RUFANI YA DAKTA DAMAS NDUMBARO-ADHABU YABAKI ILE ILE MIAKA 7 'JELA' YA SOKA!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - RELEASE NO. 72

TAREHE 11 MEI 2015

MAAMUZI YA KAMATI YA RUFAA YA NIDHAMU 

UWANJA- TAIFA-DARBaada ya mahojiano kati ya mrufani Dr Damas Ndumbaro na Wakili wa TFF     Nd Emmanuel Muga, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya rufaa ya nidhamu kuwahoji wote, Mrufani na Wakili wa TFF, Kamati ya rufaa ya nidhamu ilichukua uamuzi ufuatao:- 

Hoja ya kwanza cha rufaa, kwamba kamati ya nidhamu haikuwa na nguvu za kisheria kusikiliza shauri lake, Kamati ya rufaa ya nidhamu baada kusikiliza hoja za pande zote mbili, kwa uamuzi wa Wajumbe wote kwa maana ya kuwa zote nne za Wajjumbe wa kamati ya rufaa ya nidhamu, ilitupilia mbali hoja hiyo na kuona kwamba kamati ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa mkata rufaa ni afisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF ya 2013. Uamuzi katika hoja hii uliamuliwa kwa kura 3 dhidi ya moja.Hoja ya pili inayosema kwamba kamati ilikosea kisheria kwa kutompa muda wa kuleta utetezi wake wala vielelezo vyovyote vile kwenye shauri lake.

Kamati ya rufaa ya Nidhamu kwenye Shauri hili, baada ya kufanya maamuzi kwa kupiga kura, kura za Wajumbe watatu zilitupiliwa mbali hoja yake na kura moja kati ya kura nne ilikubaliana na hoja yake kwa uamuzi huo, kamati ya rufani ya nidhamu ilitupilia mbali hoja hiyo kwa uamuzi wa wingi wa kura kwa maana ya kuwa tatu dhidi ya kura moja.

Sababu za kutupilia mbali hoja hizo ni kwamba mrufani alipata wito wa kwenda kwenye shauri, na akawakilishwa na wakili wake ( Nestory Peter Wandiba ) kwenye Shauri hilo. Shauri liliposikilizwa kwa mara ya kwanza tarehe 10/10.2014 shauri lilipangwa kusikilizwa tarehe11/10/2014 Lakini siku hiyo ya pili si wakili wala Dr Ndumbaro alifika kwenye shauri hilo kwa maana hiyo basi shauri lililazimika kusilikizwa upande mmoja kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za TFF ibara ya 94 (3).

3. Hoja ya tatu linalosema kwamba kamati ilikosea kusiliza shauri upande mmoja bila ya mtuhumiwa kuwepo, ni kukiuka haki yake ya msingi ya  kusikilizwa.

Kamati baada ya kusikiliza utetezi kutoka pande zote mbili kamati ilifanya uamuzi kwa kupiga kura, na kura tatu (wajumbe watatu) walitupilia mbali hoja hiyo, dhidi ya kura moja (mjumbe mmoja) aliyeikubali hoja hiyo. Sababu za kutupilia mbali hoja hiyo ni kutokana na ukweli kwamba mrufani alipata wito wa kuhudhuria shauri hili na akamtuma wakili wake, lakini mrufani alishindwa kuonyesha vielelezo vya kuonyesha kwamba angesafiri kwenda nje ya nchi ili kamati ya nidhamu iweze kuahirisha shauri mpaka wakati ambao angekuwa amerejea lakini hakufanya hivyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa Ibara 144(2) (3) za kanuni ya nidhamu za TFF, mrufani  angeweza pia kuomba kamati ya nidhamu ibatilishe uamuzi iliyoutoa dhidi yake ili aweze kusikilizwa utetezi wake pia hakufanya hivyo na aliamua kukata rufaa.

4. Hoja ya nne inayosema kwamba kamati ilikosea kisheria katika uchambuzi wa ushahidi wa mlalamikaji na hatimaye kutoa uamuzi uliomtia hatiani.

Kamati ya rufani ya nidhamu ilisikiliza kwa umakini hoja za pande zote mbili na kujiridhisha kwamba mrufani alifanya makosa kwa kutoa taarifa isiyosahihi na kupotosha maamuzi ya TFF kinyume na kanuni ya 41 (6) ya kanuni za ligi kuu ya Tanzania toleo la 2014 (4) na pia kushawishi, kupotosha au kuzuia maamuzi/utekelezaji wa maamuzi ya TFF kinyume na kanuni ya 41(16) ya kanuni za ligi kuu za Tanzania ya (2014).

Wakati wa kufanya maamuzi, wajumbe watatu(3) kwa maana ya kura tatu zilitupilia mbali hoja hiyo, na kura moja, kwa maana ya mjumbe mmoja alikubaliana na hoja hiyo. Kwa maana hiyo, kamati ya rufaa ya nidhamu ya TFF imetupilia mbali hoja hiyo.

Kwa uamuzi huu kamati inadhibitisha uamuzi wa kamati ya nidhamu iliyosomwa tarehe 13/10/2014, uamuzi huu umefikiwa baada ya wajumbe kupiga kura na uamuzi kupitishwa kwa wingi wa kura za wajumbe watatu, dhidi ya mjumbe mmoja wa kamati hii kwa hoja ya 2,3 na 4 na wajumbe wote 4 walikubaliana kutupiliwa mbali hoja ya kwanza.

Kwa hiyo Dr Damas Ndumbaro ataendelea kutumikia adhabu yake kwa kutojihusisha na shughuli yoyote ya Mpira wa Miguu (Soka) kwa kipindi cha miaka saba.

Hata hivyo mrufani Dr Damas Ndumbaro anayohaki ndani ya siku 10 kuanzia leo tarehe10/05/2015 ya kuomba marejeo ya uamuzi huu mbele ya kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF chini ya Ibara 142 ya kanuni za nidhamu za TFF ya mwaka.

Kila upande utabeba gharama zake Hukumu inasomwa leo tarehe 10/05/2015/

Revocatus L. K. Kuuli.

MAKAMU MWENYEKITI.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

TFF YAKUBALI UENYEJI KAGAME CUP

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - RELEASE NO. 71

TAREHE 10 MEI 2015

TFF YAKUBALI UENYEJI KAGAME CUP

UWANJA- TAIFA-DARShirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, leo hii imekubali kuwa wenyeji wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ngazi ya Vilabu maarufu kama CECAFA Kagame Cup.

CECAFA ambao ndio wamiliki wa mashindano haya watatoa mialiko kwa vilabu vyenye sifa ya kushiriki na wakipokea uthibitisho wa ushiriki wao watatoa orodha ya vilabu shiriki na ratiba ya michuano hiyo.

Michuano hii inatarajiwa kuafanyika nchini kuanzia tarehe 11 Julai mpaka 02 Agosti 2015.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

LIGI KUU VODACOM: RUVU SHOOTING YASHUKA DARAJA, MABINGWA YANGA WAFUNGWA NANGWANDA!

UWANJA- TAIFA-DARRuvu Shooting imeungana na Polisi Moro kushushwa Daraja baada ya Leo hii kuchapwa 1-0 huko Shinyanga na Stand United ikiwa ni moja ya Mechi za mwisho za Ligi Kuu Vodacom kwa Msimu huu wa 2014/15.
Timu ya kuungana na Polisi Moro kushushwa Daraja ilikuwa ndio gumzo kubwa ya Mechi hizi za mwisho za Ligi kwani Bingwa na Mshindi wa Pili, ambazo ndizo Timu pekee zitakazocheza Michuano ya Klabu Barani Afrika, zilikuwa zimeshapatikana.
Yanga, kwa kutwaa Ubingwa, itacheza CAF CHAMPIONZ LIGI, na waliopokonywa Ubingwa, Azam FC, kwa kumaliza Nafasi ya Pili, watacheza Mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikisho.
Msimu huu Timu mbili zimeshushwa Daraja na Timu 4 zimepanda ili kufanya idadi ya Timu za Ligi Kuu Vodacom kuwa 16 Msimu ujao badala ya 14 za sasa.
Timu 4 zilizofuzu kupanda Daraja na kucheza Ligi Kuu Vodacom Msimu ujao ni Majimaji ya Songea, Mwadui ya Shinyanga, African Sports ya Tanga na Toto Africans ya Mwanza.
LIGI KUU VODACOM
MATOKEO:
Jumamosi Mei 9
***Mechi za mwisho za Ligi
JKT Ruvu 1 Simba 2
Mtibwa Sugar 1 Coastal Union 1
Stand United 1 Ruvu Shooting 0
Mbeya City 1 Polisi Moro 0
Kagera Sugar 0 Tanzania Prisons 0
Ndanda FC 1 Yanga 0
Azam FC 0 Mgambo JKT 0
MSIMAMO:
**Timu zote zimecheza Mechi 26:
1 Yanga Pointi 55
2 Azam FC 49
3 Simba SC 47
4 Mbeya City 34
5 Mtibwa Sugar 32
6 Kagera Sugar 32
7 Coastal Union 32
8 JKT Ruvu 31
9 Ndanda FC 31
10 Stand United 31
11 Tanzania Prisons 29
12 Mgambo JKT 29
13 Ruvu Shooting 29
14 Polisi Moro 25

LIGI KUU VODACOM-TAMATI: PATASHIKA NANI KUUNGANA NA POLISI KUSHUKA?

UWANJA- TAIFA-DARTayari Ligi Kuu Vodacom inae Bingwa, Yanga, Mshindi wa Pili, Azam FC, na Mshindi wa Tatu, Simba, lakini kazi kubwa ipo Jumamosi kwenye Mechi za mwisho kabisa za Msimu kuamua Timu ipi moja itaungana na Polisi Moro kuteremka Daraja.
Yanga walishatwaa Ubingwa tangu Wiki iliyopita na Msimu ujao watawakilisha kwenye CAF CHAMPIONZ LIGI na Azam FC, ambao wamepoteza Taji lao, wameshika Nafasi ya Pili na hivyo watacheza Mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikisho.
Kwa Msimu huu Timu mbili zitashushwa Daraja na Timu 4 kupandishwa ili kufanya idadi ya Timu za Ligi Kuu Vodacom kuwa 16 Msimu ujao badala ya 14 za sasa.
Timu 4 zilizofuzu kupanda Daraja na kucheza Ligi Kuu Vodacom Msimu ujao ni Majimaji ya Songea, Mwadui ya Shinyanga, African Sports ya Tanga na Toto Africans ya Mwanza.
Timu moja ambayo itaungana na Polisi Moro kuporomoka Daraja kutoka Ligi Kuu Vodacom ni moja kati ya Timu 5 ambazo ni Ruvu Shooting, Prisons, Stand United, Ndanda FC na Mgambo JKT.
LIGI KUU VODACOM
RATIBA
Jumamosi Mei 9
***Mechi za mwisho za Ligi
JKT Ruvu v Simba
Mtibwa Sugar v Coastal Union
Stand United v Ruvu Shooting
Mbeya City v Polisi Moro
Kagera Sugar v Tanzania Prisons
Ndanda FC v Yanga
Azam FC v Mgambo JKT
MSIMAMO:
**Timu zote zimecheza Mechi 25 na kubakiza 1:
1 Yanga Pointi 55
2 Azam FC 48
3 Simba SC 44
4 Mtibwa Sugar 31
5 Mbeya City 31
6 Kagera Sugar 31
7 JKT Ruvu 31
8 Coastal Union 31
9 Ruvu Shooting 29
10 Tanzania Prisons 28
11 Ndanda FC 28
12 Mgambo JKT 28
13 Stand United 28
14 Polisi Moro 25

JERRY MURO FAINI MILIONI 5, TAMBWE AWEKWA KIPORO, MALINZI ATAKA UDHIBITI MECHI ZA MWISHO LIGI!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - RELEASE NO.
TAREHE 08 MEI 2015
RAIS TFF AAGIZA USIMAMIZI MECHI ZA MWISHO VPL
UWANJA- TAIFA-DARRais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewaagiza wasimamizi wa vituo vya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuhakikisha sheria na taratibu zote za mechi zinafuatwa.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu huu 2014/2015 inafikia tamati kesho (Mei 9, 2015) ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani katika mechi ambazo ndizo zitakazotoa hatma ya timu zinazoshuka daraja. 
Mechi hizo zitakuwa kati ya Ndanda na Yanga (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara), JKT Ruvu na Simba (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Azam na Mgambo Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Stand United na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Kagera Sugar na Tanzania Prisons (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mbeya City na Polisi Morogoro (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
JERRY MURO APIGWA FAINI MILIONI 5
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF iliyoketi jumanne tarehe 5 Mei, 2015 imempiga faini ya sh. 5,000,00 (milioni tano), Afisa Habari wa klabu ya Yanga SC Jerry Muro kwa kutoa kauli za chuki, kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na TFF.
Akitoa utetezi wake mbele ya Kamati ya Nidhamu, Jerry Muro alikiri na kujutia kufanya kosa hilo na kudai ilitokana na ugeni wake katika uongozi wa michezo, kwa kuzingatia hilo kamati ilimuepusha na adhabu ya kufungiwa..
Kwa mujibu wa Ibara ya 53 (2)ya Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012, kwa kuidhalilisha TFF na Bodi yake ya Ligi mbele ya umma, kamati imemtoza faini ya sh. 5,000,000 (millioni tano), Jerry Muro na kuwaonya viongozi wengine wa familia ya mpira wa miguu kutojihusisha na vitendo vya matamshi ya aina hiyo.
Shitaka linalomhusisha mchezaji wa Yanga, Amissi Tambwe kumshika kwa kumdhalilisha mchezaji wa Simba SC Juuko Mursheed, na kiongozi wa Friend Rangers Hery Chibakasa wa Friends Rangers kuhamasisha vurugu katika mchezo wa timu yake na dhidi ya Majimaji ya Songea Januari 29, 2015, kamati imeahirisha mashitaka hayo mpaka tarehe nyingine itakapopangwa.
Kamati iliahirisha malalamiko dhidi ya Mohamed Hussein, Muhibu Kanu, Manfred Luambano, Venance Joseph, Mussa Senyange, Saleh Ali, Shafii Maganga na Ismail Salim baada ya kupokea taarifa za udhuru zilizosbabishwa na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria ya mikoani.
KUMRADHI WANAHABARI
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine ameomba radhi kwa vyombo kufuatia madai ya waandishi wa habari kupata usumbufu wakati wa utoaji wa Zawadi kwa Mabingwa na washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Mwesigwa alisema kwa niaba ya TFF anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata waandishi na wadau wote walioshindwa kushuhudia vema tukio hilo.
“TFF na FIFA vinatambua umuhimu na nafasi ya wanahabri na vyombo vya habari si tu katika kuutangaza mchezo, bali pia katika kutia chachu maendeleo ya mchezo wenyewe “ alisema Mwesigwa.
Hali mbaya ya hewa ilivuruga utaratibu uliokuwa umepangwa awali kuanzia itifaki ya shughuli za kabla na wakati wa mchezo na zile za utoaji tuzo.
Aidha Mwesigwa alisema TFF itaendelea kushirikiana vema na jumuiya ya wanahabari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wana mazingira mazuri wanapofanya kazi kwenye matukio ya mpira wa miguu.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)