TFF YAMSHUKURU RAIS DOKTA MAGUFULI, WAZIRI NAPE KWA KURIDHIA TAIFA KUTUMIKA TENA KISOKA!

PRESS RELEASE NO. 243                                             JANUARI 27, 2017

TFF YAMSHUKURU RAIS DK. MAGUFULI

TFF-HQ-1-1Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kufunguliwa tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kadhalika, TFF inamshukuru Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kwa juhudi zake na kwamba namna aliyoonesha ushirikiano kufanikisha suala la kufunguliwa uwanja huo uliofungiwa matumizi yake na Serikali, Oktoba mwaka uliopita.

TFF inachukua nafasi hii kuahidi kuwa itasimamia matumizi mazuri ya uwanja huo kwa kutoa elimu kwa wadau ili kuutumia uwanja huo vema ikitambua kuwa ni hazina ambayo imetokana na nguvu na gharama kubwa za Serikali kuujenga uwanja huo.

TFF inatahadharisha mashabiki wa mpira wa miguu kwamba uwanja huo umejengwa kwa gharama kubwa hivyo ni jukumu letu kuutuza na kuutumia vema kwa sababu ni hazina kubwa tuliyonayo na ni miongoni mwa urithi bora kwa vizazi vijavyo.

Kwa sasa tumetuma maombi yetu Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuomba kuutumia uwanja huo kwenye mchezo wa kesho Jumamosi Januari 28, mwaka huu kati Simba na Azam utapigwa kwenye uwanja huo wa Taifa, Dar es Salaam kadhalika keshokutwa katika mchezo kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Mwadui ya Shinyanga.

Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inaonesha kuwa ligi hiyo huko Mbeya kutakuwa na ‘derby’ kwa maana ya mchezo wa upinzani baina ya timu zinazotoka mkoa mmoja wa Mbeya ambazo ni Tanzania Prisons na Mbeya City utakaochezwa na Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Keshokutwa Jumapili Januari 29, mwaka huu kutakuwa na mchezo mwingine ambao Young Africans itacheza na Mwadui jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Majimaji ya Songea itasafiri hadi Mtwara kucheza na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Jumatatu Januari 30, 2017 kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

TFF YAITUPA RUFAA DHIDI YA SIMBA!

PRESS RELEASE NO. 242
RUFAA YA POLISI DAR ES SALAAM
TFF-HQ-1-1-1-1Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea rufaa kutoka Klabu ya Polisi Dar es Salaam dhidi ya Klabu ya Simba kuhusu kumchezesha Mchezaji Novalty Lufunga katika mchezo wao wa Raundi ya Tano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup 2017.
Madai ya Polisi ni kwamba Mchezaji Novalty Lufunga alioneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo kati ya Simba na Coastal Union katika mchezo wa Azam Sports Federation Cup 2015/2016 uliofanyika Uwanja wa Taifa, Aprili 11, mwaka jana.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa vigezo vya kikanuni katika uwasilishaji wake na hivyo kukosa sifa ya kusikilizwa. Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) na (2) ya Kanuni za Kombe la Shirikisho la Azam Sports HD.
Kanuni ya 18 (1) inasema: “Malalamiko yoyote kuhusiana na mchezo yawasilishwe kwa maandishi kwa kamishna wa mchezo au TFF sio zaidi ya masaa sabini na mbili (72hrs) baada ya kumalizika mchezo.”
Kanuni ya 18 (2) inasema: Ada ya malalamiko ni shilingi laki tatu (Tshs 300,000.00). Malalamiko yo yote yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada na kuwasilishwa nje ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.”
Hata hivyo, Shirikisho linapenda kutoa ufafanuzi kuhusu kadi nyekundu aliyopewa Mchezaji Novalty Lufunga katika mashindano ya Azam Sports Federation Cup 2016/2017.
Kwa utaratibu wa mashindano haya ambayo ni ya mtoano, adhabu za kadi (njano na nyekundu) zitolewazo uwanjani, zinakoma mwisho wa msimu wa shindano husika isipokuwa kadi hizo zikiongezwa adhabu ya kinidhamu (suspension) ambayo itafahamisha kwa klabu na mchezaji kwa maandishi.
Kadhalika, Kanuni ya 16 ya Kanuni za Kombe la Shirikisho Sehemu ya Tatu inaeleza wazi kuwa matumizi ya kanuni za ligi zitahusika maeneo yanayoruhusu uendeshaji wa shindano la mtoano.
“Adhabu zote zinazohusisha katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam HD zitahusisha na shindano hili tu,” inasema kanuni ya 16 (3) na (4).
KAMBI YA KILIMANJARO WARRIORS
Timu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 ‘Kilimanjaro Warriors’ inatarajiwa kuingia kambini Janauri 29, 2017 kwa ajili ya maandalizi ya awali ya kucheza mechi za kufuzu fainali za Olimipiki zitakazofanyika jijini Tokyo, Japan mwaka 2020.
Kambi hiyo ya wiki moja itafanyika kwenye Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambako pia kuna Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazoezi kulingana na program za walimu.
Tanzania haijapata kushiriki Michuano ya Olimpiki kwa upande wa mpira wa miguu jambo ambalo limeisukuma TFF kuona kuwa ni fursa ya mpira wa miguu kuchezwa hivyo inashirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kufanikisha mipango na taratibu.
Tanzania kwa sasa ina vijana wengi waliotokana na michuano ya Mradi wa kuibua na kukuza vipaji wa Airtel kadhalika na Cocacola ambao wamekuwa chachu ya maendeleo ya timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys.
Vijana hawa wa Airtel, Copa Cocacola na Serengeti Boys wataungana na baadhi ya vijana waliofanya vizuri kwenye Ligi ya Vijana wenye umri wa chini miaka 20 kutoka timu za Ligi Kuu ambao wamezaliwa baada ya tarehe 1 Januari 1997 ili kuunda kikosi imara cha awali kuelekea kufuzu kwa michuano ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo Japan, mwaka 2020.
Kwa kufuata utaratibu wa maandalizi ya Serengeti Boys na kwa kushirikiana na TOC timu hii itapewa mazoezi na michezo  ya kujipima nguvu ndani na nje ya nchi.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

VPL: DIMBANI IJUMAA, JUMAMOSI BIGI MECHI SIMBA-AZAM, DABI SOKOINE PRISONS-MBEYA, JUMAPILI MABINGWA YANGA NA MWADUI!

VPL-DTB-SITVPL, Ligi Kuu Vodacom, ipo kilingeni kuanzia Ijumaa kwa Mechi 1 na Jumamosi ni lukuki yake lakini Siku hiyo ‘Macho Kodo’ yapo Jijini Dar es Salaam kwa Bigi Mechi kati ya Simba na Azam FC na huko Sokoine, Mbeya kwenye Dabi kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City.

Ijumaa ipo Mechi moja huko CCM Kirumba Mwanza kati Ya Mbao FC na Ruvu Shooting Timu ambazo zimepishana Pointi 4 wakati Ruvu Shooting ikiwa Nafasi ya 8 na ina Pointi 24 na Mbao FC wapo wa 12 wakiwa na Pointi 20.

Jumamosi zipo Mechi 4 na mbili kati ya hizo zina majina moja ikiwa ni BIGI MECHI na nyingine ni DABI.

BIGI MECHI ipo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam kati ya Simba na Azam FC na DABI ni huko Sokoine Jijini Mbeya kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City.

Simba ndio Vinara wa VPL wakiwa mbele ya Azam FC, walio Nafasi ya 4, kwa Pointi 12.VPL-JAN25

Mbeya City, ambao wako Nafasi ya 6, wamecheza Mechi 2 zaidi ya Tanzania Prisons ambao wako Nafasi ya 9 wakiwa Pointi 4 nyuma yao.

Jumapili, Mechi pekee ni Jijini Dar es Salaam ambayo huenda ikapigwa Uwanja wa Taifa kama si Uhuru, ambapo Mabingwa Watetezi Yanga watakapokumbana na Mwadui FC.

Yanga wao wapo Nafasi ya Pili wakiwa Pointi 2 nyuma ya Vinara Simba na Mwadui FC wako Nafasi ya 10 wakiwa Pointi 21 nyuma ya Yanga.

VPL – Ligi Kuu Vodacom

Ratiba

Ijumaa Januari 27

Mbao FC v Ruvu Shoooting

Jumamosi Januari 28

Toto Africans v African Lyon

Simba v Azam FC

Tanzania Prisons v Mbeya City

Ndanda FC v Majimaji FC

Jumapili Januari 29

Yanga v Mwadui FC

Jumatatu Januari 30

Kagera Sugar v Mtibwa Sugar

JKY Ruvu v Stand United

TOKA TFF: REFA AFUTWA VPL, MWINGINE FAINI, YANGA FAINI, JAMHURI ‘STOPU’ KWA VPL, YULE VENANCE LUDOVIC…..!!

MATUKIO MBALIMBALI YA LIGI KUU YA VODACOM

TFF-TOKA-SITShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemwondoa Mwamuzi Hussein Athuman kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.

Mwamuzi Hussein Athuman kutoka Mkoa wa Katavi alichezesha mchezo namba 150 uliozikutanisha timu za Majimaji ya Songea na Young Africans ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Kadhalika Young Africans imepigwa faini ya jumla ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yao kutoingia vyumbani, na pia kutumia mlango usio rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14 (13) na (14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mwamuzi Ngole Mwangole: Mwamuzi huyo wa kati, Ngole Mwangole wa Mbeya amepewa barua ya onyo kali na kumtaka aongeze umakini wakati akichezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kubainika kukataa bao lililoonekana kutokuwa na mushkeli la Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Licha ya kujitetea, lakini kamati haikuridhika na maelezo yake. Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa Bw. Mwangole alikuwa Mwamuzi Bora wa msimu uliopita (2015/2016) na hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kuonekana kufanya uamuzi uliokosa umakini wakati akichezesha, TFF imeamua kumpa onyo.

Mechi namba 141 (Mwadui FC vs Kagera Sugar). Beki wa Kagera Sugar, Godfrey Taita anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi baada ya mechi na kuwatolea lugha chafu na vitisho kabla ya benchi la ufundi la timu yake pamoja na askari polisi kuingilia kati na kudhibiti kadhia hiyo.

Mechi namba 151 (Mtibwa Sugar vs Simba). Baada ya mchezo kumalizika mashabiki waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. Pia kamera ya Azam Tv upande wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.

Vilevile sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika hali mbaya ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

TFF imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia kilichangiwa na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya kusimamia usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika kutazama mechi.

Hivyo, Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ili kutoa fursa kwa wamiliki kufanya marekebisho makubwa kwenye eneo la kuchezea (pitch), na pia askari polisi kupata maelekezo ya kutosha ya jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama mechi. Kama marekebisho hayatafanyika, uwanja huo hautatumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

LIGI DARAJA LA KWANZA

Mechi namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 35 (Kiluvya United vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman Mzongela anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka kuwapiga wakati wa mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha chafu waamuzi na Msimamizi wa Kituo.

Mechi namba 36 (African Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti United, Andrea Mbuguni amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba moja.

Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC, Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Wachezaji wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.

Lakini pia Mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.

Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao.

Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza.

Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Makamishna.

Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.

Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo ambayo tayari yamekamilika.

Mechi namba 39 (Polisi Dar vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 33 (KMC vs JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa lugha chafu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 38 (Kimondo FC vs Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji wake wajiangushe ili kupoteza muda.

Mechi namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi; Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana wakiwa uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo, Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea vyumbani baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.

LIGI DARAJA LA PILI

Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 18 (Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mechi namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).

Mechi namba 16 (Sabasaba vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali kutokana na washabiki wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 17 (Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 35. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 19 (Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake kuingia uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya Ligi Daraja la Pili.

Malalamiko mbalimbali

Malalamiko ya klabu za Mwadui FC na Polisi Morogoro kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji wa Stand United, Kheri Mohamed Khalifa na wachezaji wawili wa Njombe Mji kucheza mechi bila leseni yamepelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.

Pia maombi ya klabu ya Singida United kuhusu kubadilishiwa Mwamuzi kwenye mechi yao yamepelekwa Kamati ya Waamuzi, wakati maombi ya Alliance Schools, Friends Rangers FC, The Mighty Elephant na Kariakoo FC yanayohusu uendeshaji yanashughulikiwa na Sekretarieti ya TPLB.

Kuhusu JKT Ruvu

Katika mengineyo, Kamati ilipitia maombi ya timu ya JKT Ruvu Stars FC kubadilisha uwanja wake wa nyumbani kutoka Mabatini mkoani Pwani hadi Mkwakwani mkoani Tanga kutokana na wachezaji wake 12 wa kikosi cha kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi mkoani Tanga.

Ombi hilo limekubaliwa. Kwa mujibu wa Kanuni ya 6(6) ya Ligi Kuu, TFF/TPLB zina mamlaka ya mwisho kuhamisha kituo cha mchezo kwa sababu inazoona zinafaa na kwa wakati husika.

Kuhusu Mchezaji Venance Ludovic

Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajiwa kukaa wiki ijayo kusikiliza malalamiko dhidi ya usajili wa wachezaji mbalimbali akiwemo mchezaji Venance Joseph Ludovic.

MECHI ZA KESHO AZAM SPORTS FEDERATION CUP

Mechi za raundi ya tano ya mechi za Kombe la Shirikisho la Azam 2016/17 (Azam Sports Federation Cup - ASFC), zitaendelea kesho Jamatano Januari 25, 2017 kwa timu za Singida United na Kagera Sugar kucheza kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Mchezo mwingine utakaozikutanisha timu za The Mighty Elephant ya Songea na Mashujaa ya Kigoma katika mchezo utakaofanyika Uwanja Majimaji mjini Songea.

RATIBA MECHI ZA KESHO LIGI YA WANAWAKE

Ligi ya wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano Januari 25, mwaka huu kwa michezo sita – mitatu kwa kila kundi.

Kundi A, linatarajiwa kuna na mchezo kati ya JKT Queens Dar es Salaam na Mburahati Queens pia ya jijini utakaofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Ilala.

AZAM SPORTS FEDERATION CUP – RAUNDI YA 5: KUANZA JUMAMOSI, YANGA NA ASHANTI HUKO UHURU, DAR

>JUMAPILI SIMBA NA POLISI DAR!

AZAM-ASFC-CUPRaundi ya tano ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam 2016/17 (Azam Sports Federation Cup - ASFC), utaanza Jumamosi Januari 21, 2017 kwa timu za Majimaji na Mighty Elephant za Songea kucheza kwenye Uwanja Majimaji mjini Songea.

Ratiba ya ASFC inaonesha kwamba timu za Alliance na Mbao za Mwanza zitacheza pia keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wakati Young Africans itacheza na Ashanti United kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Jumapili Januari 22, mwaka huu Ruvu Shooting itacheza na Kiluvya United kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Toto Africans itacheza na Mwadui ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza huku Simba itakipiga na Polisi Dar kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kadhalika Mbeya Warriors ikicheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Jumatatu Januari 23, mwaka huu Stand United itacheza na Polisi Mara kwenye Uwanja wa Karume Mara wakati Azam itacheza na Cosmopolitan kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Ndanda itacheza na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Jumanne Januari 24, mwaka huu Mtibwa Sugar itacheza na Polisi Moro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Kurugenzi ya Iringa itacheza na JKT Ruvu huko Mafinga huku Mbeya City ikipangwa kucheza na Kabela City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya ilihali Madini na Panone zitacheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Januari 25, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Singida United na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati mchezo mwingine utakaozikutanisha timu za African Lyon na Mshikamano utapangiwa tarehe mpya. Mechi hiyo imepangwa kufanyika Uwanja wa Uhuru.

IMETOLEWA NA TFF

AZAM SPORTS FEDERATION CUP – RAUNDI YA 5

Ratiba:

Januari 21, 2017

Alliance v Mbao (CCM Kirumba, Mwanza)

Maji Maji v Mighty (Maji Maji, Songea)

Yanga v Ashanti United (Uhuru, Dar es Salaam)

Januari 22, 2017

Ruvu Shooting v Kiluvya United (Mabatini, Mlandizi)

Toto Africans v Mwadui FC (CCM Kirumba, Mwanza)

Simba v Polisi Dar (Uhuru, Dar es Salaam)

Mbeya Warriors v Tanzania Prisons (Sokoine, Mbeya)

Januari 23, 2017

Stand United v Polisi Mara (Karume, Musoma)

Azam FC v Cosmopolitan (Azam Complex, Chamazi)

Ndanda FC v Mlale JKT (Nangwanda Sijaona, Mtwara)

Januari 24, 2016

Mtibwa Sugar v Polisi Moro (Jamhuri, Morogoro)

Kurugenzi FC v JKT Ruvu (Mafinga, Iringa)

Mbeya City v Kabela City (Sokoine, Mbeya)

Madini v Panone (Sheikh Amri Abeid, Arusha)

Januari 25, 2017

Singida United v Kagera Sugar (Namfua, Singida)

Tarehe Kupangwa

African Lyon v Mshikamano (Uhuru, Dar es Salaam)