake ilicheza kwa mwezi huo.

Mwezi huo ulikuwa na raundi mbili zilizochezwa. Kwa kushinda tuzo hiyo, Riphat atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

DURU LA KWANZA LIGI YA TFF U-20 

Ligi ya vijana kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea katika vituo viwili vya Kagera na Dar Es Salaam ambapo duru la kwanza linatarajiwa kumalizika Desemba 05, 2016.

Katika kituo cha Dar es Salaam, Simba ya Dar es Salaam inatarajiwa kucheza kesho Jumapili Novemba 4, 2016 na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo utakaoanza saa 8.00 mchana wakati saa 10.30 kutakuwa na mchezo kati ya Tanzania Prisons ya Mbeya na Ndanda FC ya Mtwara.

Kesho hiyo hiyo, Desemba 4, mwaka huu katika kituo cha Kagera kutakuwa na mchezo kati Stand United ya Shinyanga itakayocheza na  Young Africans saa 8.00 mchana wakati ya Mwadui pia ya Shinyanga itacheza na Mbao saa 10.30 jioni.

Jumatatu Desemba 5, mwaka huu ratiba itakamilika katika kituo hicho cha Kagera kwa Kagera Sugar kucheza na African Lyon ya Dar es Salaam saa 8.00 mchana wakati Azam FC ya Dar es Salaam na Toto Africans ya Mwanza zitamaliza saa 10.30 jioni.

Kwa siku hiyo ya Jumatatu, Kituo cha Dar es Salaam pia kutakuwa na mechi mbili ambako Majimaji ya Songea itacheza na Ruvu Shooting ya Pwani saa 8.00 mchana wakati Mtibwa Sugar ya Morogoro itacheza na Mbeya City ya Mbeya saa 10.30 jioni.

Baada ya kumalizika kila kundi litatoa washindi wawili watakaocheza nusu fainali na baadaye fainali.

Hatua ya nusu fainali itachezwa jijini Dar Es Salaam katika uwanja wa Azam Complex tarehe 09.12.2016 wakati fainali itachezwa tarehe 11.12.2016 katika uwanja huo huo.

IMETOLEWA NA TFF

 

KESI YA HASSAN KESSY, YARUDISHWA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI, UAMUZI WIKI HII!

SHINDANO MAALUM MWEZI DESEMBA 2016

TFF-HQ-1-1-1Zimekuweko taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeandaa shindano maalum mwezi Desemba.

Mwezi Desemba hakuna shindano lolote jipya  litakalaondaliwa na TFF zaidi ya mashindano yake ya kawaida ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL) na Azam Sports Federation Cup  (ASFC).

Michuano mingine inayosimamiwa na TFF ni Ligi Kuu ya Taifa ya Wanawake (TWPL), Ligi Kuu ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 (TFFU20L), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na Ligi ya Mabingwa wa  Mikoa (RCL).

Ikumbukwe tu kwamba kwa sasa, timu za VPL ziko likizo na ni wakati wa Klabu kufanya mchakato wa usajili wa Dirisha Dogo. Duru la pili lenye mizunguko 15 inatarajiwa kuanza Desemba 17, 2016 kama ilivyopangwa hapo awali.

MWANSASU AITA 12 KUIVAA UGANDA DESEMBA 9

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu unaochezwa ufukweni (Beach Soccer), John Mwansasu ameita kikosi cha wachezaji 12 kati ya 13 wanaotarajiwa kuivaa Uganda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Desemba 9, 2016 utakaofanyika Dar es Salaam.

Mwansasu ambaye hivi karibuni kikosi chake kilicheza na Ivory Coast katika michezo miwili ya  kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni bila mafanikio ni makipa  ambao ni  Rajab Galla na Khalifa Mgaya.

Mabeki ni Roland Revocatus, Juma Ibrahim, Kashiru Salum na Mohammed Rajab wakati Viungo ni Mwalimu Akida, Ahmada Ali na Samwel John huku washambuliaji wengine wakiwa ni Kassim Kilungo na Talib Ally pamoja na Ally Rabbi ambaye ni Nahodha na Mshambulaji wa timu hiyo.

Kocha John Mwansasu bado anafuatilia viwango vya wachezaji mbalimbali ili kujaza nafasi moja ya kipa kabla ya Desemba mosi, 2016 baada ya Kipa Juma Kaseja kutoa taarifa kuwa atakuwa na udhuru wakati nyota mwingine, Mohammed Banka aliyeripotiwa kuwa safarini nchini Afrika Kusini.

TAARIFA YA KAMATI YA NIDHAMU YA TFF

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefuta adhabu iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72) kwa viongozi na wachezaji wa Kimondo.

Kamati ya Saa 72, ilifanya tathmini ya mchezo huo Na. 23 kati ya Kurugenzi na Kimondo ambako iliamua kuwafungia viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye, Selestine Mashenzi, na Mussa Minga kwa miezi sita na kupigwa faini ya Sh. 500,000 kila mmoja.

Walidaiwa kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi Mussa Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji ambao waliohusika katika tukio hilo wamefungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja.

Wachezaji waliotajwa ni January Daraja Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Hata hivyo, katika kikao chake Jumapili iliyopita, Kamati ya Nidhamu ya TFF, chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas ilikubaliana na hoja ya wapinga adhabu waliowasilisha malalamiko yao TFF mara baada ya kuadhibiwa na Kamati ya Saa 72.

Hoja za viongozi wa Kimondo ni kuwa hakuwahi kuitwa mbele ya Kamati hiyo kuhusiana na jambo hilo kwa ajili ya kutoa utetezi wake na kuwa na shaka na kamati hiyo juu ya kutoa adhabu hiyo.

Kamati ya Nidhamu ilikubaliana na hoja hizo na hivyo kufuta adhabu hizo na kuagiza kamati ya saa 72 ya Bodi ya Ligi Kuu kuandikia kamati ya Nidhamu kuhusu makosa hayo ili kusikilizwa upya.

TAARIFA YA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilikutana jana Jumapili Novemba 27, 2016 kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Bodi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia mashauri manane.

Shauri la 1. Klabu ya Simba dhidi ya Young Africans na mchezaji Hassan Hamis Ramadhani Kessy

Shauri hili sasa limerudi rasmi kwenye meza ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji. Kamati iliyoketi chini ya Makamu Mwenyekiti, Mwanasheria Raymond Wawa imekubali shauri hilo kurejea kwenye Kamati yake na imeahidi kutoa maamuzi ndani ya wiki hii.

Shauri la 2. Malalamiko ya Ayoub Nyenzi na wenzake

Shauri hili pia limepangwa kusikilizwa mwishoni mwa wiki hii. Uongozi wa Young Africans, umeagizwa kuleta nyaraka/kesi inayodai kuwa viongozi hao waliofukuzwa uanachama na Mkutano Mkuu wa dharura ama walishiriki au walifungua shauri mahakamani.

Uongozi wa Young Africans, chini ya Kaimu Katibu Mkuu Baraka Deusdedit ulikubali kuwasilisha nyaraka hizo kabla ya kikao kijacho kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii. Wenzake na Nyenzi ni Hashim Abdallah na Salum Mkemi.

Shauri la 3. Klabu ya Simba na Kocha Amatre Richard

Kamati ilijikita kwenye hukumu yake na kuitaka Sekretarieti ya TFF kuandikia Simba kuhusu msimamo wa hukumu iliyotolewa kwa Simba kumlipa kocha huyo.

Shauri la 4. Malalamiko ya Young Africans dhidi ya Kagera Sugar

Wahusika kwenye shauri hili, wameamuliwa kwenda Dar es Salaam mbele ya kikao kitakachoitishwa mwishoni mwa wiki ili kujieleza. Wahusika hao ni Young Africans waliowasilisha malalamiko, Panone FC ya Kilimanjaro, Kagera Sugar pamoja na mchezaji husika ili hatua stahiki zichukuliwe mara baada ya kuwasikiliza.

Shauri la 6. Malipo ya wachezaji Jerry Tegete, Omega Seme na Thabit Mohammed

Kamati iliamua utekelezwa ufanyike kwa Klabu ya Young Africans kuwalipa wachezaji hao kama uamuzi ulivyokwisha kutoka hapo awali. TFF iandikie barua Young Africans kuhakikisha inawalipa.

Shauri la 7. Madai ya Mchezaji Said Bahanuzi dhidi ya Young Africans.

Suala la Bahanuzi limesogezwa mbele basi kwa kwa kuwa halikujadiliwa.

Shauri la 8. Mchezaji Said Hussein Morald

Mchezaji huyo kwa sasa ni huru baada ya yeye na Klabu ya Singida Unitedf kufikia mwafaka kwa barua ambazo waliwasilisha mbele ya kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji.

MALINZI AMPONGEZA MTAKA, AAHIDI USHIRIKIANO RT

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Anthony Mtaka kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) - katika uongozi utakaodumu miaka minne ijayo.

Kadhalika, Rais Malinzi amewapongeza wajumbe waliochaguliwa kadhalika Baraza la Michezo la Taifa (BMT), chini ya Mwenyekiti wake, Dioniz Malinzi kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa RT, uliofanyika mjini Morogoro Jumapili.

Katika pongezi zake Malinzi amesema kwamba atashirikiana na viongozi wa RT walioingia madarakani na amewataka kutambua kwamba wamepewa madaraka makubwa kuhakikisha wanaipeleka mbele riadha kama walivyofanya akina Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga, Zakaria Barrie, Gidamis Shahanga, Alfredo Shahanga, Mwinga Mwanjala, Rehema Killo, Zebedayo Bayo, John Yuda, Lwiza John na wengine.

Uongozi mpya upokee changamoto ya kuhakikisha mchezo wa riadha Tanzania unaanzia chini shuleni na unachezwa mikoa yote, tofauati na ilivyo hivi sasa inaonekana kuchezwa eneo fulani tu la Tanzania. Kadhalika wasiruhusu aina yoyote ya chembe ya migogoro.

Rais Malinzi aliwapongeza wagombea wengine waliothubutu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi lakini kwa bahati mbaya kura hazikutosha, lakini akawatia shime viongozi walioshika madaraka na kushirikiana na uongozi mpya.

Mbali ya Mtaka ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, wengine walioingia madarakani ni William Kallaghe ambaye ni Makamu wa Rais eneo la Utawala wakati Makamu wa Rais Ufundi, Dk. Ahmed Ndee huku Katibu Mkuu akiwa ni Wilhelm Gidabuday na Katibu Msaidizi ni Ombeni Zavalla.

Mweka Hazina ni Gabriel Liginyan wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Lwiza John, Meta Petro, Robert Kalyahe, Dk Nassoro Matuzya, Rehema Killo, Zakaria Barie, Mwinga Mwanjala, Tullo Chambo, Christian Matembo na Yohana Misese.

IMETOLEWA NA TFF

MABINGWA YANGA - ZAMA ZAANZA: TIMU ‘MPYA’ MHOLANZI PLUIJM, MZAMBIA LWANDAMINA WATAMBULISHWA RASMI!

YANGA-ZAMA-MPYAMABINGWA wa Soka Tanzania Bara, Yanga, wamewatambulisha rasmi Hans van de Pluijm na George Lwandamina kama Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Mkuu katika Hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Yanga, Mitaa ya Jangwani na Twiga Jijini Dar es Salaam.

Mholanzi Hans van de Pluijm, ambae alikuwa Kocha Mkuu, sasa ‘anapanda ghorofani’ na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Raia wa Zambia George Lwandamina anakuwa Kocha Mkuu.

Lwandamina, ambae alikuwa Kocha wa ZESCO huko kwao Zambia na sasa anamrithi Pluijm, amesema hatabadili Benchi lake la Ufundi na atashirikiana vyema na Pluijm.

Kauli hiyo inamaanisha Wasaidizi wa Lwandamina watabaki kuwa Watu walewale waliokuwa chini ya Pluijm ambao ni Juma Mwambusi, Kocha Msaidizi, Juma Pondamali, Kocha wa Makipa, Hafidh Saleh, Meneja, Daktari Edward Bavu, Jacob Onyango, Mchua Musuli na Mohamed Omar ‘Mpogolo’, kama Msimamiza wa Zana za Kikosi.

Akiongea mara baada ya Hafla hiyo ya Utambulisho, Lwandamina alisema: "Ni changamoto mpya kwangu, naijua Yanga ni Klabu kubwa lakini nitahakikisha natumia kila linalowezekana kuhakikisha tunafanya vizuri katika Ligi na michuano ya Kimataifa.

Lwandamina anategemewa kuanza kazi yake rasmi mara moja kutayarisha Kikosi kwa ajili ya Mzunguko wa Pili VPL ambao utaanza Desemba 17

VPL

Msimamo – Timu za Juu:

1 Simba Mechi 15 Pointi 35

2 Yanga Mechi 15 Pointi 33

3 Azam Mechi 15 Pointi 25

4 Kagera Mechi 15 Pointi 24

5 Mtibwa Mechi 15 Pointi 23

Mzunguko wa Pili

Round 16

17.12.2016(Sat)

121

JKT RUVU

 

Vs

 

YOUNG AFRICANS

MAIN NATIONAL STADIUM

DAR ES SALAAM

17.12.2016(Sat)

122

MBEYA CITY

 

Vs

 

KAGERA SUGAR

SOKOINE

MBEYA

17.12.2016(Sat)

123

NDANDA FC

 

Vs

 

SIMBA SC

NANGWANDA

MTWARA

17.12.2016(Sat)

124

MWADUI FC

 

Vs

 

TOTO AFRICAN

MWADUI COMPLEX

SHINYANGA

17.12.2016(Sat)

125

MBAO FC

 

Vs

 

STAND UNITED

CCM KIRUMBA

MWANZA

17.12.2016(Sat)

126

RUVU SHOOTING

 

Vs

 

MTIBWA SUGAR

MABATINI

COAST REGION

18.12.2016(Sun)

127

AFRICAN LYON

 

Vs

 

AZAM FC

KARUME

DAR ES SALAAM

18.12.2016(Sun)

128

TANZANIA PRISONS

 

Vs

 

MAJIMAJI FC

SOKOINE

MBEYA

ASFC – RAUNDI YA PILI, RAIS MALINZI ALIZWA NA MSIBA MWINGINE YANGA!

RAUNDI YA PILI AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017

TFF-ASFC-CUPWakati Baruti ya Mara ikiifunga Ambassador ya Simiyu mabao 3-1 katika mchezo wa raundi ya pili  ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ndani ya Uwanja wa  Halmashauri Kahama,  michezo mingine inatarajiwa kuendelea Novemba 27, mwaka huu kwenye viwanja mbalimbali kwa mujibu wa ratiba.

Hatua ya pili itakutanisha timu zlizopenya hatua ya kwanza iliyofanyika wikiendi iliyopita. Mechi zinazotarajiwa kucheza hatua inayofuata ni Tomato dhidi ya Jangwani katika mchezo utakaofanyika mkoani Njombe.

Mbuga FC ya Mtwara itacheza na Muheza United huko Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara huku Kabela City ya Kahama itakuwa mwenyeji wa Firestone ya Kiteto mkoani Manyara.

Raundi ya tatu itafanyika Desemba 3, 2016 kwa kukutanisha timu za Mtwivila ambayo itasubiri mshindi kati ya Tomato na Jangwani wakati Stand Bagamoyo itasubiri mshindi kati ya Mbuga na Muheza United ya Tanga huku Stand Misuna inasubiri mshindi wa mchezo kati ya Kabela City na Firestone ya Manyara ilihali Mrusagamba ya Kagera sasa inasubiri kucheza na Baruti ya Mara.

Kufika hapo Tomato iliing’oa Mkali ya Ruvuma kwa ushindi wa penalti 6-5; Jangwani iliifumua Nyundo 2-0; Mtwivila iliilaza Sido kwa mabao 7-4; Mbuga iliifunga Makumbusho mabao 5-4; wakati Muheza ilishinda 2-1 dhidi ya Sifa Politan ya Temeke.

Timu ya Stendi FC ililala kwa Kabela City kwa mabao 5-3; wakati Stand Misuna iliifunga Veyula mabao 2-1 huku Stand ikiilaza Zimamoto mabao 5-4 ilihali Baruti FC ya Mara na Mrusagamba ya Kagera zilipita baada ya wapinzani Gold Sports ya Mwanza na Geita Town kugomea mechi za awali kwa kutojitokeza uwanjani.

RAIS MALINZI ALIZWA NA MSIBA MWINGINE YOUNG AFRICANS

“Nimeshtushwa,” ni neno moja tu la Rais wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF), Jamal Malinzi mara baada ya kupata taarifa za kifo cha Hamad Kiluvia ambaye ni mmoja wa viongozi wa Young Africans Sports Club.

Hamad Kilivua amefariki dunia leo alfajiri Novemba 23, 2016 jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ambayo Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Isaac Shekiondo ‘Clinton’ amezikwa kwao Korogwe mkoani Tanga.

Kilichomshitua Rais Malinzi ni kifo cha Kiluvia akisema kinakwenda sambamba na cha Shekiondo aliyefariki dunia Novemba 20, mwaka huu kwenye Hospitali ya Amana, Ilala  jijini Dar es Salaam.

Leo amepata taarifa za kifo cha Kiluvia ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Young Africans. Enzi za uhai wake, Kiluvia akiwa Mjumbe wa bodi hiyo alishirikiana na Malinzi wakati huo wakiwa viongozi wa juu wa Klabu hiyo ambayo Makuu yake yako kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Kariakoo, Dar es Salaam.

Rais Malinzi amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha Kiluvia kwa kuwa anafahamu vema utendaji wakati huo akiwa Kiongozi wa Young Africans Sports Club. Alikuwa ni mtu mpole, mwenye kusikiliza na kutatua changamoto za klabu aliyependa mpira wa miguu na kutoa misaada na fedha na mawazo kadiri ya uwezo wake.

Kadhalika Rais Malinzi alituma salamu hizo kwa familia ya marehemu Kiluvia ndugu, jamaa na marafiki ambayo kwa muda walikuwa wakimuuguza mpendwa wao na hivyo kutokana na kifo hicho, amewataka kuwa watulivu kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.

Msiba wa Kiluvia uko nyumbani kwake, Mikocheni Regent Estate jirani na Ofisi za Baraza la Mazingira (NEMC) ambako taratibu za mazishi zinafanyika.

IMETOLEWA NA TFF